Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kwanza kabisa nianze kuipongeza Serikali kupitia Wizara yake ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri nakupongeza pamoja na crew yako yote bila kusahau Katibu Mkuu na Watendaji wote. Kwa dhati kabisa naomba nimpongeze Mkurugenzi wa TAHA Dada yangu Jackline Mkindi, kwa kweli tunakupongeza sana kwa namna ambavyo umeendelea kuwapa matumaini Wizara ya Kilimo, umeonesha mfano kwa akina mama ambao wanafanya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia Bunge hili niseme naomba urafiki wetu usiishie tu kule Arusha sasa hivi tuhamie Jimboni Momba tunatamani kukuona. Mheshimiwa Waziri kabla nielekeze mchango wangu kwenye mambo mawili kwenye Benki ya Kilimo pamoja na umwagiliaji naomba nitoe ushauri. Mheshimiwa Waziri hotuba yako ni njema sana na imeleta matumaini sana kwa wakulima wa nchi hii, kwa namna hata ulivyokuwa unawasilisha mwili wako ulivyokuwa unazungumza inaonesha umebeba matumaini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hili ili bajeti yako iweze kutekelezeka vizuri, angalau kupungue siasa kidogo, ili siasa ipungue ili matumaini haya uliyowaonesha Watanzania wakati unawasilisha naomba tuanzie hapa. Sasa hivi bei elekezi ya Mahindi ambayo mmetangaza kwa kilo ni Shilingi 570 vyovyote vile, Mheshimiwa Waziri tumepata janga la mvua hapakuwa na mvua kabisa na hayo yalikuwa ni mabadiliko ya hali ya hewa, pia tulipata mfumuko wa bei kwenye mbolea, wananchi hawajalima na hata walipolima kwa kutumia uwezo wa Mwenyezi Mungu hawakuweza kwa sababu mazao yamekauka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kukuambia huko vijijini mahindi ni bei ghali. Bei ya debe moja la mahindi linauzwa shilingi 10,000, shilingi 9,000 hadi sehemu nyingine shilingi 12,000, mwananchi huyu atanunua kutoka wapi? Tunaomba kama inawezekana kwa kuwa NFRA lengo lake kubwa ni kwa ajili ya usalama wa chakula, tunaomba bei ya mahindi kwenye maghala yetu kwa mkulima wa kawaida yauzwe kwa kilo shilingi 300, tukiwa na maana kwamba yakiuzwa shilingi 300, kilo 100 yatauzwa shilingi 30,000 sawa sawa na ile bei ambayo huwa wachuuzi wanaanza kwenda kununua kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kula lazima uliwe! Kwa hiyo ambavyo Serikali huwa inaenda kuonekana wakati wa kununua tu sasa hivi tunaomba na yenyewe ikubali kuingiliwa, wananchi hawana kabisa mahindi huko vijijini hakuna, hata wakipika hizo pombe za kienyeji hawana uwezo wa kununua mahindi. Kwa hiyo, tunaomba bei ya mahindi ishuke kwenye maghala iwe Shilingi 300. Utajuaje kwamba itaenda kumnufaisha mwananchi wa kawaida kwa sababu tunajua wafanyabiashara watachukua hiyo nafasi kwa ajili ya kujinufaisha, wale wanajeshi wako uliokuwa umewaleta pale juzi wanawajua vizuri wananchi wa kawaida wale Maafisa Ugani, wanawajua vizuri kabisa kwamba huyu ni Bibi hana uwezo na huyu ni mfanyabiashara, yule Bibi ambaye anataka kununua kuanzia gunia moja, debe mbili hadi gunia 10 tunaomba mahindi yauzwe kwa kilo moja Shilingi 300. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda kutokuwa rafiki kwenye suala la umwagaliaji, nimeshawasilisha maandiko yangu kwa watendaji wako. Yapo mabonde kadhaa kwenye jimbo langu ambapo pia mwaka 2021 nilikwambia; tunalo Bonde la Msangano ambalo likiwezeshwa kwenye umwagiliaji litahudumia vijiji zaidi 10. Pia tunalo Bonde la Kamsamba ambalo likiwezeshwa litahudumia kata zaidi ya nne pamoja vijiji zaidi 15. Vile vile tunalo Bonde la Kapele pamoja na bwawa ambalo linabeba Bonde la Kasinde pamoja na Mto Tesa, litahudumia kata zaidi ya sita pamoja na vijiji zaidi ya 15. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea lango la SADC tunamaanisha Wilaya ya Momba. Wilaya hii ina majimbo mawili; Tunduma na Momba. Sisi Momba ndiyo tunalima, Tunduma hawalimi. Sasa Mheshimiwa Waziri itakuwaje usituwezeshe sisi huku ambao ndio tunaanza kupokea kwenye lango la SADC kwenye umwagiliaji? How comes mtu unaweza usitengeneze sebule ukaenda kutengeneza chumbani, mgeni akija atajuaje? Kwa hiyo, tuanzie hapa ambayo ndiyo mapokeo ya lango la SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchele wote ambao unauona upo pale Tunduma unatoka Kamsamba na mchele wa Kamsamba unauzika sehemu yoyote. Kwa hiyo, tunaomba sana; Zambians wanakula mchele wetu, Kongo wanakula mchele wetu. Tunaomba kuwezesha kwenye mabonde yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo namwomba Mheshimiwa Waziri hili tusaidiane. Ataongea vizuri na watu wa TAMISEMI, tunaelewa dhati kabisa ya moyo wake ya kwamba anataka kuwasimamia wale Maafisa Ugani, lakini how comes mzazi awe na mtoto ambaye amemzaa, na ana uwezo, anaweza kumhudumia, lakini awe anakulia nyumba ya pili? Maafisa Ugani warudi kwenye Wizara yake. Hiyo D by D tunaona kabisa imeshindwa kufanya kazi. Haiwezekani hata kidogo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia hiyo sentensi yako ya mwisho.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia. Kule kwenye Halmashauri zetu Maafisa Ugani wanatumwa kazi nyingine na wakati mwingine hata wakipewa magari wananyang’anywa. Sasa nani ambaye ataweza kusoma kama hali. Kwa hiyo, tunaomba Maafisa Ugani warudi kwenye Wizara yako ili tuone huo usimamazi unaotaka kuwasimamia sisi tuje kukubana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)