Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya. Pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa suala la mbolea. Mbolea ya Tanzania imekuwa ni changamoto sana kwa wakulima wetu kwa sababu imekwenda juu sana. Jinsi ambavyo mbolea imepanda ukiangalia mwaka jana, mfano kwenye Mkoa wa Arusha, 2021 Sulphate Amonia ilikuwa ni Sh.45,000 kwa mfuko wenye kilo 50, lakini mwaka huu ni laki Sh.145,000. Hili ni ongezeko kubwa sana. Ukiangalia 2021 Urea ilikuwa Sh.65,000, mwaka huu 2022 ni laki Sh.150,000. Ukiangalia mbolea ya kupandia DAP ni Sh.75,000 mwaka jana, lakini mwaka huu ni laki Sh.165,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni janga kwa wakulima wa Tanzania kwa sababu hawana uwezo wa kufikia kiwango hicho cha mbolea kupanda. Ukiangalia wale wananchi wangu wa Kata za Ikiding’a ambao wanatumia mbolea Sambasha, Olomontoni, Soko Ntu, Nimnyaki na Oldonyosambu hawana uwezo ya kununua mbolea kwa gharama kubwa hivyo. Tunaishauri Serikali kwamba lazima ifike mahali iweke ruzuku ya kutosha kwenye mbolea ili wakulima wale wadogowadogo na hata wale wa kati waweze kumudu mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mbegu, nalo ni changamoto. Kumekuwepo na mbegu feki zinazoingizwa nchini na Mawakala, mbegu ambazo hazina tija, imekuwa kama ni kilio wale wakulima wanaponunua mbegu, wakidhani wananunua mbegu bora, wanaona ni bora wangerudi kwenye zile mbegu zao za zamani, kwa sababu umekuwa ni utapeli, watu wanachukuwa rangi, wanaweka kwenye mahindi, hivyo wakulima wanaona kama ni mbegu bora lakini kumbe ni mbegu feki. Hili nalo tunaishauri Wizara iangalie suala la mbegu hasa kwa kuwaangalia watu wanaouza mbegu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la madawa ya kunyunyuzia mimea, kwa maana ya mazao, nalo hili ni janga kwa sababu wakati mwingine madawa yananunuliwa, lakini hayana uwezo wa kuuuwa wadudu katika mazao. Kwa hiyo hili nalo naomba Wizara iliangalie na Mheshimiwa Bashe sina wasiwasi naye na Naibu wake kwamba kazi hii wanaiweza na wanaiweza kwa dhamira ya dhati, niwaombe sana kwamba kazi hii kubwa waliyekabidhiwa na Mheshimiwa Rais waweze kuifanya kwa uaminifu na uadilifu ili mwisho wa siku wapate karama yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwamba mwaka huu katika maeneo mengi hasa ukanda wa Kaskazini kuna upungufu wa chakula kwa sababu mvua ni kidogo. Kwa hiyo, naomba pia Wizara ilione hili na kulichukua kuwe na tahadhiri ya kwamba kutakuwepo na suala la upungufu wa chakula katika Ukanda wa Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila jambo wakati ule wa Serikali zingine zilizopita za kwetu kulikuwa na slogan mbalimbali, Siasa ni Kilimo, Kilimo ni Uti wa Mgongo. Haya yote ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunahamasisha jamii na Serikali kwa ujumla kujihusisha na kilimo ili kuleta tija ndani ya Taifa letu. ninaomba Serikali yetu kama mnavyojua sehemu kubwa ya Watanzania wanapata ajira kupitia kilimo, kama tunasema tunaongeza ajira Mheshimiwa Bashe na Naibu wako mnayo kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata ajira kwenye kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tukitumia mashamba makubwa ya kilimo na mkayafuatilia kwa makini mashamba yote yanayojihusisha na kilimo na masuala ya umwagiliaji tutaongeza suala la ajira kwa vijana wetu na wengine wote kwa ajili ya kuinua uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo mpaka shamba liwe pori ndiyo muweze kufuatilia, fuatilieni mashamba ya kilimo hata kabla hayajawa mapori, mwisho wa siku wale wanatelekeza mashamba na wamekopa kwenye benki mbalimbali, wakishakopa wakidhani wanaendeleza hayo mashamba lakini mwisho wa siku wanatelekeza yanakuwa ni mapori, ndiyo Serikali tunakuja kushtuka sasa tunasema uzalishaji wa maeneo hayo umekufa. Kwa hiyo, nayasema haya nikiamini kwamba Waziri na Serikali kwa ujumla itaona kwamba inafuatilia mashamba yote ya kilimo ili kuleta tija kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)