Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mchango wangu utakuwa katika maeneo machache, nikijielekeza katika pongezi, lakini sehemu kubwa itakuwa ni eneo la madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kama ilivyo ada, nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake, lakini nafarijika sana, kuna huu mradi mkubwa wa TACTIC mara ya mwisho Serikali imetoa tangazo, naamini kwa maana ya Mji wa Mpanda, Manispaa ya Mpanda tunakwenda kunufaika na mradi huu wa TACTIC ambapo tangazo limetolewa. Tuko kwenye awamu ya pili, zaidi ya kilometa 15 za lami zinakwenda kutengenezwa katika Mji wa Mpanda, zaidi ya kilometa 30 kutoka Mwamkulu – Kakese - Misunkumilo, hili ni jambo jema. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye msukumo wa kuzisukuma fedha hizi kwenda huko, usisite tafadhali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kama haitoshi, naiongelee upande wa reli. Tunayo reli yetu kwa maana ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda. Kuna zaidi ya Shilingi bilioni 379.3 zinapelekwa huko kuimarisha reli ile. Siyo hilo tu, wanakwenda kutujengea kituo cha kupumzikia abiria cha kisasa katika stesheni yetu ya Mpanda. Mheshimiwa Waziri, katika hili, utakapofika muda wa kuzisukuma fedha huko, naomba naomba sana. Ukanda huu wa kwetu, mkitusaidia kwenye maeneo hayo tutaendelea kujikita kwenye kusukuma kilimo mazao mbalimbali na kuyaleta kwa walaji huku. Tumebahatika, kwani maeneo yetu yana ardhi nzuri na rutuba nzuri, kwa hiyo, mnapotuletea miundombinu, nasi tunahangaika kuwaleteeni ninyi wenzetu huku ambapo wakati mwingine hali ya hewa ni mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, nimeona kuna ununuzi wa kandarasi za ujenzi katika maeneo ya meli tatu ikiwa ni pamoja na Ziwa Tanganyika. Naomba sana, Ziwa Tanganyika kama chanzo cha mapato kinachotuunganisha na hizo nchi ikiwa ni Kongo, Burundi au Zambia, kandarasi hii ya ununuzi wa meli kwenye ziwa hilo ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema, naomba sana fedha hizo zielekezwe huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema sehemu kubwa nitajielekeza kwenye suala la madini. Naomba sana, najua Serikali inatamani kupata mapato, huko nyuma wachimbaji tuliwahi kuwa na mkutano mkubwa, tukaiomba Serikali kwamba namna pekee ya kuisaidia Serikali, ipunguze utitiri wa tozo na kodi katika eneo la madini. Nami nikueleze Waziri wa Fedha, nakuomba sana, mimi bahati nzuri ni mchimbaji, kwa hiyo, nikiyaongea haya, naongea yale ambayo wakati mwingine tumekuwa tukiyafanya muda wote. Hakuna mtu anakimbia suala la kulipa kodi na vitu vingine vya namna hiyo, lakini nilichokuwa naomba sana, kwanza hebu ziangaliwe kanda tofauti za uchimbaji. Wako wenzetu wa kanda ya mwanza, Shinyanga, wako wenzetu wa Chunya huko, uko ukanda mwingine kama huku kwetu Mpanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukizungumzia kwa mfano dhahabu ya Mpanda, nilikuwa natamani sana, hapa kwenye taarifa yake amepongeza na kusema kuna suala zima la kuongeza thamani na kuthibiti utoroshaji wa rasilimali za madini. Naomba sana, refinery sikatai, ni jambo jema na ndipo hapo katika refinery amesema, “mtapunguza kutoka asilimia sita kwenda asilimia nne za mrabaha.” Ni jambo jema, lakini nilichokuwa naomba, eneo hili pia ikumbukwe kuna mchanga