Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niwe mmoja wa wachangiaji katika Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote nianze kwa kuipongeza Serikali kwa bajeti hii nzuri pamoja na utekelezaji wa bajeti iliyopita, kwa sababu tunakwenda mwishoni mwa utekelezaji wa bajeti ya 2022/2023. Na Mheshimiwa Waziri nikupongeze, yako mambo yamekwenda Jimboni kwetu ni mazuri mazuri. Hii yote imesababishwa na Mheshimiwa Rais lakini na wewe mshauri wake kwa upande wa fedha, umemshauri vizuri. Sisi tuleteeni fedha kwa sababu wananchi tuliwaahidi maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza haraka haraka, kwanza mimi nianze kwa kuipongeza Wizara ya Kilimo. Mwaka huu imetusaidia, wakulima wengi waliitikia mwitikio mkubwa katika kujiandisha upatikanaji wa mbolea ya ruzuku na haya yote yalichangia baada ya Mheshimiwa Rais kuweka bilioni 150 kwenye mbolea ya ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo lakini bado tuna changamoto; changamoto iliyopo kama tumeweza kuweka ruzuku kwenye mbolea sasa Serikali ije na mpango mkakati wa kuweka ruzuku kwenye mbegu hasa za alizeti na mahindi ili sasa ziweze kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mzalishaji kama umempa mbolea, halafu akaenda kuweka mbegu zisizo bora ni sawasawa na bure. Kwa hiyo, nimshukuru Mheshimiwa Waziri nilipata tani moja, kama kilo 1,000 za alizeti, tayari nimekwenda kuzigawa kule na zimeleta tija sana. Kwa hiyo, mwaka huu aniongezee wakulima watalima sana, anipe tu tani 10 nikalime peke yangu kule Igalula na watu wameitikia kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Wizara ya Kilimo kuwa imefanya kazi vizuri, lakini niipongeze Serikali imeendelea kulipa fidia kwa wanaoidai Serikali. Niiombe Wizara ya Fedha, pamoja na changamoto nyingi wanazokabiliana nazo za kifedha, lakini kuna wananchi ambao wamepisha maeneo ili kupisha miradi ya Serikali wakiwemo wananchi wa Kata ya Kizengi ambao wanajengewa mzani pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANROADS waliwambia wasiendeleze yale mashamba, lakini hadi leo bado hawajawalipa. Ni hela ndogo ambayo haifiki hata milioni 100. Naomba Mheshimiwa Waziri, akitoka hapa akawalipe tu ili waweze kupata fedha zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, waliopitiwa na Mradi wa SGR. Kuna wakazi zaidi ya 30 ambao wamepitiwa na Mradi wa SGR kwa kigezo cha kwamba waliifuata reli (wako ndani ya mita za reli). Sasa, wale wakazi wamekaa pale zaidi ya miaka 30 hadi miaka 40. Nilifika hapa na hoja na nimwombe Waziri, kwa sababu Wizara ya Fedha ndio inayohusika na niliongea na Waziri wa Ujenzi, akaniambia niongee na Waziri wa Fedha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, niombe kama hawa hawawezi kuwalipa ardhi, basi wawalipe majengo ili waweze kupata fidia kidogo ili wakajenge nyumba kuliko kuwabomolea na wawaache. Vile vile, Serikali ya Mama Dkt. Samia haitaki kuwaonea wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye mambo ya kitaifa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kujenga na kuleta maendeleo ni lazima wananchi tulipe kodi na hili Mheshimiwa Waziri amekuwa anasisitiza na Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia amekuwa akisisitiza sana. Mheshimiwa Waziri, jambo ambalo tunatakiwa tulifanye, la kwanza, Waziri anatakiwa akae na management ya TRA. Customer care ya TRA sio nzuri. Leo wanalazimisha watu wakalipe kodi, lakini wanavunjwa mioyo kwa sababu ya customer care ya TRA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mwananchi anatoka zaidi ya kilometa 200 pengine zaidi ya kilometa 250, anakwenda pale TRA siku ya kwanza ataambiwa mfumo, siku ya pili ataambiwa anayetoa TIN number