Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Sekta hii ya Kilimo ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu. Naomba nitoe pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri Bashe kwa Naibu Waziri Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Andrew Massawe na watendaji wote wa Wizara kwa kuhakikisha kwamba kilimo kinaweza kubadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona sasa mapinduzi ya kilimo kweli kweli, wananchi wanategemea sana, wanamwamini sana Mheshimiwa Bashe kwa mambo makubwa ambayo ameyafanya. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu kwa hotuba yake ya siku ya tarehe 24, siku ambayo walikuwa wanagawa vifaa vya wagani wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu siku ile Maafisa Ugani wamepewa vifaa, lakini naomba wapatiwe elimu, hiyo elimu iendane na maeneo ambayo tunatokea. Kwa mfano, Mkoa wetu wa Iringa tunalima mahindi, chai, pareto, alizeti, parachichi basi wale Maafisa Ugani wawe angalau wana elimu ya hayo mazao ambayo tunayalima katika maeneo yetu ili rahisi kwa sababu Wizara imeanzisha mashamba darasa inakuwa rahisi hata kutoa elimu kwa wakulima na kilimo kitakuwa na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua bado tuna upungufu kiasi gani wa Maafisa Ugani ili tuweze kujua kwamba watatusaidiaje. Pia nataka kujua tunao vijana wetu ambao wamehitimu masomo ya kilimo katika vyuo vyetu nchini. Hawa vijana wako katika wilaya zetu, halmashauri zetu lakini je, Serikali haiwezi kuwachukua wakasaidia hata katika haya mashamba darasa? Kwa sababu tulivyokuwa zamani tuna upungufu wa Walimu tuliwachukua Walimu katika masomo ya sayansi wakawa wanajitolea. Huu ndio uzalendo, lakini vijana wetu wamekatwa, wamehitimu masomo yao vizuri, wamekaa hawafanyi kitu chochote. Tunaomba pia hili Serikali iliangalie ili tupunguze hata upungufu wa Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze Serikali kwa mambo yafuatayo:-

(a) Kuongeza pesa ya utafiti;

(b) Kuongeza eneo la umwagiliaji;

(c) Upatikanaji wa mbegu bora;

(d) Ununuzi wa nafaka; na

(e) Ushirika na masoko ya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea tunaomba Mheshimiwa Waziri ajitahidi. Mbolea ukienda kila sehemu, kila mkutano, changamoto kubwa ni bei ya mbolea. Kwa hiyo tuna imani kabisa kwamba sasa hivi tumesema kwamba kuna kiwanda, lakini ulikuwa unaomba ruzuku kwa ajili ya mbolea ili bei iweze kupungua kabisa, maana yake wakulima wengi wameshindwa hata kulima sasa hivi, wamevuna eneo dogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lingine, naomba pesa ya utafiti ipelekwe kwa wakati ili hizi tafiti ziweze kufika kwa wakulima, kwa sababu changamoto kubwa ya utafiti kwamba tafiti nyingi zinafanyika, lakini hazifiki kwa wakulima. Kwa hiyo kilimo kinakuwa hakina tija kwa sababu zile tafiti zinafanyika, lakini zinakaa katika vituo vya tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uwekezaji wa eneo la umwagiliaji. Kwa kweli na niwapongeze sana kwa sababu hata katika Mkoa wetu wa Iringa tuna miradi mingi ya umwagiliaji, lakini wametukumbuka katika Mradi wa Mgambirenga katika Wilaya ya Kilolo. Kwa hiyo niombe, kwa sababu umwagiliaji ndio kilimo kinachotakiwa, ndio kilimo cha uhakika. Umwagiliaji kwa mfano, Zimbabwe mabenki hayawezi kukukopesha kama hulimi kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo niombe na sisi sasa tuweke pesa nyingi katika umwagiliaji ili wakulima wengi wamwagilie ili tuwe na uhakika wa mazao yetu tunayoyalima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunashukuru sana katika Mkoa wetu wa Iringa wameweza kutupatia fedha kufufua zao la chai katika Wilaya ya Kilolo. Wilaya ya Kilolo watu walikuwa wamekata tamaa kabisa kwamba sasa hivi hatuwezi kabisa, tunaichukia na Serikali. Mheshimiwa Naibu Waziri alikwenda Kilolo akawaahidi na sasa hivi hii Serikali ni Sikivu, inatoa pesa na zao sasa la chai katika Wilaya ya Kilolo linafufuka, Halmashauri ya Kilolo itapata pato, wananchi watapata pato na Serikali itaongeza pato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kuhusu kilimo cha mbogamboga. Kwa kweli sekta hii ni ndogo lakini inaongoza katika mapato ya export na mapato ya soko la ndani. Hapa naomba nimpongeze Dkt. Jacqueline Mkurugunzi wa TAA pale Arusha. Kwa kweli tulimtembelea pale Arusha, amesaidia sana katika kuhakikisha kwamba mbogamboga na matunda Tanzania sasa hivi inawezekana. Nipongeze pia hata Serikali yetu kwa kutafuta soko la parachichi. Lakini nimpongeze pia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia pongezi yako.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hadija Jabiri pale Iringa na yeye anatusaidia sana katika zao la mbogamboga na matunda ambako wanawake wengi sasa hivi tumejikita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitaandika kwa maandishi kwa sababu naona kwamba point zangu zingine sijazitoa, lakini namshukuru Mungu…

MWENYEKITI: Pole sana Mheshimiwa Ritta Kabati.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.