Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, napenda kuwapa pole wananchi wangu Ulanga kwa janga la ajali ya kivuko. Ajali hii ya Ulanga siyo ya kwanza, nashangaa Ulanga sijui tumeikosea nini Serikali hii. Daraja mwaka wa tatu haliishi, miradi yote mikubwa inakuja inakwisha, ile ya Kigamboni imekwisha, mradi wa mabasi yaendayo kasi umekwisha, daraja la Ulanga haliishi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wakandarasi waliopewa mradi ule kila mwaka wanaomba kuongezewa muda. Nashangaa wakati wanaomba kujenga lile daraja walikuwa hawajui kama kuna kipindi cha masika? Kwa mfano, sasa hivi hawapo, ujenzi hauendelei. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Fedha alisimamie suala hili kwa sababu sasa hivi mafuta hayaendi Ulanga, bidhaa haziendi Ulanga, vile viboti vidogo walivyoweka kwa ajili ya kuwavusha watu mvua zikinyesha haviwezi kufanya kazi. Mimi mwenyewe shahidi juzi nilivyoenda nimenusurika kifo. Tumefika katikati ya mto boti limezimika. Kwa hiyo, ili kuwanusuru wananchi wa Ulanga naomba tuwasaidie kile kivuko kisitumike tena, daraja liishe wananchi wanufaike na daraja lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuongea katika Bunge hili, naomba nimpongeze Rais Magufuli na uongozi wote uliochaguliwa. Nampongeza Mheshimiwa Magufuli kwa utendaji wake, nawashangaa ndugu zangu Wapinzani wanasema kuwa Mheshimiwa Magufuli anatekeleza Ilani yao, sasa kama anatekeleza Ilani yenu mbona mnalalamika. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuongea Bungeni, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya familia, kwa ofisi za Bunge kwa namna walivyoshughulikia ugonjwa wa mama yetu mpendwa Celina Kombani, walivyoshughulikia shughuli yote ya msiba. Napenda kutoa shukrani za pekee kwa mama yangu Mheshimiwa Hawa Ghasia, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Mheshimiwa Angellah Kairuki na Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa jinsi walivyolichukulia suala lile na kuchukua nafasi ya mzazi. Naomba waendelee kutuchukulia hivyohivyo kama watoto wao, hatuna cha kuwalipa bali tunawaombea maisha marefu yenye afya na mafanikio makubwa. Pia siwezi kusahau uongozi wa Chama cha Mapinduzi kwa namna walivyotusaidia katika msiba ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Rais mstaafu Mheshimiwa Jakaya Kikwete kwa uongozi wake mahiri wa miaka kumi kwa kutunza amani na utulivu. Pia napenda kuipongeza Serikali ya CCM kwa kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa demokrasia ya hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa kusoma kwake hotuba kwa umahiri. Ila nilikuwa napenda kumwambia kuwa katika level ya Ubunge kuna vitu vya ku-present mbele za watu siyo kila anachoandikiwa asome. Akili za kuambiwa uchanganye na za kwako. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ku-declare interest nimeoa mchaga, Mheshimiwa Mbowe ni mkwe wangu, sasa mkwe kuonyesha udhaifu mbele ya mkwe wake ni aibu. Tunapozungumzia Upinzani Bungeni tunamzungumzia Mheshimiwa Mbowe. Sasa naomba nimpe taarifa kuwa mkwe wake nipo humu Bungeni, hatakiwi kuonyesha udhaifu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mpango wa kuimarisha umeme vijijini, naomba niwape taarifa, kipindi cha masika Ulanga umeme haupatikani. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Muhongo umeme umefika Ulanga lakini zile fito walizoweka za kupeleka umeme kipindi cha masika zote huwa zinavunjika kwa hiyo hatupati umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mto Kilombero pale unatuletea mafuriko kila mara. Naomba ufanyike mradi kama ulioko Mto Ruvu. Badala ya mto ule kutuletea mafuriko tutumie yale maji kwa kuyanywa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kusahau upande wa viwanda, Ulanga kuna Kiwanda cha Pamba lakini hakijaingizwa katika mpango huo wa kufufuliwa. Nimeona sehemu zingine tu lakini Ulanga imesahaulika. Bila kuisahau Morogoro, Morogoro ndiyo ulikuwa mkoa ambao unaongoza kwa kuwa na viwanda vingi lakini sasa hivi yamebaki magofu, sijaona mpango wa kufufua viwanda vya Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi na kwa sababu ndiyo naanza haya yanawatosha. (Kicheko)