Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii adimu. Kwa sababu nilishaongea naomba nianze moja kwa moja kwenye mada, naunga mkono hoja ya hotuba hii ya miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze moja kwa moja na ujenzi wa viwanja vya ndege na moja kwa moja nielekee katika Mkoa wangu wa Iringa. Kiwanja cha Nduli ni kiwanja ambacho toka nimeingia hapa Bungeni miaka mitano iliyopita, siku zote nimekuwa nikichangia hotuba ya Uchukuzi lakini kiwanja hiki tumeambiwa kwamba kipo katika mpango wa ujenzi wa vile viwanja 11. Haya majibu tulishapata toka hotuba ya Bunge lililopita, sasa ni lini hasa Kiwanja cha Nduli kitajengwa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hakijajengwa hiki kiwanja kina changamoto nyingi sana na najua kwamba ujenzi wa hiki kiwanja utasaidia sana kukuza uchumi wa Mkoa wetu wa Iringa, hata Taifa zima. Kwa sababu tunategemea sana ile hifadhi ya Ruaha ambayo tunajua kwamba watalii wengi sana tungewapata na tungeweza kupata ajira kwa vijana wetu na vilevile tungeweza kabisa kuongeza kipato cha utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja huu una changamoto nyingi sana. katika njia zile za kuruka na kutua (running way) kuna makorongo, yaani sio ma-corrugation, zile njia ni balaa, kwa sababu mwaka 2012, mwaka 2015 kulishawahi kutokea ajali ya ndege ya Auric. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri au na ile Kamati ingepita kuona, wakati wowote tunaweza tukapata matatizo. Ule uwanja sasa hivi hauna uzio, mara nyingi sana mifugo inakatiza katikati ya uwanja na vilevile bei ya ndege ni kubwa sana kwa sababu hakuna kituo cha mafuta. Kwa hiyo, inasababisha nauli inakuwa kubwa sana. Ningeomba kabisa uwanja huu ukakaguliwe mapema na ikiwezekana katika vile viwanja 11 basi kiwe cha kwanza kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia na ujenzi wa barabara za kiuchumi katika Mkoa wetu wa Iringa. Kwa kuwa Serikali hii ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele kabisa kujenga viwanda kwa ajili ya kujenga uchumi na kufufua viwanda vyetu nchini ili kuongeza ajira na pia kuongeza uchumi katika nchi yetu. Katika Mkoa wetu wa Iringa zipo barabara za kiuchumi ambazo siku zote Wabunge wangu wa Mkoa wa Iringa wamekuwa wakizizungumzia kwamba zijengwe kwa kiwango cha lami ili ziweze kupitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kwenye Mkoa wetu wa Iringa, kwanza kabisa kuna Kiwanda kile cha Mgololo cha Karatasi, kuna Viwanda vya Chai ambavyo viko pale Mufindi na kule Kilolo. Vile vile kuna msitu na kuna hifadhi, lakini barabara zake zote za kiuchumi hazina lami, sasa utakuta malori yanapokwenda kuchukua bidhaa na kuna malighafi nyingi tu ambazo zingesaidia kwenye viwanda lakini wanapokwenda kuchukua zile malighafi wakati wa mvua malori yanakwama mno. Kwa hiyo, naomba kabisa Serikali sasa iangalie na izipe uzito. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwenye kile kitabu, kuna baadhi ya barabara zimetengewa japokuwa ni finyu sana, lakini naomba sasa ungefanyika upembuzi yakinifu, ile miradi ya kiuchumi, barabara zile za kiuchumi zianze kujengwa ili kusaidia uchumi kwenye nchi hii. Labda hata nizitaje kidogo, kuna barabara hasa inayokaa katika hifadhi, Ruaha National Park, hii nafikiri ipewe kipaumbele kikubwa sana katika mkoa wetu, kwa sababu ile hifadhi ni ya pili katika Afrika. Halafu katika Wilaya ya Mafinga kuna ile barabara ya Mafinga-Mgololo, kwenda Shangalawe kupitia Sao Hill, Mtula – Matana kuelekea mpaka Nyololo, kuna ile barabara ya Nyololo - Kibao, hizi zipewe kipaumbele katika Wilaya ya Mufundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukienda Kilolo, barabara inayounganisha mkoa na Makao Makuu siku nyingi sana, hata Profesa Msola alikuwa anaisemea sana, haina lami kabisa. Ile inaanzia Ipogolo- Ndiwili- Ihimbo- Luganga- Kilolo, hii nayo ipewe kipaumbele. Pia kuna ile ya Dabaga- Ng‟ang‟ange- Mwatasi- Mufindi, hizi barabara ni za kiuchumi, naomba zipewe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizungumzie kuhusu reli ya kati. Mimi nimeolewa na Wasukuma, ni vizuri nikiwazungumzia. Huu ujenzi wa reli ungesaidia sana kuponya barabara zetu, tumekuwa tukitenga pesa nyingi sana kwa ajili ya barabara lakini kama hakuna reli tumekwenda kuona kwenye nchi za wenzetu, nchi nyingi zenye miundombinu mizuri hata uchumi unakwenda kwa haraka sana. Kwa hiyo, ningeomba kwa kweli reli safari hii ipewe kipaumbele cha hali ya juu kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pengine ningetoa tu hata ushauri wangu, pengine kungekuwepo na TANRAIL ambayo itafanya kazi kama TANROADS. Hii TANRAIL ishughulikie tu masuala ya reli, reli ya kati, reli ya TAZARA na ijenge hizi barabara ya Tanga, Tanga mpaka Kigali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niizungumzie kidogo reli ya TAZARA, kwamba, kulikuwa kuna ile sheria ambayo muda mrefu sana tulijua kwamba hii sheria ingeletwa mapema ikabadilishwa tungeweza pia kuwasaidia hii Reli ya TAZARA. Mara ya mwisho Waziri aliyekuwepo alikuwa amefanya mpango kwamba wale Wajumbe wa Miundombinu wangekwenda Zambia wakakutana ili warekebishe hii sheria. Sasa nataka kujua imefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ambalo nataka kulizungumzia, ni kuhusu hizi nyumba za Serikali zilizouzwa. Ukisoma kitabu cha Kambi ya Upinzani ukurasa wa tisa unaelezea, lakini nataka kwanza kunukuu kwamba unapozungumzia kitu, nimesoma neno la Mungu kwa sababu Mbunge wangu ni Mchungaji, anasema kwamba toa kwanza boriti kwenye jicho lako ndipo utaona kibanzi kwenye jicho la mwenzio. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimeangalia, hizi nyumba zimeuzwa lini, mwaka 2002, wakati huo Waziri Mkuu alikuwa Mheshimiwa Sumaye na sasa hivi yuko kwenye Kamati Kuu ya CHADEMA. Vile vile nikaona kwamba mgombea wa upinzani naye aliuziwa Plot No. 68 na nikaona kwamba mgombea wa Upinzani, Mheshimiwa Lowassa na yeye pia anahusika. Aliuziwa kwenye 590, sasa ningeomba ushauri huu wangerudisha kwanza wao…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kabati muda wako umekwisha!
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.