Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kusema naunga mkono hoja. Ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja na mapendekezo mengi na kwa kuchukua maoni ya Waheshimiwa Wabunge; na hasa katika maeneo ambayo tuliyasema kwa hisia kubwa. Kwa hiyo nianze kwa kuunga mkono hoja lakini nianze kwa kuipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri ambayo inafanya kwenye Jimbo langu la Geita na Mkoa mzima wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu kubwa hapa ni kushauri namna ya kutafuta fedha halafu tukatumie fedha ambazo tumeziomba kwa miezi mitatu. Mimi sasa nianze na eneo la madini. Kwa mujibu wa taarifa yako eneo la madini limekuwa kwa takribani asilimia 10.6; haya ni mafanikio makubwa sana. Lakini nina mapendekezo na ushauri katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza niishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye maeneo ya CYP. CYP tulizonazo ambazo ni za Serikali zilijengwa kama vile za majaribio. Sasa imethibitika kwamba wachimbaji wengi wanahitaji CYP nyingi ili kuweza kuongeza tija. Kwa hiyo Ofisi yako, Wizara yako itoe fedha nyingi kwa sababu kwa mujibu wa takwimu za sasa wachimbaji wanachangia takribani asilimia 40 ya dhahabu ambayo inauzwa nje ya nchi. Kwa hiyo hili ni eneo ambalo tunaomba Serikali iweze kuwekeza zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili katika eneo hili, tuna Watanzania wenzetu na raia wa nje wengi ambao wamekuja wakachukua PL, wamechukua PL wakatokomea; wengine wana miaka kumi, wengine miaka mitano na wengine miaka 20. Kila mwaka wanachokifanya ni kulipia na kujificha. Nimetoa mapendekezo katika michango yangu huko nyuma, kwamba wengi wanafanya kama vile kutegesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije na mkakati, mifumo ituambie kwamba huyu mtu ana PL hii kwa takribani miaka kumi na haizalishi na iweke ukomo wa mtu kukaa na PL bila kuitumia. Kwa sababu kama kuna wachimbaji wadogo wanachangia kwa asilimia 40 lakini tunaruhusu mtu anakaa miaka 20 na PL haitumii, hafanyi nini, wakiingia wachimbaji wadogo wanaenda kufukuzwa ni sawasawa na kusema kwamba fedha tunazo lakini tumeshindwa kuzitumia. Kwa hiyo mimi nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tubadilishe utaratibu. Wachimbaji lazima wanapochukua PL watoe mpango kazi na waitumie wasipo itumia Wizara ipewe mamlaka ya kubadilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili nakushukuru sana kwa kufanya marekebisho ya kodi, tulikuwa na mgogoro mkubwa sana kwenye kodi. Wachimbaji kila wanapokwenda kuuza walikuwa wanabishana na TRA. TRA akiona umeuza bilioni moja anajua hii ni faida, lakini palikuwa na gharama kubwa. Nakushukuru kwa asilimia mbili ambayo umeleta. Sasa ombi langu, mimi nimefanya biashara kabla ya kuwa Mbunge; tumepitisha asilimia mbili watu wako watakapoona watu wanafanya biashara na turn over inakuwa kubwa watageuka tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba ofisi yako na watendaji wako waheshimu mambo haya ili turuhusu wachimbaji na watu wengine waweze kutumia mifumo ya kibenki. Kwa sababu wachimbaji walikuwa hawawezi kutunza hesabu; wachimbaji kwa nature ya kazi yao wanafanya kazi ngumu mpaka kuja kufika kwenye kuuza mazao kabla ya kuanza kupata faida. Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo mimi nakushukuru sana hapa; lakini naomba sana isije ikabadilika baada ya muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, tunakubaliana kwamba katika nchi hii tumezungukwa na mito, maziwa na maeneo mengine mengi kwa ajili ya kilimo na mifugo. Naomba niishauri Serikali; bado hatujatumia vya kutosha uwepo wa maziwa, mito, bahari na eneo la mifugo. Nimeangalia kwenye maeneo ambayo umeyawekea msisitizo; umeonesha kwamba unakwenda kufanya tathmini na kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais. lakini ukiangalia vizuri nature ya failure ya kwenye mifugo inategemea na uwezeshaji ambao mnaupeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ranch saba Tanzania, ukienda pale Mwabuki utagundua kwamba hawa watu wako dhofulhali, wako pale wana mifugo ambayo imeshakaa miaka. Ukienda hapa Kongwa utaona jinsi shamba lilivyochakaa, lakini utashangaa ukija kwenye bajeti; hawa wanamiliki takriban watumishi 2,000 nchi nzima. Ukija kwenye bajeti leo kurugenzi inayowasimamia ina fedha nyingi kuliko watu walio kwenye sekta za utafiti. Sasa utaona hapa hakuna seriousness. Kama tunataka kufanya mabadiliko lazima tupeleke fedha nyingi zaidi huku kwenye ranch ili waweze kuzalisha mitamba mingi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye taarifa, wamezalisha mitamba 1,000. Mitamba 1,000 kwa nchi ya watu milioni 60 huwezi ku-transform ng’ombe milioni 36. Wanatakiwa wapewe fedha nyingi ili wafanye mabadiliko. Tuwatoe wafugaji kwenye mifugo hii midogo midogo ambayo ina kilo ndogo, na wanakimbizana nayo kwenye mapori na Serikali ilhali maeneo hakuna tuwapeleke kwenye kufuga mifugo ya kisasa. Jambo hili haliwezi kufanikiwa kama Wizara haitoi fedha za kutosha. Tutoe fedha za kutosha kwenye utafiti na kwenye miundombinu. Tupeleke wataalam halafu wao wasambaze hii mitamba bora kwa wafugaji wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kwenye uvuvi. Ukiangalia vizuri tumeanza kuzungumza uvuvi kwa miaka mingi. Wewe umesema umetoa exemption ya tozo na VAT kwa wanao-export; lakini nasoma kwenye taarifa yako sioni wapi umehamasisha uvuvi kwa kutoa kodi kwenye fishing gears. Kwa sababu kinachosababisha sasa hivi tunauza kidogo ni gharama ya uwekezaji kwenye uvuvi. Ili kuongeza uzalishaji wa samaki ziwani, Ziwa Victoria au baharini unahitaji kuwa na zana za kisasa. Tunahitaji kuwa na out body engine, tunahitaji kuwa na boti zenye fiber, watu wanahitaji kuwa na fish finders nets.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo huwezi ukaongeza uzalishaji kwa sababu utakuwa una wavuvi wadogo wadogo wanaokomea mlingotini. Tumezungumzia mkakati wa Serikali wa kuanzisha boti za uvuvi leo takriban ni mwaka wa tatu ama wa nne lakini hatujaona productivity yeyote inayozungumzwa hapa. Kwa hiyo maana yake ni nini? Tunaendelea kuwategemea wavuvi wadogo wadogo ambao kwenye kodi hapa ni kama vile wamekuwa marginalized; Serikali haikuonesha kwamba wanatakiwa wakuzwe walelewe waweze kuwa productive kwenye nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tunataka kuongeza uzalishaji kwenye maziwa, na hasa kwenye kilimo cha Samaki Ziwa Victoria na maeneo mengine. Dunia nzima sasa hivi wanapata samaki wengi kwenye cages lakini its too expensive ku-invest. Hii ni kwa sababu mwanzo utahitaji zaidi ya milioni 50. Hakuna mvuvi wa Tanzania ambaye anaweza ku-invest milioni 50 kwenye cages akaanza kupata fedha baada ya mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana.