Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana katika eneo hili la kilimo pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Anthony Mavunde. Kwa kweli wanafanya kazi kubwa na nzuri sana ambayo imeanza kuonekana. Tunataka kuona sasa kazi hii itoke kwenye zile suti ambazo wameziandaa ielekee kwenye vitendo na uhalisia zaidi ili mwisho wa siku tusifanye tathmini kwa mavazi, bali kwa tija ambayo itaonekana kupitia kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitaulekeza katika zao la kimkakati la kahawa. Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa takribani 15 ya nchi yetu ambayo inalima kahawa na hususan katika milima ya Usambara kwa maana ya Wilaya za Muheza, Korogwe pamoja na Lushoto. Zao hili kwa muda mrefu Serikali imekuwa haitoi motisha kwa wakulima kiasi kwamba zao hili sasa linakwenda kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utakumbuka, hata jana Mheshimiwa Anne Kilango Malecela alikuwa anaongelea zao la tangawizi, na hali ya hewa ya Same na Lushoto zinafanana kwa asilimia kubwa, lakini watu wamehama kutoka kilimo cha kahawa kwenda kilimo cha tangawizi kwa sababu ya changamoto mbalimbali zikiwemo huduma hafifu za ugani, uchakavu au umri mkubwa wa mibuna, upatikanaji wa pembejeo; madawa na mbolea na matumizi ya mbegu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye mbegu bora ndiko ambako nataka niweke msisitizo. Ni kwamba Bodi ya Kahawa (TCB) ifanye kazi ya ziada kuhakikisha kwamba kunakuwa na miche mingi ya kahawa hasa katika mikoa hii ambayo nimeitaja hapo awali. Mkoa wa Kagera ndiyo unaoongoza kwa uzalishaji wa kahawa hapa nchini ambapo wanazalisha takribani kwa mwaka tani za kutosha tu, ambazo kwa ujumla wa tani zote nchi nzima, wao wanachangia asilimia 45.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkoa unaofuata ni Mkoa wa Mbeya, Kigoma na Songwe nako kahawa inazalishwa. Yapo maeneo ambayo wanazalisha kwenye baadhi ya wilaya ikiwemo Ruvuma ambako ni Mbinga pamoja na Nyasa, pia Mkoa wa Arusha, Mara, Njombe, Iringa, Manyara, Katavi, Morogoro na Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo langu hapa ni kuishauri Serikali kwamba sasa tuweke ruzuku katika zao hili la kahawa. Tunaona kabisa kwamba zao la kahawa kwa ripoti za mwaka 2021 tumeuza nje takribani dola milioni 142. Ni kiasi kikubwa sana ukilinganisha na pesa ambayo tumeuza kwenye tumbaku ambapo tumbaku ina ruzuku, lakini kahawa haina ruzuku. Kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba tukiongeza uzalishaji katika kahawa, hata hili pato litaongezeka kwa kiasi kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetazama hapa kwenye takwimu, nchi ya Ethiopia ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa kahawa, inazalisha takribani tani 457,000. Yenyewe tangu mwaka 1959 mpaka tunavyozungumza sasa, haijawahi kupunguza uzalishaji. Kadri mwaka unavyoongezeka ndivyo na uzalishaji unavyoongezeka, maana yake wao walilichukuwa hili kama ni zao mahususi, zao la kimkakati ambalo linaibeba nchi ya Ethiopia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali kwa ujumla nawaomba sana kwamba pamoja na mazao mengine yote ya kimkakati tunayoyajadili, tuweke nguvu ya ziada katika zao hili la kahawa ambalo sasa linaelekea kupotea. Matarajio yetu ni kuzalisha wastani wa tani laki moja kwa mwaka, lakini mpaka sasa hivi tumefika tani 68,000 tu. Hizi ni chache sana kwa ukubwa wa nchi yetu ukilinganisha na nchi jirani ambazo kahawa inalimwa lakini siyo kwa ardhi kubwa kama ambayo tunayo hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la kahawa, tofauti na mazao mengine ya kimkakati, ukishapanda una uwezo wa kukaa miaka 30 mpaka 40 kutegemea na aina ya kahawa. Kwa mfano, Arabika, kubadilisha mti uliochoka unahitaji miaka 50 mpaka miaka 60. Hata hii ambayo sasa hivi tunaendelea kuvuna huko, ni kahawa ambayo imeanza kulimwa na wakoloni na baadaye ikalimwa na babu zetu. Sasa sisi kama kizaki kipya tunatakiwa tupeleke mbegu, tuanzishe vitalu vya miche ya kahawa katika maeneo yote niliyoyataja ili sasa tuongeze uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya Robusta, mche unaweza kukaa hadi miaka 40, ndiyo unakwenda kuzeeka kiasi cha kupunguza uzalishaji. Kwa hiyo, naomba sana katika eneo hili tufanye maboresho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la uzalishaji, nikitoa tu mfano wa eneo la uzalishaji wa kimkakati ambalo tumejifunza katika Wilaya ya Mbinga kule Ruvuma; kupitia ushirika wa MBICUFARM tumejifunza jambo kubwa sana. Kahawa yote tunaiona inakobolewa katika mashine ambazo ziko chini ya Vyama Vya Ushirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, tukitaka kwenda kujifunza ushirika wa ukweli, ni vizuri tukaenda kujifunza kwenye Chama cha Matengo kule ambacho sasa hivi kinaitwa MBICUFARM. Wanafanya kazi nzuri sana na tumeiona kahawa yote ikiwa kwenye maghala imehifadhiwa. Hapa ndipo tunapopata somo kwamba haya maghala na yenyewe tukiyawekea takwimu yanaweza yakasaidia hata kuvutia wateja kutoka nje kwa sababu watakuwa na uhakika kwamba akifika mahali fulani kwenye ghala namba fulani anaweza akapata tani za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana na nitoe rai kwamba tuige mifano mizuri ya wenzetu kama hawa ambao tumezikuta tani takribani 15,000 ziko kwenye maghala na tayari mnunuzi amepatikana kutoka nje ya nchi. Halmashauri haikamatani na wafanyabiashara kwenye mageti, hela yote inapatikana kupitia mfumo sahihi wa stakabadhi. Halmashauri inachukua mrabaha wake, Vyama Vya Ushirika vinachukuwa mrabaha, AMCOS zinachukua kilicho chao; na tumeona AMCOS zikitoa CSR hata kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika AMCOS moja inaitwa Kimuli, imeweza kutoa makalavati kwa TARURA ili waweze kuboresha miundombinu ya barabara. Sasa hii ni dhana pekee unayoweza kuipata kupitia ushirika nje ya ushirika itakuwa ni kukimbizana na wachuuzi wadogo hawa ambao baadaye pia wanasaidia kutorosha mazao hata kwenda nje ya nchi na mwisho wa siku inaonekana turnover ya nchi ni ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho lakini siyo kwa umuhimu, ni hili ambalo limezungumzwa kuhusu leseni za maghala. Tumejifunza jambo kwenye maghala haya ya mafuta kwamba baada ya kupata mfumuko huu wa mtikisiko wa soko la mafuta duniani, kila wakati Wizara ya Nishati ilikuwa inatoa takwimu za mafuta yaliyoko katika maghala ya mafuta. Ningetamani kuona jambo hili nalo likitokea katika kila aina ya bidhaa ambayo tunayo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litawezekana tu kama tutakuwa na takwimu sahihi na ghala lilipo na linahifadhi kitu gani? Maana yake hapa tunachotafuta ni takwimu siyo jambo lingine. Mambo ya ubora na mambo mengine yatasimamiwa na idara zinazohusika, lakini angalau kujua kwamba nchi yetu ina sukari kiasi gani? Nchi yetu ina ngano kiasi gani? Nchi yetu ina mafuta ya kupikia kiasi gani? Hili linahitaji takwimu na sehemu sahihi ambayo tunaweza tukafanya hili, ni kupitia wakala wa maghala nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)