Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia natumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama Bungeni siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Urambo kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya ya kuleta maendeleo nchini. Na wakati huohuo niwatakie kila la heri Wizara ya Fedha, ikiongozwa na Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote, kwa sababu kazi ya bajeti si mchezo, ni kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama wananchi wa Urambo tunangojea mradi wa maji kwa hamu sana. Kwa hiyo, tunaomba bajeti hii iwezeshe mradi wa maji ya kutoka Lake Victoria kuja Urambo kuanza kwa sababu tumeusikia kwa muda mrefu, tunaomba sasa mradi huo uanze. Kwa hiyo, lini Serikali itaanzisha mradi huu wa maji ili na sisi tufaidike na maji kwa sababu ya shida ya maji tuliyonayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili ni shida ya nishati. Tuna kituo cha kupoozea umeme kinachojengwa Urambo ambacho tunaamini kitatupunguzia shida ya umeme wilayani kwetu. Lini kituo cha kupoozea umeme, TANESCO substation, kitaanza kufanya kazi ili na sisi tupunguze matatizo ya nishati tuliyonayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huohuo, naipongeza Serikali kwa jitihada kubwa ya kujenga shule, madarasa tumeona mengi, lakini pia vituo vya afya na hospitali. Ombi langu leo kwa niaba ya wananchi wa Urambo ni kwamba tuna uhaba mkubwa sana wa wafanyakazi. Tunaomba bajeti hii tutakayoipitisha, kwa njia moja au nyingine iwezeshe kupata wafanyakazi shuleni (walimu), na wafanyakazi katika vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano shule za msingi tunahitaji walimu 627. Kwa upande wa sekondari tunahitaji walimu 78 ambao tunaamini watatusaidia angalau kupunguza uhaba wa walimu. Kwa upande wa afya ndiyo kabisa tuna uhaba wa wafanyakazi 476. Tunaomba bajeti hii tutakayoipitisha ituwezeshe kupata wafanyakazi wengi zaidi ili yale matunda ya maendeleo kwa kupitia sekta hizo mbili yaweze kuzaa matunda vizuri kwa manufaa ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara; katika mambo ambayo yanachangamsha uchumi kwa haraka sana ni ujenzi wa barabara. Na tumeshuhudia sisi watu wa Tabora baada ya hii Barabara ya Manyoni – Chaya – Tabora kukamilika, hali ya wananchi imebadilika kule ambako barabara inapita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo naiomba Serikali, kwa kupitia bajeti hii, ili kuamsha maendeleo ya kiuchumi Wilayani Urambo, tunaomba barabara ya Kahama itoke Kahama iwe ya lami kwenda Ulyankulu – ni kama kilometa 50 tu – ikitoka Ulyankulu inakuja Urambo, kilometa kama, yaani hata 40 hazifiki. Halafu ukitoka Urambo kwenda Usoke ni lami, ukitoka Urambo kwenda Tutuo ni kama kilometa 70 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukipiga hizo lami kilometa 120 tayari watu wa Kahama mnaoniangalia ninyi Waheshimiwa Wabunge, mtakuwa mnatoka Kahama mnakuja Ulyankulu, mnakuja Urambo, mnakwenda Tutuo, mnakwenda Sikonge, moja kwa moja mpaka Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshukuru Waziri wa Fedha ameniona, ni kweli Kahama – Ulyankulu – Urambo – Usoke – Tutuo – Sikonge – Mbeya, ninyi Waheshimiwa Wabunge wa Shinyanga mtakuwa hampitii Tabora, mtapunguza kilometa 70, mtakuwa mnapita kwetu Urambo ninyi, mnapunguza urefu wa njia. Kwa hiyo, tunaomba hii barabara ijengwe safi sana, hata Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba anakubali kwamba barabara ni safi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumzia ni lile ambalo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wameliongelea sana; suala la wafanyakazi kupata haki zao. Nina majina ya walimu hapa, ambao walipandishwa madaraja mishahara yao haikurekebishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walipostaafu sasa kwenda kufanya mahesabu ya pensheni zao imekuwa ni vigumu kwa sababu mishahara ile ilikuwa haijarekebishwa. Kwa hiyo, mtu anapanda daraja lakini mshahara haurekebishwi, anapostaafu sasa kunakuwa na mapungufu ya hela kwa sababu mshahara wake haukurekebishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini; nasema kwa ukweli nina majina ya walimu ambao walitoa hela zao wenyewe ili kuwezesha mafao yao yaweze kufanyiwa kazi. Kwa sababu wanaambiwa mwajiri wako alikuwa hajaleta hela kwa hiyo, anafanyiwa mahesabu kwa kupitia mshahara wa kwanza kabla hajapandishwa. Sasa yeye ndio anabaki anadai Serikali kile kiasi cha fedha alichoongezewa ili afanyiwe mafao yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali yeti sikivu wafanyakazi wanaopandishwa madaraja mishahara yao irekebishwe ili waweze kufanyiwa mahesabu vizuri pale wanapostaafu. Nina imani kabisa na Serikali yetu inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi, na nahodha wetu akiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, suala hili tunapolizungumza tunaonekna kwamba linafanyiwa kazi, lakini bado kabisa. Nina ushaidi utakapotakiwa naweza kutoa nina jina la mwalimu hapa ambaye ametoa yeye mwenyewe fedha zake ili afanyiwe mahesabu ya pensheni; inakuwa siyo haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo, kwa hao naomba sana Serikali izingatie, na hasa naona kabisa Mheshimiwa Waziri alivyojipanga hii bajeti itakwenda vizuri, ili yale mapungufu ambayo tunayataja sisi Wabunge yakifanyiwa kazi basi nchi yetu itaendelea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)