Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika nchi yetu kwa kweli kilimo kinafanyika sana, na ndiyo maana kwenye takwimu za Serikali tunaelezwa kwamba kilimo ndiyo ambayo imeajiri asilimia kubwa ya Watanzania. Cha kushangaza, miaka yote pamoja na jitihada kubwa za Serikali yetu, lakini mkulima anakutana na Serikali baada ya kuvuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilimo ni mfumo wa mambo yafuatayo: Kilimo ni utafiti na utaalam (expertise), kilimo ni sayansi teknolojia na mitambo, kilimo ni udongo ama ardhi, kilimo ni mbegu, kilimo ni maji kwa maana ya mvua ama umwagiliaji, kilimo ni urutubisho, kilimo ni madawa, kilimo ni miundombinu ya uvunaji, kilimo ni miundombinu ya uhifadhi na mwisho kabisa, kilimo ni soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mtitiriko ukikosea jambo moja tu, tayari umeshaondoa tija kwenye kilimo. Nasi kama Wabunge kila siku tunapiga makelele, tunataka kilimo cha nchi hii kiwe na tija. Kwa hiyo, kwa mara ya kwanza nimeshuhudia tangu niwe Mbunge, hii ni bajeti ya kwanza haijawahi kuambiwa kwamba ni ndogo kwa kilimo. Kwa hiyo, nimpe pongezi Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ama hakika ameonyesha kwamba yeye ni mwanakilimo kwa vitendo; kwanza kwa kututeulia watu ambao wametupa matumaini, wanakuja kukivusha kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe alikuwa Naibu Waziri, meno yalikuwa madogo, sasa ana meno kama ya mamba ya kuja kuendeleza kilimo. Vile vile msaidizi wake Anthony Mavunde, ama hakika hii ni hazina yetu sisi Dodoma. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haleluya!

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Ni mtu ambaye kila unamweka lazima aoneshe vitendo. Kwa hiyo, mimi nawapa shime muende mkayafanye, lakini Mheshimiwa Waziri angalia sana watu wa chini. Ninyi viongozi mna commitment, lakini huku chini hasa kwa Maafisa Ugani, nendeni mkaweke mechanism ya kuangalia utendaji wao, watakuja kuwaangusha. Kwa hiyo, lazima mwangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa mkulima kwa muda mrefu, na-declare interest. Naweza kuwa na shamba zaidi ya heka 1,000. Kwenye eneo husika sijawahi kuona hata siku moja Afisa Ugani akija hata kuomba mbegu tu niweze kuwapa wananchi wanaonizunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa watu tulioenda kuwapa vifaa, tumeona Rais wetu ameenda kweli sasa kuongeza utaalam, kawapa pikipiki, kawapa vifaa vya kupimia udongo, nendeni mkawasimamie ili wa-translate yale maono yenu. Unless otherwise they are going to fail you. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza bajeti imepanda 45.7 billion, hiyo ni hatua kubwa sana. Tumeonga mme-involve vijana. Niliwahi kushauri vijana lazima watengenezewe mazingira ya kushiriki kwenye kilimo. Naona sasa kwa mipango mliyokuwanayo, ama hakika kundi kubwa la vijana ambalo nimekuwa mtetezi wao siku zote, sasa wanaenda kushiriki kwenye kilimo kwa uadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti ya umwagiliaji, siku zote bajeti inaenda kwenye kujenga mabwawa, lakini mmeenda mbali, mmeenda kutoa mpaka vitendea kazi. Naomba tu mjifunze, kule Egypt wanatumia River Nile kulisha karibu robo ya dunia, lakini River Nile source yake ni Lake Victoria. Sisi tuna mto, mpaka ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage jana kaongelea Ngono Project. Hebu tuangalie hii mito tuliyokuwanayo; Kagera na Morogoro tunaitumiaje? Tusiende kuchimba mabwawa ya irrigation scheme wakati tuna mito ambayo miezi 12 ina-flow bila kukatika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikienda kwenye mawazo yangu manne: Naomba tuanze sokoni. Leo hii uhaba wa mafuta umekuja kugundulika kupitia viwanda na biashara, lakini source ya upungufu wa mafuta ni kwenye kilimo. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara m-synchronize, mkae chini, mpange kwa pamoja. Leo hii India, nchi ambayo inaongoza kwenye kilimo, mkulima haendi kulima mpaka viwanda na biashara viseme msimu tunaoenda, ni zao gani litakuwa na soko zuri? Wanashauri watu wa kilimo, nao wanaenda kuwaambia wananchi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano, nilienda kutafuta soko la green beans. Tukakuta kuna watu kutoka Malawi nao wameleta green beans. Yale ya Malawi yalikuwa na size moja, yana rangi imependeza, kwa kweli tulipigwa, ila basi tu kwa vile tunaipenda nchi yetu, tukayala. Hawa sijui wanaweka madawa, wanaweka nini, lakini kitu cha kwanza ni appearance. Kwa hiyo, naomba sana, watu wetu wa viwanda na biashara, shirikianeni na Wizara ya Kilimo ili tuanzie sokoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna kitu kinaitwa agricultural zones. Nimekuwa nikipigia kelele kila nikichangia. Hata kipindi cha Hayati Mwalimu Nyerere ilikuwa hivyo, ndiyo maana kusini walikuwa wanalima korosho; ukija Tanga kuna Mkonge. Zao humea sehemu yoyoye, lakini linamea kwa ubora? Kuna mwaka watu walileta mikorosho huku Dodoma, imeishia wapi hiyo mikorosho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mmeweka clusters that is the way to go. We don’t have enough resources. Hatuna resources za kutosha, sasa utatawanya hizo resources zote? Bora ukiziweka sehemu moja zitaenda kufanya kazi kwa weledi na vizuri ili tuone matokeo na tija katika kilimo chetu tunachokifanya, lakini tusiache sayansi na teknolojia Mheshimiwa Waziri. Lazima tuende sawa na dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna kitu kinaitwa genetic modified seeds, tunazikataa kwa nini? Leo hii tunalima pamba, tunataka tuzalishe nguo, lakini katika nchi kumi zinazozalisha pamba hatumo. Nchi zote kama Brazil, India, China wanatumia GM Cotton Seeds. Sisi tunachotaka, tuleteeni hizo teknolojia halafu mkulima mwenyewe aamue. Leo mnasema oh, sijui zina madhara, ni uongo mtupu. Hayo ma-apple tunayoingiza kutoka nje mbona mbegu ndiyo hizo hizo zinatumika!

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe tu taarifa mzungumzaji kwamba suala la GMO ni tofauti anavyotaka kulichukulia. Kile ni kifo unachokula mwenyewe ukiona. Siyo sumu, ni kifo unachokula unakiona. Kwa hiyo, suala la GMO lina utata mkubwa na ni jambo siyo katika nchi yetu kuanza kulijadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam Ditopile, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa. Hata simu zilipoanza walituambi oh, mionzi, hamtazaa. Simu tunatumia mpaka leo na zinarahisisha kazi zetu. Tusiogope sayansi. Leo hii kuna watu wanapata mimba bila hata kuingiliwa, wanapandikiza. Hiyo ndiyo sayansi, usibishane na sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri, kusema ukweli mmefanya jitihada kubwa kupunguza riba za kwenye mikopo, lakini niseme ukweli, mkulima hakopesheki. Leo hii mimi ni mkulima lakini vilevile nina kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti. Nilienda kuomba mkopo Benki ya NMB, walikuja pale kwenye ghala langu wakakuta nina dumu za mafuta za lita 20 zaidi ya 2,000, nina stock ya kutosha, lakini walishindwa kunipa mkopo wakiniambia kwamba nyumba yangu moja hapa Dodoma Mjini ndiyo niiweke dhamana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mariam, malizia point yako, kengele imeshagonga.

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi mengine nitaenda kuyachangia kwa maandishi. Niwape moyo, niwatie nguvu, kwa kweli tunaenda kwenye the right direction. Mimi kama mkulima na Mbunge wa muda mrefu ambaye nimekuwa nalia na kilimo, sasa tunasema dalili ya mvua ni mawingu, mawingu tumeyaona na sasa tunaona zile rasharasha. Naamini mvua kubwa inakuja.