Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Mwenye wingi wa Rehema kwa kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako tukufu. Namshukuru sana Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu kwa jinsi inavyowatumikia Watanzania. Nampongeza Mheshimiwa Bashe kwa kazi nzuri anayoifanya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunafahamu kwamba Sekta ya Kilimo imeajiri watu wengi sana. Asilimia 65 ya Watanzania wote wameajiriwa na kilimo, wakiwemo wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa jinsi ambavyo imejipanga kwa ajili ya kukiinua kilimo. Kilimo kikipewa kipaumbele wananchi wataweza kufanya vizuri katika kilimo. Ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wakiwekewa mazingira wezeshi katika kilimo wataweza kufanya vizuri. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri, Serikali iweze kutoa ruzuku kwa ajili ya mbolea. Kwa muda mrefu sana mbolea imekuwa ikileta shida kwa wakulima. Maeneo mengine mbolea inachelewa kufika na tunafahamu kabisa kwamba mvua za kwanza ni zakupandia na maeneo yanatofautiana. Kigoma na Rukwa ni tofauti, na hata Tanga. Kwa hiyo, mvua zinazoanza kunyesha Kigoma pengine Tanga zinakuwa hazijanyesha. Kwa hiyo, tunaomba mbolea ifikishwe kwenye maeneo husika mapema kabla wakulima hawajaanza kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuishukuru Serikali kwamba kwa muda mrefu tumeona imekuwa ikitumia pesa nyingi kuagiza mafuta kutoka nje, lakini kwa sasa Serikali imedhamiria kabisa kuhakikisha mazao yanayotoa mafuta yanapewa kipaumbele. Naishukuru Serikali kwa kuendelea kutusaidia sisi watu wa Kigoma, na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi anavyoendelea kuhamasisha michikichi katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Kigoma walihamasishwa na wakahamasika kulima kilimo cha mchikichiki. Walio wengi tayari wamelima michikichi na inaanza kutoa matunda. Hata hivyo, bado mahitaji ya miche ya michikichi ni makubwa sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iendelee kutusaidia miche ya michikichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunipatia miche 3,000. Mheshimiwa Waziri naomba uendelee kuniongeza miche mingine kwa sababu mimi ni mama ninayezunguka Mkoa mzima wa Kigoma na mahitaji ya miche ya michikichi ni ya Mkoa mzima. Kwa hiyo, naomba niongezewe miche mingine ya michikichi ili wananchi waweze kulima kilimo hiki na hasa wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile zao la alizeti nalo wananchi wameweza kuitikia kulima zao hilo. Naomba katika mikoa ile ambayo itapewa mbegu ya alizeti naomba na Kigoma nayo iweze kupewa kwa sababu alizeti inastawi katika Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, kwa sasa mazao katika Mkoa wetu wa Kigoma mahindi na maharage kwa wakati huu wanapovuna bei ipo juu kidogo. Niendelee kumwomba Mheshimiwa Waziri mipaka iwe wazi ili wananchi waweze kuuza mazao yao nje ya nchi, kwa sababu wakiuza mazao yao nje ya nchi wanapata bei ambayo ni nzuri. Kwa hiyo, wanaweza kunufaika wao wenyewe, lakini wanarudisha gharama wanazozitumia wakati ule wanapokuwa wanalima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzunguma maneno hayo, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)