Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kunijalia afya njema niweze kusimama hapa. Baada ya kilio kusikika cha zao la soya naamini Wizara imeelewa vizuri, itafanya marekebisho kidogo ili kilimo cha soya kiweze kuenea Tanzania nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba nijielekeze katika maeneo machache kama mawili matatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wote; na niwakumbushe kwamba hakuna Taasisi hata moja iliyoanzishwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo haikuanzishwa kwa makusudi. Nianze na Food Security. Kama Taifa lazima tuwe na uhakika wa chakula ndiyo maana ilianzishwa Food Security ikaja ikaitwa Strategic Grain Reserve ikaja ikaitwa National Food Reserve Agency. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kusahau kwamba ukitaka kupata mazao yaliyo bora lazima ujihakikishie kwamba unakuwa na mbegu iliyo bora, lazima uhakikishe kwamba pembejeo kwa maana ya mbolea inapatikana iliyo bora; na ndiyo maana zikawepo TFC, na NRFA. Pia kukawa na Taasisi ambayo inachunguza na kuhakikisha kwamba tunakuwa na pembejeo zilizo salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa katikati kuna kosa kubwa ambalo kama Taifa tulitaka kufanya. Nashukuru Mheshimiwa Waziri umekumbuka kuhakikisha kwamba tunaifufua TFC kwa kuiwezesha kimtaji na kuhakikisha kwamba hii habari ambayo umekuwa unahangaika na makampuni ya watu binafsi kwa kuwa cartel na kuwa na bei ambazo mwananchi wa kawaida hawezi kumudu. Hakika kwa kuwawezesha kampuni hii nina uhakika kama taifa tutakuwa na uhakika wa pembejeo kumfikia mwananchi wa kawaida, na hasa mbolea, na kule Kalambo zitafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nikuombe Mheshimiwa Waziri, kwa sababu fedha ambayo tunayo kwa ajili ya ruzuku haitoshi. Ikupendeze kwamba kwa taasisi ya Serikali ambayo una uwezo wa ku-monitor na kufuatilia kuhakikisha inamfikia mwananchi ambaye umemkusudia tuanzie na taasisi hii, tukipata nguvu ndipo tuje kwenye hizo kampuni nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba kampuni nyingine zinataka kupeleka kule ambako wanapata faida. Nimeshuhudia hivi karibuni ukawa unakimbizana nao, wanaweka bei ambayo mwananchi wa kawaida hawezi kumudu hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nikumbushe, kuna taasisi moja inaitwa Early Warning and Crop Monitoring, kilikuwa ni kitengo katika Wizara yako ambacho kilikuwa kinakupa taarifa mwenendo wa hali ya chakula nchini na kama Serikali inaweza ku-make decision timely. Ni vizuri kitengo hiki ukakifufua ili kifanye kazi iliyokuwa imekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo na baada ya kuwa na uhakika kwamba zao la soya limeeleweka kilichobaki tu ni maeneo ambayo umesahau kutaja. Maeneo ya Mikoa wa Songwe, Rukwa lakini Manyara pia soya inakubali. Naamini sasa tunaenda kufanya mapinduzi makubwa tuhakikishe kwamba tunakuwa na mafuta ya kutosha nchini na mafuta ambayo yako bora. Mungu akubariki, mapinduzi haya ambayo yameanzishwa na Mheshimiwa Rais wa Tanzania asilimia zaidi ya 75 watanufaika na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)