unasafirishwa kwenda nje, hiyo mnayoiita makinikia, lakini kule ndani Mheshimiwa Waziri tujiulize kama sehemu ya mchanga huo yapo madini ya dhahabu, yapo madini ya fedha, yapo madini ya shaba, Tanzania tunafeli wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa naomba sana, bado iko nafasi ya kuwa na viwanda vya uchanjuaji hapa hapa nchini, kama ambavyo tumesema refinery ile inayotengenezwa Mwanza; na hapa mimi nashukuru maana tunaambiwa hata dhahabu sasa hivi itaanza kununuliwa na Serikali, ni jambo jema, lakini nasema bado tuna nafasi ya kufanya uchenjuaji hapa hapa nchini. Kwa sababu kama unabebwa kama mchanga kwenye nje lakini ukumbuke huko ndani mmesema kuna shaba, kuna fedha, ni madini haya, ni chanzo cha mapato, hiki kitu ni vizuri kama kingeongezewa thamani hapa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi tena kuuliza, lengo ni nini? Dhahabu hii nyingi iliyopo hapa nchini, naomba sana, leo katika maeneo ya uchimbaji yawezekana hawa watu wachimbaji kwa ujumla wake, tukiwapa motisha tukawapunguzia ongezeko hilo la tozo na kodi mbalimbali, kubwa ambao Mheshimiwa Waziri atakutananalo, wachimbaji hawa kwa ujumla wao, wakihangaika ikapatikana dhahabu, kodi mbalimbali atazipata kutokana na hawa watu kufanya manunuzi katika maeneo mbalimbali. Naomba aliangalie hilo, na bahati nzuri wachimbaji inapokuja kwenye matumizi ni watumiaji wazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huko ndiko ambako kama ni kwa maana ya kodi tuzipate huko. Ukumbuke dhahabu kama ilivyo, ikibaki ardhini huwezi ukaiona thamani yake. Utakuja kuiona thamani kama imetolewa ardhini ikawekwa hapa juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize, zipo nchi hawana hata shimo moja la madini, iwe ni dhahabu au vinginevyo, lakini wametengeneza refinery. Unajiuliza wanakusudia wapate dhahabu kutoka wapi? Kwa hiyo, maana yake sisi hapa nchini tulichotakiwa kwanza ni kufungua milango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikikupa mfano wa kule kwetu Mpanda, DRC Congo siyo mbali. Tukitengeneza mazingira rafiki hapa, ipo nafasi Mheshimiwa ya hata majirani zetu kuleta mali hapa nyumbani kwetu. Kwa hiyo ni wewe kufungua milango Mheshimiwa. Taabu iko wapi? Nimesema kuna nchi nyingine hawana hata shimo moja la kuchimba dhahabu, lakini wametengeneza viwanda vya kusafisha dhahabu. Unajiuliza, wanapata wapi dhahabu? Sasa kudhibiti utoroshaji, ushauri wangu, eneo hili la tozo mbalimbali wewe Mheshimiwa jipange vizuri. Watu hawa wakipewa motisha kila mmoja huko aliko, hata sisi tunaofanya uchimbaji wa kienyeji huwa tunatoa motisha kwa watu wetu nikiamini wakipata motisha hawa, wataongeza kasi ya kutafuta mali na mali ikipatikana upande wa pili wa Shilingi Serikali nayo inanufaika kwa sura hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba katika eneo hilo, ukumbuke wachimbaji hawa bado kuna tozo nyingine nyingi. Mfano mtu ana karasha ambalo ni kitendea kazi, anaambiwa alipie, maji alipie. Sasa tozo hizo mbalimbali ukizijumlisha, leo tunataka kwenda karibia zaidi ya asilimia kumi tozo mbalimbali zaidi ya kumi ambapo utashindwa kuiona thamani na mchango wa wachimbaji hawa ambapo naamini kwa kupitia madini ya dhahabu tuna uwezo mkubwa wa kuitoa nchi hapa ilipo ikapiga hatua mbele zaidi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja.