Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimesikiliza hotuba ya Waziri Mheshimiwa Bashe. Mheshimiwa Bashe ni ni Waziri wa 27 wa kilimo katika nchi hii toka tumepata Uhuru. Katika hao Mawaziri 27 ni kwamba tulikuwa tuna Mawaziri wanane baada ya kupata Uhuru. Mawaziri hawa wanane walisimama katika uzalishaji wa mazao makuu sita katika tuliyokuwanayo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hawa Mawaziri wanane tuliokuwanao katika utawala wa Hayati Baba yetu wa Taifa Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere, ni Waziri mmoja tu aliyekaa katika miaka mitano; 1975 mpaka 1980, Mheshimiwa John Malecela ambaye yuko hai, katika miaka yake mitano alisimamia mazao sita ya kimkakati. Zao la kwanza likiwa pamba; zao la pili likiwa kahawa; zao la tatu, mkonge; zao la nne, korosho; zao la tano, chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mazao yalileta pesa nyingi sana za kigeni, lakini mazao haya yalionesha biashara. Mapinduzi ya biashara yalianza kuonekana katika misimu yetu katika nchi hii, ikawa ni misimu yenye kashikashi ya biashara. Unajua kwamba mwezi wa sita bei itatangazwa ya pamba, mwezi fulani itatangazwa bei ya Kahawa na mwezi fulani itatangazwa bei ya kitu fulani, mwezi wa kumi itatangazwa bei ya korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili lilileta mapato makubwa katika nchi hii; na idadi yetu ya wananchi katika nchi hii walikuwa ni wachache, leo nchi inakwenda kuwa na wananchi zaidi ya milioni 60, lakini tumeondoka katika haya mazao yetu ya kimkakati, haya mazao yameachwa. Nawe Mheshimiwa Bashe sasa hivi tunavyozungumza, ni kwamba umekuja kuongeza mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mpo katika Wizara yenu ninyi, hii ya kilimo katika mwaka 2011 mpaka leo, wamekaa Mawaziri zaidi ya wanane na wewe hapa sasa hivi unakuwa ni Waziri wa tisa. Mmeongeza zao la mchikichi, mmeongeza zao la alizeti, mmeongeza zao la mpunga, mmeongeza mahindi na parachichi kama matunda, lakini hayo mazao yote ya kimkakati, ninachoona mimi, ushauri wangu Mheshimiwa Bashe ni kwamba lazima ifikie mahali mkamshauri Mheshimiwa Rais kwamba tunahitaji sasa wawepo Manaibu Wawili katika Wizara yako. La sivyo, utachoka. Huwezi kusimamia mazao ya kimkakati 12, wakati huo huo mwende katika mazao mengine mchanganyiko, na wakati huo huo tunataka mbolea, wakati huo huo tunataka viuatilifu, itakuwa ni ngumu sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba bajeti hii ya kilimo ni ya kwanza toka tumepata Uhuru ya kiwango cha juu kiasi hiki. Inaonesha dhamira ya Mheshimiwa Rais moja kwa moja kwenda kwa wakulima kuwasaidia waweze kutoka. Sasa kama tunataka tutoke kwa kilimo hiki tulichonacho, nimekuona Mheshimiwa Bashe umejitahidi sana. Wewe ni miongoni mwa Manaibu Waziri waliokaa na Mawaziri tofauti karibu miaka sita. Ni Naibu Waziri pekee katika nchi hii aliyekaa kwa miaka mingi, alikuwa ni Sumaye. Sumaye amekaa kwa miaka 10 kama Naibu Waziri, na baadaye akafanya vizuri akaja kuwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na historia ya Wizara Kilimo ilivyo, Manaibu mnaokuja kupata nafasi hii kuwa Mawaziri wa Kilimo mmepita katika changamoto nyingi katika nchi hii. Sasa nafasi yako kama kijana, uende kwa hawa wazee, bado wako hai; nenda kwa Malecela ukamsikilize aliwezaje ku-perform? Nenda kwa Sumaye ukamwulize, aliwezaje ku-perform? Kwa sababu naye alikuwa kijana kama ninyi. Leo mkiacha kuwasikiliza hawa wazee, ni kwamba bado mtapewa fedha nyingi na hamtaweza kuzifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kwamba hizi pesa zilizotajwa kwa wingi wake, ni kwamba kwenye irrigation tayari kuna ongezeko kubwa la pesa tumepewa, kwenye utafiti kuna pesa nyingi tumepewa. Sasa hizi pesa zigawanyike vizuri katika suala la utafiti. Ushauri wangu ni kwamba, hivi vituo vyetu vya utafiti, kuna TARI halafu kuna Mwanza pale Ukiriguru, tunaomba waingie katika utafiti katika mazao haya ya kimkakati. Tuangalie mbegu gani ambazo zitakazoweza kutumika na mbegu ambazo tutaweza kutoa mazao mengi ndiyo zifanyiwe kazi. Pia gharama za utafiti pia mziangalie sana, zinaweza zikawa kubwa na zisije kuwa na tija. Hili uliangalie sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine cha msingi katika jambo hili ni kwamba tunakuja kuzungumzia suala la umwangiliaji. Tumepata skimu nyingi sana za umwangiliaji katika nchi hii, zinakuja kuongezeka na fedha mmepewa nyingi za kutosha. La kwanza ambalo linanitia shaka, kwenye kituo hicho cha umwangiliaji hapo Iringa Road, hao watu wanaokaa pale kwa ajili ya utafiti wa umwangiliaji na kushughulika masuala ya umwangiliaji wanakaa kwenye mabanda ya stoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hawa watu mnaenda kuwapa zaidi ya Shilingi bilioni 200 na kitu, kama 300, angalia na ofisi zao hao watu wanazokaa. Wanakaa garage. Mimi nimeenda juzi kuangalia, wapo garage Mheshimiwa Waziri. Unayeenda kumpa pesa kiasi hicho, bado hata ofisi hana, itawezekana wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika suala hili ni kwamba usiangalie mabwawa ya irrigation peke yake, lazima mchimbe visima tuingie katika umwangiliaji wa visima. Wenzetu Kenya sasa hivi wanamwagilia mashamba yao kwa kutumia visima. Hapa tumefaulu.

(Hapa kengele ililila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine, naona kengele imelia…

MWENYEKITI: Ndiyo Mheshimiwa. Muda wetu wa kuchangia asubuhi hii umeisha.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Dah, sasa…

MWENYEKITI: Malizia kuunga mkono hoja.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ni mdogo, naogopa kuunga mkono hoja.

MWENYEKITI: Muda wetu umeisha kwa sababu time ya asubuhi ndiyo hiyo imeishia hapo.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.