Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Robert Chacha Maboto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kwa ajili ya Taifa letu. Juzi ameongeza asilimia 23 ya mishahara ya watumishi wa Serikali, ambao naamini ametimiza wajibu wake kwa nafasi yake, lakini na watumishi wa Serikali kwa sehemu yao na wao wana sehemu yao ya kutimiza wajibu wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo maji ni uhai, chakula nacho ni uhai, lakini pia huduma za afya nazo ni uhai. Kilimo ni uti wa mgongo wa kwetu sisi Tanzania, lakini pamoja na kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu, wakulima wetu uwezo wao wa kulima chakula chao, tofauti na mikoa mitano, mikoa mingine wananchi wetu wanalima chakula chao ambacho hakiwezi kuwatosheleza hata kwa mahitaji yao kwa mwaka, jambo ambalo ni hatari kubwa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo matatu ni mambo muhimu kwa afya ya binadamu. Leo mimi Mbunge nasimama Bungeni kuzungumza bila ya kuwa na afya bora, bila ya kunywa maji, bila kula chakula, uwezo wa kuzungumza sitaupata. Kwa hiyo, najaribu kuishauri Wizara ya Kilimo kwamba suala la chakula ni suala muhimu. Jambo muhimu hapa Taifa letu litengeneze utaratibu au Wizara na wataalam wetu wa kilimo, nchi yetu iwe na uwezo wa kujiwekea akiba ya chakula kwa muda angalau miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za wenzetu wao wana mafuta yao kwa sababu uwezo wao ni mafuta yao wamejiwekea akiba ya kutosha, wanaweza wakaamua kuyafungia mafuta yao halafu sisi huku Tanzania tukawa tunalalamika, wakati hatuzalishi. Sasa na sisi kwa nchi yetu kwa sababu Mungu ametupa ardhi, na mvua tunapata kwa kiasi cha kutosha, ningeishauri Wizara ije na mpango wa kuhakikisha kwamba nchi inajiwekea akiba ya chakula kwa muda wa miaka mitano, angalau ikitokea siku moja au miaka miwili au mitatu mvua hainyeshi, wananchi wetu waweze kupata chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi tunayo, mvua tunapata ya kutosha, lakini bado wakulima wetu chakula wanachokilima hakitosheleza mahitaji yao ya mwaka. Napata tabu sana kwenye jambo hili. Kila jambo sisi kama nchi au Wizara hatutakuwa na uwezo wa kujitosheleza, ardhi tunayo mvua tunapata, halafu wakulima wenyewe wanalima chakula kidogo ambacho hata wao wenyewe hakiwatoshelezi. Kwa hiyo Wizara itengeneze utaratibu au mkakati wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanahamasishwa kuhakikisha kwamba wanajilimia chakula ambacho kinawatosheleza kujilinda kwa mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mara hasa Wilaya ya Bunda zao kuu la kibiashara pale lilikuwa ni pamba, lakini leo pamba takribani miaka 10 haifanyi vizuri. Sio kwamba wakulima wale walikuwa hawana uwezo wa kulima isipokuwa tatizo ni soko, soko limeleta tabu, kwa hiyo limesababisha wale wakulima, badala ya kulima pamba sasa na kwa sababu wanalima pamba halafu uwezo wa kupanga bei hawana, anayewapangia bei mtu mwingine, wao wamekata tamaa ya kulima pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wananchi wetu wamerudi kuwa maskini. Naiomba Wizara ya Kilimo kwa sababu ina wataalam wa kilimo ambao wao wanaweza kutusaidia kututafutia zao mbadala hasa Mkoa wa Mara ambao sisi zao letu kuu la kibiashara lilikuwa ni pamba ili kwamba zao lile Wizara itakalotuletea lipate kuwasaidia wananchi wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kwa mchango mzuri.

MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)