ana msiba, siku ya tatu anaambiwa sijui kuna kikao gani. Sasa huyu ametembea kilometa 200 anakula na analala, ndio maana watu wengi hawalipi kodi kwa sababu ya uzembe wa watumishi wa TRA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali waongeze watumishi wa TRA, lakini wawe na kauli nzuri. Hata kama kuna changamoto ya mifumo waangalie namna ya kuwasiliana na mteja aruhusiwe kwenda halafu mfumo ukikaa vizuri wawasiliane ili aweze kuja kufanya usajili na baadaye awe mlipakodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linakera, leo ili uweze kukadiriwa, kwanza unakadiriwa hatua ya kwanza na baadaye mnatengeneza hesabu unapeleka. Leo wanatengeneza risiti na wanasema tudai risiti na kweli watu wanadai risiti, lakini risiti zao zinakaa wiki mbili zinafutika. Sasa baadaye akija kuniambia nimeuza mauzo ya bilioni tatu, anasema nilete risiti, risiti zenyewe zimefutika kwa zaidi ya bilioni moja. Baadaye anakuja kumpigia tena kodi mfanyabiashara kwa ile hela ambayo anasema risiti yake haijapelekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali wakae na wataalam, mtu akifanya manunuzi inapoingizwa TIN number kwenye manunuzi yake, basi iwe reflected moja kwa moja TRA, iseme tarehe fulani ulinunua kitu cha milioni 200. Kwa hiyo, hesabu inakuja moja kwa moja ili kama akileta mahesabu, alete yale matumizi ambayo aliyafanya na ambayo hayajapita kwenye TIN number ikiwemo Payee ya mishahara na matumizi mengine ya kawaida ili a-submit pale wamtolee hesabu zao, kuliko sasa hivi unamwambia mfanyabiashara ndani ya mwaka mzima aandae risiti zake ambapo unakuta risiti zimefutika au zimepotea, baadaye TRA hawaelewi wanaanza kumpigia tena kodi ambazo sio rafiki kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri mwaka 2022 alikuja hapa na bajeti nzuri sana na akasema hivi anakwenda kubana matumizi ya Serikali. Nimwambie tu sehemu ambayo anaweza kusaidia Serikali kubana matumizi ni riba za wakandarasi. Hebu waliangalie. Kwa mwaka tunapoteza zaidi ya bilioni 800 kwenda trilioni moja. Sasa hizi fedha ukizi–calculate tunakwenda kuwapunguzia wananchi mzigo. Kwa hiyo, riba za wakandarasi Waziri akizidhibiti vizuri na kupunguza ukiritimba ulioko kwenye Wizara yake na watumishi wake wakawa weledi wa kulipa kwa wakati, nadhani haya mambo hayatokwenda kwa namna hii inavyokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku tunalalamika hapa fedha tumekosa, lakini fedha za riba zinapatikana na wanakwenda kulipa kwa wakati, lakini fedha za kwenda kwenye matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo kwa nini zinachelewa? Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri ang’ang’ane hapo hapo, abane matumizi lakini abane riba zisiendelee kupatikana katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nataka nichangie, takwimu ya sensa ya mwaka 2022 ilionesha Watanzania tuko milioni 62, lakini majengo yako milioni 14. Leo amekuja na bajeti ambayo inakwenda kuongeza tozo kwenye vifaa vya ujenzi hasa cement. Sasa ukiangalia kwa Takwimu kila nyumba moja wanaishi Watanzania wa nne. Leo tunakwendaje kuwasaidia Watanzania kujenga nyumba zao kuwa nyumba bora ambazo sisi wenyewe Serikali tunatoa maelekezo? Kwa hiyo, niombe hii tozo ambayo tunakwenda kuiweka kwenye cement haiendi kuwasaidia wananchi wetu wa kipato cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali iangalie namna bora ya kuongeza hizi tozo katika bidhaa muhimu ikiwemo chakula hebu tuangalie kuweka msamaha. Ndio maana Watanzania hapa kuna wakati huwa wanajiuliza kwa nini makampuni makubwa yanayotoka nje yanasamehewa misamaha mingi ya kodi, lakini sisi wa ndani huku tunabanwa sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)