Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza jana tulipewa kitabu, pamoja na cha bajeti, kitabu kingine kidogo chenye taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote hadi Aprili 16. Kwenye ukurasa wa 17, naomba ninukuu, kwenye Wilaya yangu ya Chunya, wanatoa taarifa ya minara iliyoweka inayofanya kazi ya mawasiliano na ambayo haifanyi kazi, kwenye Wilaya ya Chunya:
“Kata ya Kambikatoto mtoa huduma Vodacom, ruzuku dola 51,000, mnara haujawaka. Kata ya Lualaje, mtoa huduma TTCL, ruzuku dola 62,000, mnara haujawaka. Kata ya Mafyeko, Vodacom, ruzuku dola 121,000, mnara haujawaka. Kata ya Makongorosi, Vodacom, mnara haujawaka. Kata ya Matwiga, Vodacom, haujawaka”
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda tu rekodi iwe wazi kwamba minara haipo, kwa hiyo wanavyosema haujawaka ina maana upo lakini haujawaka, hii minara haipo. Kwa hiyo, kama ruzuku wameshapewa wapeleke minara, kama hawajapewa ruzuku basi wapewe ambao watapeleka minara. Minara haipo!
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua na mambo makubwa, mazuri yanayoonekana. Jambo la kwanza, bajeti ya maendeleo, Serikali ya Awamu ya Tano wameitoa kutoka asilimia 20 kwenda asilimia 40 ya maendeleo, jambo zuri sana, imejipambanua. Pia akiongea Mheshimiwa Rais ukimtazama usoni amejipambanua sana na wanyonge, watu wa chini. Ukimwangalia anavyoongea unasema huyu kweli inamuumiza, ukiwaangalia Mawaziri wanavyoongea na wanavyofanya kazi vijijini unaona kwamba kweli hawa wanataka kumkomboa mnyonge, wanataka kumkomboa Mtanzania, lakini kwa kuanzia na mnyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hawa wanyonge ambao wanatuumiza, bajeti tunayoipitisha hapa inakwenda kutatua matatizo yao, ndiyo bajeti hii ambayo Bunge linapitisha. Hakuna kitu kinaumiza au kinakera kama Bunge hapa linapitisha bajeti iende kwenye Wizara hii kiasi kadhaa, Wizara hii kiasi kadhaa, zikija Kamati kupitia bajeti mwaka unaofuata mwezi wa Tatu au wa Nne, unaambiwa Wizara hii imepewa asilimia 10, Wizara hii asilimia 17, Wizara hii asilimia 15. Sasa Serikali yetu nzuri, Serikali ya Chama cha Mapinduzi tunawapa KPI hiyo sasa, hiyo ndiyo tutawapima. Mwaka kesho tukifika mwezi wa Nne tunataka tuone bajeti ambayo tunapitisha hapa ya kuwakomboa wanyonge ikifika mwezi wa Nne imepita asilimia 80, asilimia 90. Tutawapima mwezi wa Nne mwaka kesho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, naomba niongelee barabara ya Mbeya- Chunya- Makongorosi. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, kwanza napenda kuishukuru sana Serikali kwa kujenga angalau kutoka Mbeya kufika Chunya, nawashukuru sana. Barabara hii ina historia ndefu sana, hii ndiyo ilikuwa zamani ambayo Cecil Rhodes alisema ni barabara ya kutoka Cape kwenda Cairo ilipita toka Zambia- Mbeya- Chunya- Itigi- Manyoni- Babati- Arusha kwenda Cairo, ingawaje Serikali yetu baadaye ilipitisha sheria, Government Notice, kwamba itakuwa inatoka Mbeya- Iringa- Dodoma, lakini asilia ilikuwa Mbeya- Chunya- Itigi- Manyoni- Singida- Babati- Arusha, ndiyo Great North Road ilikuwa inapita hapo. Sasa naishukuru sana Serikali kwa kujenga angalau mpaka Chunya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi nauli kutoka Chunya kwenda Mbeya, kutoka Sh. 10,000/=, 15,000/= sasa hivi ni Sh. 3,500/=. Sasa hivi mazao kutoka Chunya kwenda Mbeya yanakwenda kwa urahisi. Ndiyo uzuri wa kuweka miundombinu mizuri kwa ajili ya wananchi, nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mwaka huu sasa barabara hii imepangiwa Shilingi bilioni 45.8 lakini zaidi ya asilimia 80 ya hela hizi zinalipa madeni, kwa hiyo, itakayojenga barabara kutoka Chunya kuelekea Makongorosi ni karibu bilioni tisa. Kama alivyosema Mheshimiwa Massare, jirani yangu, kipande kingine cha kutoka Mkiwa kwenda Itigi, bilioni sita. Yote katika hiyo 45 billion itakwenda kwenye kulipa madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ilianza kujengwa kabla ya barabara ya Iringa- Dodoma haijaanza, kabla ya barabara ya Msata- Bagamoyo haijaanza, hii itakwisha lini! Naomba sana Mheshimiwa Waziri aongezewe fedha kwa ajili ya kumalizia barabara hii kufika Makongorosi ili iendelee kutoka Makongorosi kwenda Rungwa na mwishoni kwenda Mkiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa watu wa Chunya ni lulu, ni mboni ya jicho, sana, tena sana. Sasa imejengwa juzi nimetoka Chunya mwezi wa pili nimekwenda TANROADS Mkoani kuwaambia kuna sehemu mbili zimeanza kubomoka sababu kuna malori yanabeba tumbaku, kuna malori yanabeba mbao ambayo yanaweka rumbesa, kutoka Chunya kuja Mbeya, lakini yakifika Mbeya yanagawa kwa sababu kuna weigh bridges, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iweke mizani ya kupima hiyo mizigo ya malori ili tuweze kuilinda hiyo barabara yetu, hata mkiweka temporary au mobile weigh bridge itasaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwakibete ameongelea Uwanja wa Songwe na mimi nitaongelea Uwanja wa Songwe huo huo. Uwanja wa Songwe ulianza kujengwa miaka kumi na nne iliyopita, Uwanja wa Kigoma umeanza kujengwa miaka minne iliyopita, Uwanja wa Bukoba miaka minne iliyopita, Uwanja wa Tabora miaka minne iliyopita, Uwanja wa Mafia miaka minne iliyopita, huu wa Songwe miaka kumi na nne iliyopita. Mara tatu, mara nne ndege zinatoka Dar es Salaam kwenda Mbeya zinageuza zinashindwa kutua, hasa mwezi wa Tano, wa Sita kwa sababu ya ukungu, kwa sababu uwanja hauna taa. Kwa hiyo, naomba uwanja huu nao uishe tunahitaji sasa hivi kuweka taa za kuzielekeza ndege kutua, kuweka fensi na kumalizia jengo la abiria. Sasa mwaka huu tumetenga bilioni 10 sijui kama zitatosha. Naiomba Serikali Uwanja wa Songwe ni gateway kubwa sana kwa Mikoa ya Kusini na nchi jirani, naomba uishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kiongozi mmoja wa nchi jirani…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.