Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu. Kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuletea bajeti hii ambayo sasa imeakisi kwamba Serikali imekuwa na dhamira ya dhati kabisa kuweza kumkomboa mkulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza pia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote wa Wizara kwa ujumla kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Pamoja na dhamira kubwa ambayo Serikali imeendelea kuifanya kwenye Wizara hii, tunaona namna ambavyo kule kwetu ambako tunalima zao la tumbaku wameweza sasa kuona umuhimu wa zao hili na kuhakikisha kwamba tunakwenda kupata makampuni mengine zaidi kwa ajili ya kununua zao la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali imepata kampuni, kampuni ya AMIS ambayo nayenyewe tayari imeshachukua kiwanda cha kichakata tumbaka pale Morogoro na wametuhakikishia kwamba kwenye mwaka huu wataweza kununua tani milioni 10, tunawapongeza kwa kazi kubwa ambayo mmefanya, yale ambayo tulikuwa tunawashauri mmeyachukua na mmeenda kuyafanyia kazi, tunawapongeza kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo hii kampuni imetuhakikishia kwamba mwaka ujao wa kilimo itanunua tani Milioni 30, hii maana yake tunaenda kuongeza makisio kwa wakulima wetu wa zao la tumbaku na tutakapoongeza makisio watalima zaidi na wanapolima zaidi maana yake uchumi wao utakukua. Ninawaambia wakulima wangu wa Tarafa ya Kipembawe Wilaya ya Chunya wajiandae sasa kampuni hii inakuja, makisio yataongezeka hivyo uchumi wa eneo husika utaenda kukuwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo bado kuna changamoto kwenye mbegu na miche ya tumbaku. Tumeona kwenye hii bajeti upande wa utafiti, maeneo mengine wamewekewa fedha lakini upande wa mbegu za tumbaku na miche ya tumbaku hawajawekewa fedha, hii kampuni ya utafiti ya TORITA haijawekewa fedha. Ninaiomba Serikali kama ina dhamira ya dhati kabisa ya kuhakikisha kwamba zao hili linaenda kumkomboa mkulima mwaka ujao waweke fedha ili ziweze kuwasaidia kupata mbegu ambayo ni bora na tunaweza kupata tumbaku ambayo ni nzuri zaidi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu watu wa Malawi pamoja na Zimbabwe wamewekeza kwenye utafiti, wamewekeza kwenye mbegu bora za tumbaku. Wao wanapata tumbaku yenye daraja la juu zaidi. Sisi tumbaku yetu iko chini na ndiyo maana hata bei ya tumbaku Tanzania iko chini. Tuna wastani wa dola 1.4 mpaka wastani wa dola 2.2 ambayo iko chini, wakati wenzetu wananunua kuanzia dola mbili na kitu na bei ya juu ni dola nane. Kwa hiyo, tukiwekeza huko tutaweza kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nizungumze habari ya pembejeo. Serikali imeongeza ruzuku kwenye bajeti hii kwa ajili ya pembejeo, ni jambo zuri sana, nasi tunapongeza kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya. Tunampongeza sana Waziri kwa ubunifu wake huo. Tuna imani wakipata fedha ambazo wameziomba, bei ya pembejeo inaenda kushuka. Sisi sote tumekuwa mashahidi huu musimu wa kilimo uliopita hapa, bei za pembejeo zilikuwa hazishikiki. Kila Mbunge hapa alikuwa analalamika kwamba pembejeo ziko juu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)