Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, najua dakika tano ni chache sana nitaongelea mambo mawili. Suala la kwanza ni masoko ya kibiashara ambayo hayo masoko Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukieleza sana watu wa Mkoa wa Kagera. Nimeangalia kwenye taarifa ya Waziri sijaona amesema nini. Hayo masoko ndiyo biashara kubwa, hayo masoko ndiyo kiunganishi tunachokitegemea ili tukafanye biashara. Masoko yako Nkwenda, Mrongo na pia Mtukura. Hayo masoko yamejengwa kwa fedha za mikopo, lakini pia na Serikali, sasa kuyatelekeza haina maana ina maana hakuna value for money. Naiomba Wizara hii na Mheshimiwa Waziri ni mchapakazi, hebu aseme neno moja na watu wa Mkoa wa Kagera ili wapone. Kwa hiyo hilo ni suala la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hayo masoko ninayoyaongelea yana uhusiano sana na biashara tunayofanya. Sisi ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya ndizi, leo tunavyoongelea biashara kubwa ya ndizi zinaelekezwa Uganda. Nakumbuka wakati fulani nilimpigia simu Mheshimiwa Waziri nikitaka atatue mgogoro wa wafanyabiashara wa Murongo na wafanyabiashara wa Uganda kuhusu ununuzi wa ndizi. Tulipata solution kwamba ndizi ziweze kuuzwa eneo la wazi pale Mrongo, chafu limechakaa, lakini sasa tukiwa na hayo masoko tutaweza kufanya biashara nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ndizi ni asset kwa Uganda kwa sababu wanasafirisha nje. Ukienda kwenye Mataifa mbalimbali unakuta ndizi produced from Uganda wakati in reality zinatoka Kagera, ni ndizi za Kagera zinavushwa zinaenda kupandishwa hadhi na kuuzwa nje ya nchi. Kwa hiyo naomba sana hayo masoko yapewe umuhimu ili tuweze kuweka tija katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea kama walivyoongea wengine kuhusu zao la kahawa. Nilikuwa nasoma journal moja wamesema ni journal business insider Africa, wanasema baada ya maji na chai kinachofuata kwa kunyweka zaidi ni kahawa. Kwa hiyo kuna fursa nzuri ya biashara tukiwekeza vizuri kwenye kahawa. Nimeangalia nikafanya study tu kwamba tumeweza kuzalisha tani 65,000 it is a peanut, lakini leo tunakuwa na malengo ya kuzalisha tani 72,000, its still small, kwa Mkoa wa Kagera tu ukiangalia wana uwezo wa kuzalisha zaidi ya hekta milioni moja, lakini eneo linalozalisha ni hekta 600,000, lakini siyo hiyo kahawa tu, wanazalisha less than hekta 48,000. Kwa hiyo unaona kwamba maeneo makubwa hayajaweza kuzalisha vya kutosha bado tuna potential ya kuzalisha zaidi kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnadhani kwa nini watu hawapendi kuzalisha kahawa kwa wingi, kuna wakulima takriban 130,000 kwa Mkoa wa Kagera, ni wachache sana kwa sababu eneo la Mkoa wa Kagera linaweza kuzalisha zaidi kwa jinsi nature yake ilivyo. Watu hawazalishi kwa sababu ya rasimu kwenye biashara ya kununua na kuuza kahawa. Niishukuru ofisi yao kupitia Waziri Mkuu, leo wanatangaza biashara ya kahawa itapata uhuru wa kiasi fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri pia ameongelea minada na bado nabaki hapa kwenye swali langu, bado tumejiridhisha kiwango gani kwamba wale wanaokuja kununua kwenye minada hawataweza kuwa na maswali ya price fixing. Kwa sababu hilo pia lipo, wanaweza kuwa wamepanga wakaja watu 10, wameshaweka idadi au kiwango wanachotaka kununua, kwa hiyo automatic mkulima ataumia. Kama hatutapata fedha nzuri ya kuuza kahawa, wasidhani kwamba tutaongeza uzalishaji wa kahawa. Watu watatelekeza kahawa, wamekuja kwetu, namshukuru Naibu Waziri alikuja akagawa miche zaidi ya milioni mbili kwa Mkoa wa Kagera, Kyerwa…

MWENYEKITI: Kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. SAASHISHA. E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa pamoja na mchango wake mzuri na maelezo yake na faida za kahawa, lakini nataka kumpa taarifa kahawa hiyo haijapewa ruzuku.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anatropia, taarifa hiyo unaipokea?

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nimeipokea na niongezee hapo hapo. Nimem-quote mkulima mmoja anasema unaweza ukapepeta ukaweka kahawa kwenye magunia, lakini bei inavyokuja hairidhishi. Kwa hiyo automatic kama bei ya kahawa haiwezi kuridhisha, mkulima ata-ignore biashara ya kahawa. Kila siku tutakuja tunatoa mifano mizuri ya Uganda, leo ameeleza Mbunge mmoja hapa, Uganda leo ina rank, the second in Africa kwa kuzalisha kahawa wakati kahawa inatoka Mkoa wa Kagera, siyo sawa, which means kuna shida kwenye soko letu. Tuna shida katika kuendesha masoko na ununuzi mzima wa kahawa kwenye eneo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi kuomba sana kwamba mfumo ambao nimeona na mwongozo wameweka wausimamie vizuri, tuone kama utaleta tija. Kuna madalali wanaumiza sana wakulima, lakini hatuwezi ku-avoid, tutengeneze mfumo madhubuti ambao hawa madalali hawatawaumiza wakulima. Pia walipwe kwa wakati, first come first save. Mkulima anaweza kupima mazao yake leo akaja kulipwa baada ya wiki tatu, yule anayelipwa wa kwanza ni yule anayetoa chochote. Wakiweza kusimamia hiyo mifumo, tunaweza kuleta mabadiliko kwenye soko la kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)