Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana Wizara ya Kilimo na kama tunavyofahamu kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kazi kubwa sana inayofanywa na Mheshimiwa Bashe na Msaidizi wake Mheshimiwa Mavunde na Wizara yote kwa ujumla na imekuwa yenye tija kubwa kwa wakulima. Nitakuwa na mchango wangu wa maandishi ambao tayari nimeshautuma ukihusu suala la Bodi ya Zabuni inayosimamia masuala ya pembejeo pamoja na magunia, madeni ya wazabuni mbalimbali kwenye Bodi yetu ya Korosho kwa maana ya CBT. Pia nimeleta mchango wangu wa maandishi kuhusu udhaifu wa Menejimenti ya CBT na malalamiko ya watumishi pamoja na viambatisho vyake, nimeleta pia mchango wangu kwa maandishi kuhusu madeni ya Wazabuni mbalimbali hasa madeni ya bond. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo, tunashukuru maazimio yaliyofanywa na Serikali kuhusu suala la pembejeo lakini ninamuomba sana Mheshimiwa Bashe kwamba mara nyingi pembejeo hizi zinaletwa bure huwa hazitoshelezi kwenye soko lote. Hapo nyumba tulikua na utaratibu wa ruzuku, sasa uone namna ya kusaidia kwa sababu pembejeo zinakwenda chache hazifiki mara nyingi kwa wakati lakini wakulima bado wanalazimika kwenda kununua kwenye maduka ya kawaida ya kibiashara. Sasa wanapofika kwenda kununua ili waweze kuongeza pembejeo ile iliyotolewa na Serikali bure wanakuta pembejeo hiyo ikiwa na gharama kubwa sana. Kwa mfano, mfuko wa sulphur unaweza kufika shilingi 50,000 au shilingi 80,000 ili waweze kujitosheleza. Kwa hiyo, ninakuomba tuangalie sasa na ule utaratibu wa ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, jingine ni kuongezee kwamba wakati huu Serikali imeweze kulipia hizi pembejeo zinazoitwa za bure kutokana na fedha ambayo ilikuwa ni ya export levy iliyokuwa inachangiwa na wakulima hapo nyuma, jambo hili halipo kisheria na Mheshimiwa Waziri umelifanya labda kwa sababu mahusiano yako mazuri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, sasa ninaomba wakati wa Finance Bill muilete hiyo, muibadilishe ili fedha hii ya export levy itamkwe kabisa kwamba inakwenda kulipia pembejeo na wakulima wa korosho na wengine wapate pembejeo hizo za bure tunazoziita lakini kwa kutumia fedha hiyo na iwe kabisa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni usambazaji. Mwaka jana tulishuhudia upungufu kidogo kwenye usambazaji hasa zaidi kwenye upande wa magunia, sasa Waziri utakapokuwa unahitimisha pia utueleze Kama umejipanga kiasi gani mwaka huu kuhakikisha hakuna uhaba wa magunia kwenye zao la Korosho kwa sababu ilisumbua sana kwenye misimu iliyopita, kwa hiyo tunaamini wewe pamoja na Wizara yako umejipanga vizuri kwenye hili sambamba na masuala ya Sulphur ili wakulima waweze kupata Sulphur inayojitosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ninakuomba hakikisha sasa unasimamia vizuri ili magunia yaeleweke pamoja na hizi Sulphur mchakato wa usajili wa wakulima, zoezi hili lilianza lakini mpaka sasa hivi halijakamilika na ni muda mrefu sana. Nikukumbushe pia kwa sababu ya muda suala la Bodi. Bodi yetu ni mpya lakini huduma inayotolewa na Bodiā¦.
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Spika, taarifa!
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Cecil Mwambe naomba usubiri; Mheshimiwa Katani.
T A A R I F A
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kuwa Mheshimiwa Waziri tena kwake kule kwenye Tumbaku ameweka mfumo sahihi wa wakulima na hakuna dhuluma ya kwenye pembejeo. Sasa taarifa yangu anapo windup ahakikishe kile alichokifanya kwenye Tumbaku kinakwenda kwenye korosho ili aweze kubaini wakulima sahihi.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Cecil Mwambe, unapokea hiyo taarifa?
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Katani na mimi nimuongezee Mheshimiwa Waziri kwamba hata kwenye masuala ya viwanda, tulikuwa tuna viwanda vya korosho Masasi, Lindi, Mtama, Nachingwea pamoja na Newala lakini sasa tunaona Mheshimiwa Waziri anatumia juhudi kubwa sana kufufua Kiwanda cha Tumbaku kilichopo Morogoro cha TLTC labda kwa sababu pia nacho kama anavyoniambia Ndugu Katani kwamba ni mdau wa tumbaku na anatoka Tabora anataka kuwapendelea zaidi watu wa Tabora na sisi watu wa Mtwara kutuacha nyuma kidogo. Kwa hiyo, nimuombe kabisa, mikakati ile iliyofanyika kwenye Tumbaku na mazao mengine ailete sasa kwenye korosho ili tuweze kwenda nae sambamba, tuweze kumshukuru kwa kazi nzuri anazozifanya, tuendelee na tunaamini kwamba haya yote atayafanya katika mwaka huu wa fedha ili tusiwe na malalamiko Wabunge tunaotokea kwenye maeneo yanayozalisha korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo waangalie na masuala ya bei. Kuwe na timu ya uhakika kwenye Bodi yetu ya Korosho inayoweza kupata bei za uhakika ili hata wanunuzi wanapokuja kununua kuwe kunafanana kidogo na bei zilizopo kwenye soko la dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mwaka 2021 bei zikidondoka, tunaambiwa matatizo yalikuwa ni UVIKO na mengine. Tunaamini kwa sababu UVIKO sasa umekwisha, bei zitakuwa bora. Miaka miwili mitatu iliyopita korosho iliuzwa mpaka Shilingi 4,000/= lakini mwaka 2021, hapo kati kati tumeshuhudia korosho inauzwa kwa Shilingi 1,500/= mpaka Shilingi 2,000/= kwa wastani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine namwomba Mheshimiwa kuhakikisha tunarasimisha ule utaratibu wa upili. Hata kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi lipo hili suala. Upili ni Soko la Umoja kwa maana ya ile Primary Market. Hili ni lile soko ambalo linawasaidia wananchi kuweza kutatua matatizo yao kwa mara moja. Huwa linatumika jina la Kangomba, lakini siyo neno jema kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka sisi ni kwamba mwananchi ambaye ana korosho debe moja ndani ya nyumba yake, baba yake anaumwa, anatakiwa kumpeleka hospitalini, maghala hayajafunguliwa, atazipeleka wapi korosho zake akazibadilishe ziwe fedha aweze kupata huduma? Kwa sababu hawezi kupeleka debe la korosho hospitalini akapata huduma. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine nitachangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)