Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo. Nitakuwa mchache wa shukrani, wa fadhila kama sitatambua na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kuiheshimisha nchi ya Tanzania na kuwaheshimiwa wakulima wa Tanzania kwa kuweka bajeti hii ya kihistoria mwaka huu. Nampongeza pia Waziri pamoja na watendaji wake kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kabisa tatizo kubwa katika kilimo ni uzalishaji mdogo kwa eneo na uzalishaji huu mdogo unasababishwa na upungufu au ukosefu wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu, mbolea pamoja na viuatilifu. Tunafahamu kabisa ikifika wakati wa msimu upatikanaji wa mbegu unakuwa wa shida kabisa na zikipatikana bei yake inakuwa juu na wakati huo ndiyo wakati ambapo wakulima wanakimbizana na unyevunyevu wa mvua. Naomba kuishauri Serikali kwa bajeti kubwa iliyoipata ya uzalishaji wa mbegu, mbegu nyingi tuzizalishe huku Tanzania, tupunguze mbegu tunazoziagiza kutoka nje ili wakulima wetu waweze kumudu bei ya mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile watu wameongea kuhusu bei ya mbolea, tunafahamu changamoto tulizozipata kipindi kilichopita, lakini mwarobaini wa tatizo hili ni kuwa na viwanda vyetu wenyewe huku ndani, hatuwezi ku-control bei ya mbolea tunazoagiza kutoka nje na ruzuku iwekwe katika viwanda vinavyozalisha mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kuchangia kidogo kuhusu kilimo cha umwagiliaji. Tuna fursa kubwa sana katika kilimo cha umwagiliaji. Tuna maeneo yanayofaa kwa umwagiliaji, potential area zaidi ya hekta milioni 29 na pointi, lakini japokuwa sasa hivi tumeweza kuendeleza hekta kwenye 700,227 na lengo la kwenda kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ni hekta 1,200,000. Bado eneo hili ni dogo na Serikali haiwezi kufanya kila kitu, naomba kuishauri kwamba, Wizara ikaweke fursa katika eneo hili ili kuwahamasisha wawekezaji waweze kuweka mchango wao katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo hiki ndiyo kilimo ambacho nategemea kitajenga mazingira mazuri kwa vijana, kiweze kuwafanya vijana wawekeze katika kilimo cha umwagiliaji kwa sababu anaweza kupata mapato mapema zaidi hata kuanzia wiki tatu, mwezi au miezi miwili. Hapo vijana watapata kipato kutokana na kilimo cha umwagiliaji. Nimeona mpango wa Wizara unaoitwa National Strategy for Involvement of Youth in Agriculture, mahali hapa nategemea Wizara itawatafutia vijana mashamba kwa kufidia maeneo na kuweza kuwakodisha vijana ili waweze kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nategemea pia katika bajeti hii kubwa iliyowekwa kwenye kitengo hiki cha umwagiliaji wataenda kuchimba mabwawa na kuvuna maji ya mvua ambayo mara nyingi yanasababisha mafuriko, vile vile kwenda kuboresha miundombinu. Kuna miradi mingi ya mabwawa ambayo yameshachimbwa ambayo bado ufanisi wake haujawa mkubwa kwa sababu ya kutokuweka miundombinu ya kupeleka maji katika mashamba na mifereji mingine tunajua inapoteza maji. Kwa hiyo mifereji hiyo pamoja na miundombinu ingesakafiwa na kutengeneza miundombinu mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kule Manyara, Mradi wa Bwawa la Dongobesh umekamilika lakini hauna miundombinu ya kupeleka maji mashambani. Naomba uwe mmojawapo pamoja na kuchimba mabwawa. Naomba bwawa ambalo limewekwa katika mpango wa Mheshimiwa Waziri, Bwawa la Dawi, lipate kuchimbwa. Vile vile kuna wakulima wanapenda kilimo cha umwagiliaji lakini mashamba yao yako juu ya mifereji wanatumia pump na generator kumwagilia mashamba yao. Niiombe Serikali kabisa kwa nia njema waweze kutoa kodi kwenye vifaa hivi ili wakulima wengi waweze kununua pump hizi na waweze kumwagilia maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri kidogo, kwa sababu tumepata bajeti hii kubwa ya kihistoria, katika ufanisi naomba kushauri tu kwamba, Wizara iajiri watendaji wa kutosha, kwa mfano, Wahandisi wa Umwagiliaji kule kwenye halmashauri hawapo na ndiyo wanaoenda kusimamia miradi hii. Vile vile kuna vitengo kwa mfano Kitengo cha Agro-mechanization ambacho kilikuwepo, wale waliokuwepo baada ya kustaafu Serikali imeacha kuwaleta watu hawa, ndiyo maana wakulima wanabaki kwenye kilimo cha mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wamenunua trekta zilizoharibika, hakuna mtu wa kuwashauri. Kuna power tiller tulihamasisha, wakulima wana ma-power tiller yameharibika hakuna mtu wa kuwasaidia. Kwa hiyo katika ajira ijali tusiangalie tu labda pengine ma-agronomist, kuna vitengo hivi vya agro mechanisation, kuna wakulima bado wanalima kwenye miteremko mikali, lakini kulikuwa na washauri, hawa watu wa land use, tunaomba tu Wizara ikaangalie hivyo vitengo muhimu ili kwenda kuwasaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha, tayari kengele imepiga.

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)