Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru nanimshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema ambaye ametujalia kuwepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana anayoifanya hasa katika kuongeza fedha na kuongeza bajeti hii ili kufanya kazi. Amejitahidi vya kutosha kuhakikisha maafisa ugani ambao kwa muda mrefu walikuwa hawaonekani na hawana vitendea kazi wameletewa vifaa vya kufanyia kazi pikipiki; sasa kilichobaki ni kuhakikisha tunawasimamia hawa maafisa ugani ili wafanyekazi ili kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa kuendelea katika sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe, ni kijana msikivu, mwenye kupenda hasa na ana imani kuwa anataka kuleta kilimo chenye maendeleo vilevile nimpongeze Mavunde, nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bwana Tumbo ambaye huyu ni mtaalamu wa masuala ya vifaa vya kilimo alikuwa CAMARTEC, amekuja pale, naye ni mchango mkubwa katika maendeleo ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumza kwa muda mchache sana kutokana na muda nilio nao, na nitakwenda kwenye dhima. Dhima ya kilimo ya kwanza ni kuandaa kilimo bora chenye mazingira bora, lakini vilevile kuwaandaa wakulima wapate tija katika kilimo hicho pamoja na kutengeneza mifumo ya kimasoko ambayo itawasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile muda nilio nao nitazungumzia Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Ni mikoa ambayo sasa hivi kama Serikali haisimamii itaonekana na mikoa ya kimasikini wakati ni mikoa tajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kunatakiwa kuwepo na mifumo ili mifumo hii iweze kuitoa hii mikoa. Itakuwa ni aibu ukienda mikoa mingine inaonekana iko busy inafanya kazi, kuna viwanda kuna maendeleo; lakini Mkoa wa Lindi na Mtwara hatuna viwanda, bandari hazifanyi kazi, njia kuu zote za uchumi zikiwemo barabara ni mbovu sasa unategemea watu hawa watafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninazungumzia kutokea Songea mpaka Bandari ya Mtwara ina- kilometa 657 lakini kutoka Songea kwenda Dar es Salaam ni kilomita 948 lakini kutokana na urasimu wa bandari ya Mtwara ambayo Serikali hajijataka kuwekeza mizigo yote na nafaka na mazao yanakwenda katika bandari ya Dar es Salaam. Jiulizeni, Bandari ya Dar es Salaam kuna nini ilhali ukiangalia Bandari ya Dar es Salaam sasa hivi iko busy kiasi ambacho watu wanakaa na mizigo zaidi ya wiki nzima na urasimu huu unafanya kuingia katika corruption katika bandari ya Dar es salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri ashirikiane na Waziri wa Fedha na Waziri wa Ujenzi waje watupe taarifa kuna nini mpaka bandari ya Mtwara mapaka sasa hivi haifanyi kazi. Urasimu uliokuwepo katika bandari ya Mtwara mizigo yote inayotoka Lindi na Mtwara na Ruvuma inabidi iende Dar es Salaam, hivi jamani kweli tunapiga hesabu za kibiashara hapa? Inamaana hakuna biashara inayofanyika hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ufuta unalimwa Kilwa barabara ya Liwale hakuna lakini ufuta ule ule unabidi uzunguke mpaka Lindi, Lindi mpaka Dar es Salaam ilhali Bandari ya Mtwara iko karibu. Hiki ni kitu ambacho mimi sielewi; ni kama ni zig zag ambalo naliona kabisa. Mimi nitataka nitachangia tena katika Wizara ya Fedha, watuambie Bandari ya Mtwara na Tanga zimekwama wapi? Mazao yote yanakwenda Dar es Salaam, tumeifanya Bandari ya Mtwara ikose kazi kwa ajili ya kupeleka mizigo yote Dar es Salaam. Wao wanatoa sababu za wafanyabiashara, lakini mimi hiyo wala haingii akilini. Kama kweli kuna mikopo inaweza kusaidia Bandari ya Mtwara wakaleta makasha mimi naomba Serikali isimame na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia biashara za korosho, Kawaha na biashara mbalimbali ambayo iko katika mikoa hiyo, kwa kweli inasikitisha, inasikitisha kwasababu hawajatengenezewa mazingira rafiki, viwanda vyote vimefungwa. Hapa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitengeneza biashara kikanda na mazao kikanda. Mkoa wa Lindi ulikuwa ni mkoa wa kulima karanga, soya, ufuta, na kahawa; ndiyo ilikuwa mikoa hiyo. Lakini mikoa mingine ilikuwa imetengenezewa kama pamba, Mikoa ya Kanda ya Ziwa wanalima pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mikoa ya Lindi sasa imetiwa umaskini kwa ajili ya mifumo mibovu ambayo haijataka kuwa rafiki wanawananchi wa Mikoa ya Lindi ikiwemo bandari na barabara, lakini vile vile mazao hayana soko, viwanda mmefunga unategemea watanda wapi? Leo unachukua korosho unaipeleka nje as raw material, korosho ile ile ukibangua mwenyewe unakuja kuuza Dodoma shilingi 25,000. Je, tutaondoaje umasikini kwa watu wa Mkoa wa Lindi na Mtwara tukiwa na mifumo mibovu ambayo haiku rafiki na haiongei?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia tena wakati wa Wizara ya Ujenzi watueleze kwanini Bandari za Mtwara na Tanga hazifanyi kazi? Tujue, kwanini Barabara ya kutoka Kilwa mpaka Liwale haifanyi kazi? Kila mpaka Nachingwea watu wanaangaika na mazao. Unategemea watu wale watategemea nini? wataendelea kuwa maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naunga mkono lakini sifurahi, nataka nione kabisa mfumo wa kilimo katika mikoa hii ya Lindi inapewa kipaumbele ili wananchi wale wasionekana kama ni wananchi maskini. Hii ni mikoa Tajiri, hivyo inahitaji msukumo na mfumo ahsante.