Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kwa rehema zake. Nianze mchango wangu moja kwa moja kwa suala zima la ukuaji wa kilimo katika nchi yetu. Suala la ukuaji wa kilimo limekuwa gumu kwa muda mrefu na niseme tu sababu kubwa sana ambayo imechangia shida ya ukuaji wa kilimo ni kuongeza maeneo ya kilimo, lakini hatuangalii vizuri suala la productivity ambalo ni production per unit area.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia pia hapa Serikali au Wizara ina mpango wa kuongeza eneo la umwagiliaji na niombe sasa kwa kuwa bajeti imeshaongezeka ijikite zaidi kwenye suala la productivity kwa sababu kwa bajeti hii sasa tunaweza kuwa na mbolea na tumesikia pia tutakuwa na mbegu bora, huduma za ugani zimeshaimarishwa na kadhalika. Kwa hiyo niombe Serikali sasa ijikite kwenye productivity.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye utoshelevu wa chakula. Tumesikia mara kadhaa kwamba kuna dalili kwamba Bara zima la Afrika litakuwa na shida ya utoshelevu wa chakula, lakini sana kwa upande wa kwetu ngano tunaona kwamba ina upungufu mkubwa na kwa takwimu tumesikia kwamba mahitaji ya ngano katika nchi yetu ni tani milioni moja na wakati huo huo sisi tunazalisha tani 70,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli tunaona kabisa kwamba hapa tunahitaji kuagiza ngano nje lakini mimi sikubaliani sana na hili suala la kuagiza ngano nje. Kwanza tunao hawa waagizaji wa ngano, tunaweza tukawatumia hawa hawa, tukawawezesha tukawapa maeneo, tukawapa extension services wakazalisha ngano, hata kama haitafikia hiyo tani 1,000,000 Watanzania sasa tubadili mitazamo yetu tuna chakula cha aina nyingi sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi niwapongeze wale Watafiti ambao wamefanya utafiti na kuboresha viazi wakatengeneza viazi lishe wamevifanyia Biofortification sasa hivi unaweza ukapata keki nzuri sana kutokana na unga wa hivi viazi, ukapata maandazi na ukapata pia biscuit kutokana na hivi viazi, ninaomba tutumie pia mazao yetu. Tuna mazao ya aina nyingi sana tunayo mihogo, tunayo viazi mviringo, tunayo magimbi, tunao mchele tunapata pia hata mkate kutokana na mchele, vitumbua tunaweza tukatengeneza bagia kutokana na dengu tunalima dengu, tunaweza tukatengeneza bagia kutokana na kunde. Kwa hiyo mazao tunayo mengi sana ambayo tunaweza tukatumia, tuachane na huu mtazamo kwamba bila mkate bila chapati za ngano, bila maandazi huwezi ukanywa chai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mazao kama korosho unaweza ukafanya mchanganyiko mzuri korosho, maboga pamoja na matunda ukapata breakfast yako nzuri sana, sitaki kuwarudisha labda kwamba tunafanya mambo ya kizamani lakini ndivyo vyakula ambavyo tunavyo na ni vyakula ambavyo vina lishe bora. Kwa mfano, maboga yanasaidia pia kwenye suala la kudhibiti diabetes, ni mazuri sana ukitumia ukaepukana na mkate au maandali ni mazao mazuri sana. Tunazo karanga pia kwa hiyo hata ndizi ni nzuri sana unaweza ukatumia kwenye breakfast uka-balance pamoja na karanga pamoja na matunda ukatengeneza mlo wako mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba sana tutoe kipaumbele kwenye umwagiliaji wa mazao haya ili yaweze kupatikana kwa mwaka mzima, tunaweza pia hata tukawasaidia wakulima wetu wakapata kipato badala ya kupeleka fedha nyingi kununua ngano tani 1,000,000 wakulima wetu wadogo wanaweza wakapata kipato na wakatusaidia pia kupata lishe bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hifadhi ya chakula naomba nizungumzie kidogo eneo hili muda ni mdogo, tuna matatizo ambayo yametokea wakati Fulani, watu wamepoteza maisha kutokana na sumukuvu na hii mara nyingine inatokana na hifadhi ambayo siyo nzuri ya nafaka au mazao ya karanga. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kuna wasambazaji wa ile mifuko ambayo hairuhusu hewa kupita au unyevunyevu, tuhitimize sana hii mifuko isambae kwa wakulima wa mahindi ili waweze kuhifadhi nafaka. Naomba dakika moja, mifuko iweze kusambazwa kwa sababu hii inazuia sana sumukuvu na tunaweza tukapata chakula ambacho kipo safe zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna wale wabanguaji wadogo wa korosho wawezeshwe kupata vacuum sealer, Tanzania nzima ukitafuta vacuum sealer hazipo mpaka uagize nje na ukiagiza nje hizi zinatozwa VAT, mimi naomba VAT iondolewe kwenye vacuum sealer ili wabanguaji wadogo wabangue korosho na ziweze kuhifadhiwa vizuri kwa kutumia vacuum sealer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesahau kuunga mkono hoja, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)