Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye amenipa mimi umaarufu na kuwa Selemani Bungara Bwege, pia kwa kukupa Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa mjanja kwa hiyo, namshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, nawashukuru wapiga kura wa Jimbo langu la Kilwa Kusini, mwaka 2010 nilishinda kwa kura 500 kuna watu wakasema wewe umemuonea tu Madabida nitamwita Mhindi Bin Asineni, mwaka huu nimempiga kwa kura 5,595. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba CCM mjiandae mumlete mgombea mwingine nimpige tena. Kwa mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili mambo mengi yamesemwa hapa, lakini naomba vijana wangu wa upande wa UKAWA msiwe na wasiwasi, humu ndani sasa hivi hatupambani na Serikali ya CCM, humu tunapambana na Serikali ya Magufuli na tunapambana na Serikali ya Mapinduzi, CCM hamna Tanzania sasa hivi, hii ni Serikali ya Magufuli na Serikali ya Mapinduzi.
Sasa mkitambua kwamba tunapambana na Serikali ya Magufuli, tusimlaumu sana Magufuli kwamba ndiyo kwanza anaanza na wamekubali wenyewe Serikali ya CCM kwamba tulifikia hapa na udhaifu huu ni kwa ajili ya Serikali iliyopita ya CCM, hii sasa ni Serikali ya Magufuli. Kwa hiyo, tutamwona Mheshimiwa Magufuli kwa miaka yake hii mitano atafanya nini akishindwa na yeye tutamwajibisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nawashukuru sana vijana wangu wa UKAWA tushirikiane tuzidi ili 2020 tuielekeze kibla Serikali ya Magufuli maana yake CCM tena hakuna nchi hii. Waheshimiwa nimepokea pole, kuna watu hapa wametaka kulia hapa eti kwa sababu…
Bunge lisioneshwe live wanataka kulia, aah, mimi nilifikiri wanataka kulia kwa sababu watu hawapati maji vijijini…
TAARIFA....
MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa siipokei kwa sababu anapingana na mwenyewe Mheshimiwa Magufuli, kila siku anasema kwamba Serikali yangu, wakati mwingi anasema Serikali yangu hasemi Serikali ya CCM, kwa hiyo siipokei taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu bado saba ilikuwa tatu tu, narudia kusema kwamba napenda sana Wabunge msililie kwamba Bunge lisioneshwe live mlie kwa kuwa watu hawapati maji, hawapati tiba vizuri, hawapati elimu. Nashangaa sana mtu anayelia anaomba kulia, mimi ninavyojua kulia kuna mambo mawili tu, utamu au uchungu, na ukipata utamu au uchungu huombi kulia unalia tu, ukimwona mtu anaomba kulia au anatamani kulia hataki kulia huyo. Ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naanza na mambo ya viwanja vya ndege, katika kitabu ukurasa wa 99 nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwamba anaanza mchakato katika Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko, nimefurahi sana, lakini Uwanja wa Kilwa Masoko walikuja kutathmini mwaka 2013 na tathmini ya uwanja ili upanuliwe bilioni mbili, milioni themanini, laki nne na sitini elfu mia mbili na sitini mpaka leo, wametathmini watu wale hawajawalipa. Leo wanasema wanafanya mchakato ili wapanue sasa kabla bado hawajafanya mchakato huo wakawalipe wapiga kura wangu, 2,080,460,260, mkawalipe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013/2014, 2015/2016, wanawaambia wasiendeleze majumba wala wasilime mashamba yao mwaka wa tatu sasa hivi au wa nne. Naomba sana katika majumuisho ya Mheshimiwa Waziri aniambie kwamba lini watakwenda kuwalipa wale watu ili waendelee na mchakato wa kuupanua uwanja huo. Kama hawakuniambia lini wanataka kuwalipa nashika shilingi. Najua mtapiga kura nyinyi mko wengi, lakini shilingi mimi nitaishika safari hii isipokuwa katika majumuisho yake akiniambia watawalipa lini kesi imekwisha kwa sababu Serikali ya Magufuli ndiyo kwanza inaanza, sisemi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili barabara, katika ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyepita kulikuwa na ahadi ya barabara ya kwa Mkocho – Kivinje, lakini mpaka leo. Mheshimiwa Majaliwa alikuwa Waziri akasema kabla ya Uchaguzi, uchaguzi umekwisha, naomba Waziri Profesa, Msomi leteni hela hizo barabara ya kwa Mkocho – Kivinje ijengwe, maana yake kuna watu hapa wa CCM wanasema Majimbo upinzani usipeleke hela, jamani ehee mimi nilipata kura elfu kumi na tano, Asineni elfu kumi, Mheshimiwa Magufuli alipata elfu kumi, Mheshimiwa Lowassa alipata elfu kumi na nne, haya hizi elfu kumi za Mheshimiwa Magufuli ndiyo zimemfanya yeye ashinde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukisema kwamba Jimbo la Kilwa huleti maendeleo kwa sababu Magufuli hakushinda mnawaumiza elfu kumi waliomchagua Magufuli, haki sawa kwa wote timizeni. Sina wasiwasi, kama hamkuleta hayo nitashinda zaidi kwa sababu kila ukimuumiza mtu wa Kilwa basi anazidi kupata uchungu anaipiga CCM, leteni Maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nangurukuru – Liwale itiwe lami, sisemi sana amesema Mheshimiwa Bi Lulida hapa, Naiwanga – Nainoko – Ruangwa mtengeneze, mjenge. Kilanjelanje na Njilinji mmepanga milioni 85, jamani ehee milioni 85 haifai, haitoshi tuongezeni hela, mvua ya mwaka huu, mafuriko ya mwaka huu barabara yote imekufa tunaomba hela iongezwe, naomba sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, siisemi sana Serikali ya CCM kwa sababu tayari ishashindwa na wenyewe Mawaziri mmesema kwamba Serikali yetu ilikuwa dhaifu, ilikuwa haikusanyi hela, ilikuwa hivi, lakini Serikali ya Magufuli inakusanya hela haina udhaifu, wala siilaumu Serikali ya CCM iliyopita, najua nitailaumu Serikali ya Magufuli mwakani siyo mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, kuna vijiji kumi havina mawasiliano ya simu Nainokwe, Liwitu, Kikole, nawaomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri watuletee mawasiliano watu wapige simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya, bandari, nimeangalia humu Bandari ya Kilwa haipo, lakini gesi ya Kilwa akisimama Mheshimiwa Muhongo hapa, gesi ya Kilwa italeta mambo, ehee, lakini watu wenyewe wa Kilwa thuma amanu thuma kafara. Naomba bandari nayo muiangalie, sasa gesi hiyo mngeipitisha wapi? Naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, sisi watu wa Kusini mnatuonea, maendeleo yote mnawapa watu wenye maneno mengi tu huku. Sisi wengine hatujui kusema, wanyonge, tunaomba Serikali ituangalie. Kuna mradi wa maji, kuna wafadhili kutoka Ubelgiji, basi mpaka leo hawataki kutuletea, tangu mwaka 2014, Mbelgiji amesema anatuletea maji hamtaki kutuletea maji. Kwa sababu gani, sisi watu wa Kusini tu! Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.