Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara ya Kilimo. Jambo la kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, moja kati ya Mawaziri ambao ni vijana, tunajivunia lakini na Bunge linajivunia, Mheshimiwa Bashe pamoja na Mheshimiwa Anthony Mavunde kwa sababu wanatupa ushirikiano wa kutosha nyakati zote, hata usiku ukimtafuta anakusaidia. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri anatuongoza vizuri vijana na tuko tayari kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya yanayoendelea kwenye bajeti zote alizozisoma Mheshimiwa Waziri, wakati ule tunagawa vifaa na hii iliyosomwa, inaonesha wazi kwamba kilimo kinaenda kubadilika kwenye Taifa letu. Waziri ana mwono wa mbali kwa kiwango ambacho mimi kama kijana najivunia sana uwepo wa Mheshimiwa kaka Bashe kwenye Wizara ya Kilimo na tunampongeza sana. Kwa niaba ya wananchi wa Makete nimpongeze sana. Uono wake wa mbali ni pamoja na kwenye bajeti yenyewe ambayo alimwomba Mheshimiwa Rais. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kufanya change kwenye kilimo kwa kuongeza bajeti hadi bilioni 700.5. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliomba zaidi ya trilioni mbili kwenye Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Rais kwa sasa ametuanzia na bilioni 7. Ukienda kwenye bajeti ya Kenya wanacheza na bilioni 900 hadi trilioni moja, kwa hiyo anawafukuzia, yuko nyuma yao kidogo anawasogelea, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. Akienda kwenye bajeti za Zambia na Uganda naona bado sisi tunazidi kukimbiza kwa hiki ambacho anaenda kukifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu uko kwenye mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza ni suala la mbolea, naungana na Mheshimiwa Waziri kwa asilimia 100. Siku ile alimwambia Mheshimiwa Rais ampe bilioni 150 kwa ajili ya ruzuku kwenye mbolea. Mimi kama Mbunge wa Makete namuunga mkono na kwa niaba ya Wabunge wa Kusini tunamuunga mkono kuhusu ruzuku kwenye mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea sisi kwetu ni siasa, mbolea kwetu ndio uhai wa wakulima wetu, mbolea kusini ndio kila kitu kwa wananchi wetu. Nimwambie wazi Mheshimiwa Waziri, yeye ndiye amebeba Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa sababu Chama cha Mapinduzi ni chama cha wakulima na wafanyakazi. Mbolea ni kilio na naiona direction ya Waziri anayoenda kuichukua ya kuomba fedha bilioni 150 kwa ajili ya kwenye ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amesema jana kwamba ni bora Wizara ya Kilimo isifanye kitu chochote lakini iongeze ruzuku kwa wakulima. Niwaahidi wananchi wa Makete Mheshimiwa Bashe hili tutamwombea kwa Mheshimiwa Rais na namwomba Mheshimiwa Rais bilioni 150 na zaidi hapo aweze kumpatia Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alifika hadi Makete Kijijini kule Kinyika alijionea hali ya wananchi wangu. Changamoto ya parachichi tuliyonayo ni kubwa sana. Parachichi, limeanza na mguu mzuri, parachichi kwa sababu halina lumbesa wanapima kwenye mizani, tunaishukuru Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza ya parachichi ni kwamba kumekuwa na wakulima holelaholela ambao hawafikiwi na Maafisa Ugani, uzalishaji wa miche holela holela ambao miche mingine ina ubora huu, mingine ina ubora huu. Changamoto tunayoipata tutafika wakati miti imekua hatuna wa uwezo tena wa kurekebisha kwenye miti ya mbolea. Tunaomba wizara iwahi mapema sekta ya parachichi ndani ya Mkoa wa Njombe, Mbeya na maeneo mengine iwekewe mpango mkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukienda Wakenya wanaingia hadi mashambani kununua parachichi zilizoko kwenye shamba. Sasa ni vyema tukaandaa mazingira, wakulima wetu wawe na muundo mzuri wa jinsi gani biashara ya parachichi itaenda.

Mheshimwa Mwenyekiti, nimemwandikia barua Mheshimiwa Waziri na nimempelekea mezani kwake. Naomba miche milioni 15 kwa ajili ya wananchi wa Makete kwa sababu nina kampeni Makete ya nyumba moja miche 50. Leo naomba tena Waziri atuwekee kitalu cha parachichi Makete, ile miche inayozalishwa pale iendane na hali ya hewa ya Makete na izalishwe katika ubora kupitia Maafisa Ugani. Ninamsihi na namwomba Waziri, miche milioni 15 iko mezani kwake, namwomba wananchi wa Makete wanasubiri kampeni ya nyumba moja miche 50 kwa sababu tunaamini ndiko utajiri uliko na mkakati wa wazi kabisa wa kuwakomboa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata cold room, Mheshimiwa Waziri amesema anajenga cold room nyanda za juu kusini. Tunaomba hata Makete tuna eneo la karibu na airport ya Mbeya kwa sababu Njombe airport hawajatujengea. Ili tuwahishe mzigo Mbeya kwenye airport yetu ambayo itakuwa inapakia parachichi kwenda kule na kwenye treni, Waziri ajenge cold room Mbeya pale au Makete itusaidie ili wananchi wetu wasipate shida ya kuhangaika kutafuta sehemu ya kuweka cold room.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine sawasawa na hilo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kuhusu suala la lumbesa. Waziri amehangaika kadri awezavyo, suala la lumbesa na wananchi walimwambia. Lumbesa itatatuliwa tu kwa kuweka mizani na hili ni suala la viwanda na biashara. Watu wa viwanda na biashara kama wako hapa waweke mizani tuondokane na changamoto ya lumbesa. Tuondokane na changamoto ya lumbesa kwa nini?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja tu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia sentensi yako tu.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia sentensi yangu moja. Mheshimiwa Bashe iko hivi, Wakenya wanavyokuja na wakulima wengine wanakuja kununua viazi, wananunua gunia moja lina lumbesa, lakini wakienda kwao wanapima kwa mizani. Kilo mia ni sawasawa na gunia moja. Hapa imeondoka na gunia lina kilo 140. Kwa hiyo kama liliondoka na gunia 300 akifika Kenya anakuwa na gunia 400 mpaka 500. Wakulima wetu huku wananyonywa tunafaidisha wananchi wengine. Serikali iweke mizani ili tuondokane na lumbesa. Wizara ya Viwanda na Biashara tunaomba watusaidie,waweke mizani, lumbesa linawamaliza wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)