Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu asilimia 23 ya ardhi ndiyo inayotumika katika kilimo. Nchi yetu ina watu milioni 40 ambao wanajihusisha katika kilimo. Kwa hiyo, ukiangalia Sekta ya kilimo ndiyo sekta kubwa inayoajiri, ndiyo inayotegemewa katika maisha yetu katika ustawi wa Taifa letu. Kwa hiyo, nilitaka kusema jitihada za Mheshimiwa Waziri ni nzuri, lakini ukizipima siyo jitihada za kimapinduzi, bado dira ya kimapinduzi ya kuboresha kilimo chetu na kwenda katika malengo hasa ya kuliendeleza Taifa hili bado, nimeangalia hii bajeti kuna eneo bado hatujakaa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amerejea Awamu ya Kwanza Awamu ya Pili na Awamu ya Tatu. Nilitaka rejea ileile ya kuanzia Awamu ya Kwanza na kuishia Awamu ya Tatu. Awamu ya Kwanza tuliamua kwamba kilimo cha nchi yetu kiwe ni kilimo cha wakulima wadogo wadogo, lakini tuliamua kwamba wananchi watengenezewe viwanda ambavyo vitahudumia kilimo chetu. Kwa bahati mbaya Awamu ya Tatu tukaja tukabinafsisha viwanda vya kuhudumia kilimo, vilevile tukabinafsisha mashamba makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilitaka kusema na ili nimshauri Mheshimiwa Waziri Bashe, kwamba pamoja na jitihada zake kubwa ni lazima tuamue tunafanya kilimo cha wananchi wengi au tunataka kufanya kilimo cha kibepari au tunataka kuunganisha kilimo cha wananchi wengi pamoja na ubepari. Ninasema hivyo kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija katika hoja ya msingi ukitaka tulete makampuni makubwa, kampuni kubwa inahitaji uwe na eneo kubwa, Wilaya nzima ya Bahi unaipa kampuni kubwa iweze kulima na iweze kusafirisha. Lakini kwa wananchi wetu katika umoja wao, unaweza ukawaunganisha ukawatengenezea ushirika mzuri na tukaweza kulima kwa pamoja na tukawa na viwanda vya kutuhudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo naliona katika nchi yetu bado tunapandishia mifumo, tunachukua mfumo wa Kimarekani tunachanganya na mfumo wa China na mfumo wa Vietnam hatuwezi kusogea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu kwa mfano Vietnam, Vietnam sasa ndiyo inayouza mchele ukijumlisha mchele wa Afrika wote katika ku-export hauwezi kuifikia Vietnam nchi ndogo. Wenzetu wamefanya katika maana ya ushirika, vyama vyao vya Ushirika vina nguvu. Kwa hiyo, kazi ya Serikali kwanza itoe fedha katika ku-finance agriculture ambapo tumeanza kwenye umwagiliaji kwa kiasi kikubwa lakini vilevile ushirika wetu tuimarishe, mahusiano ya Serikali na Ushirika usiwe kama Polisi na mtuhumiwa! Kwenye Ushirika bado kuna shida hakuna Uongozi. Kwa hiyo, nilitaka kwanza hiyo contradiction Wizara ya Kilimo na Serikali waweze kuiangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka nichangie kuhusu Kanda ya Kati. Kanda ya Kati tuchukulie kuanzia Mkoa wa Tabora, Wilaya za Nzega kuja Singida na Dodoma, bado Serikali haijawekeza kwenye kilimo! Hali ya chakula bado ni mbaya, tunasumbuliwa na ukame, lakini bado hatujawa na sera madhubuti kwamba ni namna gani tunasaidia kilimo katika Kanda ya Kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Nigeria walianzisha sera ya maeneo yenye ukame na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo sisi bado, pamoja na hisi skimu ambazo mmetuletea nazo nilikuwa nazihesabu ni kidogo mno lakini bado suala la Kanda ya Kati hatuja-address kilimo hiki, bado kuna dilemma kubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme kuhusu suala zima la zabibu. Mimi nimekua katika miaka ya 1980 tulikuwa tunalima sana zabibu, bahati mbaya zabibu ikaja ikafa kwa maana ya kuharibu kile kiwanda na tukakosa soko Zaidi, lakini sasa….

MWENYEKITI: Malizia sentensi ya mwisho.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iamue kuwekeza kwenye zabibu, kiwanda chetu cha DOWICO kirudishwe lakini tuanzishe bodi ya kusimamia zao la zabibu, ahsante sana. (Makofi)