Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kinondoni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika hali ya uchumi wa Taifa na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha ujao, 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kabisa moja kwa moja niseme naunga mkono hoja hii, na wala sitasubiri mpaka mwisho wa mazungumzo yangu, nataka niseme mapema. Ninatamka hivi kwa sababu kule Kinondoni, na ndugu zangu wa Kinondoni na wananchi wa Kinondoni, tunaiona bajeti hii kwamba ni bajeti ambayo ina maono na matarajio ya wana Kinondoni, kwa hali kubwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hiyo, nataka nimpongeze kwanza Mheshimiwa Rais. Na mimi sichoki kumpongeza kwa sababu haya ambayo nitakwenda kuyazungumza yanaakisi pongezi zangu kwa nini nampongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze mwananchi mwenzangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, na msaidizi wake, Mheshimiwa Hamad, hawa watu wanafanya kazi vizuri. Nawapenda kwa sababu wako creative, wanatuletea mambo ambayo yanamgusa Mtanzania wa kawaida kila siku. Na haya ndiyo maono ya Mheshimiwa Rais, mnayatekeleza kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini nasema nataka Watanzania maana yake leo nazungumza na Taifa hili nikitoka Bungeni, Watanzania wanisikie huko. Kwamba pale Kinondoni kuna Kata inaitwa Kinondoni, ndiyo kata ambayo inachukua jina la jimbo, lakini jina la Wilaya ya Kinondoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kata ile kwa miaka yote hii tangu tupate Uhuru haijawahi kuwa na secondary school. You can imagine. Yaani hebu fikiria kata iko mjini lakini secondary school ya Serikali haikuwa nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimshukuru Mheshimiwa Rais, mwaka 2021 tukaja na ujumbe wetu hapa kuwaona Mawaziri wa TAMISEMI kuwaeleza matatizo tuliyonayo pale Kinondoni, wakatupatia shilingi milioni 600. Tunajenga shule ambayo ni afadhali imechelewa lakini ni shule ya kisasa. Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hilo tu; hatukuwa hata na zahanati au kituo cha afya pale katika kata kubwa kama ile. Leo hivi tuna kituo cha afya cha kisasa kasoro tu mtutafutie madaktari wa kutosha na wauguzi, ili kisionekane kinapwaya, kitimie kabisa kile kituo cha kisasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka niipongeze Serikali, ingawa hapa kuna tatizo kidogo fedha ambazo Serikali imetupatia nilivyokuja kuomba fedha hapa milioni 600 zikapelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya shule ya Sekondari ya Tandale. Mwaka 2021, Mheshimiwa Waziri na Mawaziri miliopo hapa, fedha zile hazikujenga secondary school.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tandale ni mahali ambapo pana idadi kubwa sana ya wananchi, na hata mahitaji ya elimu kwa watoto wanaokaa pale, watoto maskini. Serikali ilifanya kitu wanaita household budget survey kuangalia hali ya umaskini inaletwa na nini. Kaya ambazo hazina watu ambao wamekwenda shule, wamepata elimu ili iwasaidie katika maisha yao huwa wanatengeneza umaskini, hasa katika maeneo ya mjini, kwa mujibu wa bajeti hii inavyoeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kule tumepeleka hela kwa ajili ya kujenga secondary school, secondary school haijajengwa. Natamani Serikali ichunguze sababu zilizofanya secondary school ile isijengwe na fedha zile zikapelekwa kwenye jimbo lingine. Hili jambo linanichukiza sana, linatia doa kazi nzuri ya mama Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifanyie utafiti kwa nini secondary school Tandale, mahali ambapo pana primary schools tatu bado wanashindwa kuweza kupata secondary school.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niipongeze Serikali kwa kumalizia Mto Ng’ombe. Sasa hivi maeneo yale ya Magomeni, Ndugumbi na Makumbusho mafuriko hayapo, mmetusaidia sana kuokoa maisha ya wananchi pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tunalisubiri kwa hamu ni ujenzi wa Mto Msimbazi pamoja na Daraja la Magomeni. Hivyo watu wa Kinondoni wamekaa mkao wa kula wanasubiri hayo mambo. Nataka Mheshimiwa Waziri aje tu awatoe wasiwasi kwamba mradi wa Mto Msimbazi unaendelea kama ulivyopangwa. Ninajua sasa hivi watu wanalipwa fidia, kwa wale ambao watapisha mradi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niipongeze tena Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kukusanya mapato. Serikali imeonesha kwamba ukiangalia uwiano wa kodi na Pato la Taifa imejitahidi imefikia asilimia 12.5, hongereni sana. Lakini ningependa nione kwamba Serikali yangu inakusanya angalau asilimia 15 ya Pato la Taifa kama kodi kwa sababu huo ndio uwiano ambao utatusaidia kuondokana na bajeti deficit.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nchi kama Lesotho wanakusanya asilimia 30.8 ya Pato la Taifa, nchi kama Namibia asilimia 28.27, Zambia wanafanya vizuri asilimia 16. Ninapenda nione tunaweza tukajifunza mambo gani kutoka kwenye nchi hizi ili tuweze kukusanya mapato ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo nilikuwa nikiliangalia halinipi furaha, nalo linahusiana na matumizi ya EFD. EFD inatusaidia sana kukusanya VAT, EFD ndiyo iko kwenye story ya kwenda kununua bidhaa ukinunua unaambiwa una risiti…ohoo!
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Hitimisha Mheshimiwa.
MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba niiambie Serikali ifanye utaratibu wa kutumia mifumo. Elimu ya dai risiti toa risiti haitusaidii. Tangu VAT imeanzishwa mwaka 2010 mpaka leo miaka kumi na tatu bado tunaimba wimbo huo huo na watu hawatoi risiti. Sasa ningeomba mtumie mifumo ya stock verification na stock controls ili kuweza kuondokana na shida hii ya utoaji wa risiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana.