Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwepo hapa leo kutekeleza majukumu yetu ya Kibunge. Pia nichukue nafasi hii kukushukuru wewe binafsi na Wenyeviti wa Bunge, kwa kusimamia mjadala wa hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha, 2022/2023 ambao tunauhitimisha leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii vile vile kushukuru mchango mkubwa uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. Kwa dhati kabisa nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwani wametoa hoja nzuri sana, zenye malengo ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu katika Wizara yangu na kuharakisha mapinduzi ya kilimo. Hii inaonesha umuhimu wa kilimo katika usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa shukurani zangu za dhati kabisa kwa Naibu Waziri Mheshimiwa Antony Peter Mavunde, kwa kuchangia hoja hii na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizojitokeza. Niwashukuru pia Katibu Mkuu, Bwana Andrew Massawe; Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Profesa Siza Tumbo na Ndugu Gerald Mweli; pamoja na Watendaji wote wa Wizara na Taasisi zake, kwa ushirikiano na ushauri wanaoendelea kunipa katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba kuwasilisha maboresho katika kitabu cha Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mwaka wa Fedha, 2022/2023. Aya ya 61 ukurasa wa 35 jedwali Na. 4 mchanganuo wa matumizi ya fedha zilizotolewa kwa Mafungu yote matatu kwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla kuu ni shilingi bilioni 151,863 badala ya shilingi bilioni 272,931. Aidha, matumizi ya shilingi bilioni 151,863 ni asilimia 51.63 ya fedha zilizoidhinishwa na sio asilimia 92 kama zilivyooneshwa katika jedwali. Aya ya 366, ukurasa wa 194 inaonesha kuwa katika kuongeza thamani kipato cha mkulima na kupunguza upotevu wa zao la zabibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kujibu hoja za Wabunge ambao wametoa mawazo yao. Hoja yetu imechangiwa na Wabunge 92 kwa kuchangia na vile vile imechangiwa kwa maandishi na Wabunge 10. Naomba nianze kuongelea eneo ambalo Waheshimiwa Wabunge wametoa maoni ya muda mrefu. Naomba nianze na Mheshimiwa mama Anne Kilango Malecela, kwanza nikiri mimi nikiwa Naibu Waziri wakati huo Waziri wangu Profesa Adolf Mkenda, alinituma na nimekwenda Jimboni kwake na nimefanya survey, nimetembelea wakulima wote wa tangawizi. Vilevile nimeitembelea scheme yake ambayo ilijengwa na Baba wa Taifa ya Ndungu na nikaenda mwenyewe kufika pale na kutatua changamoto zile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie hana sababu ya kuondoka na shilingi ya kijana wake. Nataka nimhakikishie mbele ya Bunge lako na kuwahakikishia wakulima wa tangawizi sio wa Same tu, lakini vile vile wakulima wa tangawizi wa Buhigwe, Wizara ya Kilimo baada ya miaka 38 tumelichukua zao la tangawizi tumelikabidhi Taasisi yetu ya Utafiti ya TARI Mlingano kuanza kufanya utafiti na kufanya multiplication ya mbegu, ili maradhi yanayowakabili wakulima wa eneo lile wanaolima tangawizi tuweze kuliondoa tatizo hili kwa kudumu na mazao yote ya viungo. Kuanzia mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya utafiti wa tangawizi na mazao mengine ya viungo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, nataka tu nimhakikishie Mama Anne Kilango, wataalam wa Wizara ya Kilimo wako Wilaya ya Same, wanafanya kazi kubwa mbili. Ya kwanza, watafiti wa TARI wamekwenda kuchukua sample za udongo na mazao ya tangawizi kwa ajili ya kuyapeleka maabara, tuweze kutambua maradhi halisi yanayowakabili wale wakulima wa pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, watu wetu wa Tume ya Umwagiliaji wanafanya kazi ya kufanya stadi kuitambua mifereji, kujua tufanye design ya namna gani kuweza kuweka mifumo ya umwagiliaji. Ndugu zetu wa Hai walituvumilia na mwaka huu tumeshatatua tatizo lao tumewapelekea fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwombe mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango asiwe na hofu wakulima wa tangawizi wa Wilaya ya Same wanakwenda kutatuliwa tatizo lao. Watu wa Tume ya Umwagiliaji wako kule, wanafanya design ili tuweze kujua tunatumia solution gani kuweza kuvuna maji yale na kuwaondolea matatizo ya muda mrefu ya wao kujiunganishia mipira kienyeji kwa ajili ya kupeleka mashambani kwao. Kwa hiyo, Serikali inalifahamu tatizo, lakini vile vile tunalifanyia kazi hatujawaacha na hatutawatupa mkono. Mwaka kesho kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu aje aniulize ndani ya Bunge hapa na anisute mbele ya Wabunge hawa na Watanzania kwamba, Hussein uliniahidi unakwenda kushughulikia tatizo la wananchi wa Same la tangawizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa linalowakabili wakulima wa tangawizi kule Buhigwe, wanavuna hawana sehemu ya kuhifadhi, mwaka huu tumewawekea fedha tunakwenda kuwajengea maghala. Nataka niwaambie wakulima wa tangawizi, Serikali inachukulia mazao yote ya viungo kwa u-serious mkubwa na hatutoyapa nafasi ndogo kama ambavyo miaka 30 iliyopita ilichukuliwa kwa style hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge wapo waliochangia na kusema kwamba, bajeti ya Wizara ya Kilimo ni ndogo haitoshi, ni kweli lakini kuna hatua ambayo tumepiga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na bajeti kwa zaidi ya miaka sita isiyozidi Shilingi bilioni 200, leo tunatenga bajeti ya Shilingi bilioni 751, asilimia 88 ya bajeti hii, inakwenda kwenye maendeleo, haiendi kwenye vikao, haiendi kwenye matumizi ya ofisi. Nataka tu nitaje maeneo ambayo tunapeleka. La kwanza tunapeleka kwenye suala la mbegu. Nataka niseme mbele ya Mungu na mbele ya Bunge hili, kama kweli nchi hii tunataka kuondoka kwenye matatizo, kwenye sekta ya kilimo, tusifanye maamuzi ya sekta ya kilimo kisiasa. Kilimo ni biashara, kilimo ni sayansi, kilimo ni teknolojia na kilimo kina basics. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwape hizi takwimu na ni vizuri kwa kuwa sisi ndio wawakilishi wa wananchi tufahamu. Nimechukua mazao 13 na ili food security ya nchi hii iweze kupatikana, tuna mazao mawili makubwa, mahindi na mpunga ndio mazao tunayokula Watanzania wengi. Swali la kujiuliza sisi, toka tumepata uhuru kati yetu tumewahi kukaa kujiuliza swali, tunahitaji mbegu bora tani ngapi ili tumpelekee huyu mkulima mdogo maskini kwa msaada wa Serikali ili aweze kwenda shambani? Nataka niwape hizi takwimu tunahitaji tani 652,000 kwa mwaka ili tuwagawie wakulima, sasa tujiulize swali tunazalisha tani ngapi? Tunazalisha tani 15,000 sisi na sekta binafsi, halafu tunaamini kwamba we are safe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mahitaji ya tani 652,000 uwezo wetu wa sekta binafsi na Serikali tunazalisha tani 15,000, ndicho tunachozalisha. Sisi kama Wizara na nawaomba mtuunge mkono. Tumekwenda kuongea na Mheshimiwa Rais, tumemwambia mama, cha kwanza kwenye sekta ya kilimo ni tija. Tija haiji kwa jina la Roho Mtakatifu wala haiji kwa kumwomba Mwenyezi Mungu kwa kupitia Mtume Muhammad, ina equation. Equation ya kwanza ni input na input namba moja ni mbegu, ni lazima kama nchi tujitosheleze kwa mbegu na tuwe na uwezo wa kuzalisha mbegu zetu. Sisi kama Wizara ndio tumekipa kipaumbele namba moja. Tunafanya nini? Bajeti ya utafiti imeongezwa kutoka shilingi bilioni 5.0 kwenda shilingi bilioni 43. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya uzalishaji wa mbegu tumeongeza kutoka shilingi bilioni 5.0 ya mwaka 2020 kwenda Shilingi bilioni 40.7. Zinakwenda kufanya nini? Cha kwanza, tunakwenda kufanya kazi kubwa moja; kwanza kwenda kuweka miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya mbegu. Haiwezekani mkulima anakwenda shambani na sisi Serikali ndio tunakwenda kuzalisha kwa kudra ya Mungu. Tunawaomba mtuunge mkono ili tupate tani 600,000 tunahitaji kuzalisha pre-basic seed. Kwanza tunatakiwa kufanya breeding tufanye pre-basic seed tuzalishe basic seeds halafu tuwape sekta binafsi na Serikali kwa ajili ya multiplication tuweze kuzipeleka kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni safari, tunaomba watuunge mkono Waheshimiwa Wabunge, tunakwenda kufungua mashamba ya Serikali. Nitumie Bunge lako Tukufu niiombe sekta binafsi ya Watanzania, waje Wizara ya Kilimo, tutawapa ardhi kwa mikataba ya muda mrefu, tutawagawia wazalishe mbegu, tutanunua kama Serikali na tutawagawia wakulima kwa ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili ambayo tumejiamulia kama nchi ni lazima tuwekeze kwenye umwagiliaji. Nataka nimkwambie hiki kipindi mimi ni Muislam, sio hamsa swalawat lakini naswali swali. Mvua zilivyokuwa zinachelewa, wewe tunaswali wote Gaddafi, kila Ijumaa Imamu anatuongoza kuomba dua na kufanya kunuti Msikitini Mungu alete mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya yote, Mwenyezi Mungu katupa akili, Mwenyezi Mungu katupa nafasi, Mwenyezi Mungu katupa ikolojia nzuri, ni suala la kuamua tunawekeza fedha zetu wapi? Tumekwenda kwa Mheshimiwa Rais, tukamwambia mama, naomba tuongezee bajeti ya umwagiliaji. Mheshimiwa Rais tumepata fedha tumeongeza bajeti ya umwagiliaji kutoka Shilingi bilioni 46 kwenda shilingi bilioni 361. Hata hivyo, tumesema nini? Tumeamua na nawaambieni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutayafanya haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niliombe Bunge hili hata kama Bashe hayuko Wizara ya Kilimo Mungu kamchukua, au kwa jambo lolote, Bunge hili lisimamie vision hii ya irrigation kwenye nchi. Cha kwanza, tulichoamua kwenye umwagiliaji tumesema hivi lazima tufanye comprehensive feasibility study and design kwa mabonde yote ambayo ni ya uhakika na tuanze kujenga mabwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeamua kufanya nini? Tunakwenda kufanya feasibility study na design ya Bonde lote la Rufiji, hekta 64,000 tumeweka Shilingi milioni 835. Tumeamua kwenda kuweka feasibility study bonde lote la Mto Manonga na Wembele hekta 57,000. Tumeamua kuchukua bonde lote la Kilombero hekta 53,000. Tumeamua kuchukua eneo lote la Usangule, Malinyi hekta 2,500 na tumeamua kuchukua Mkoa wa Ruvuma Bonde la Mto Ruvuma hekta 26,000. Katika hili nimewaambia wenzangu Wizarani mambo ya joint effort na neighbour’s country, tukikutana nao kwenda pamoja hewala, hawapo sisi tunaanza safari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwa tunakutana mikutano ya pamoja ya joint effort, vikao vya kuitwa Waziri tunakwenda, safari hii nimealikwa kwenye Ruvuma Basin sijakwenda kwa sababu I don’t see a reason, we can do our own design, tunaweza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya hekta 306,000 zinazohusu eneo la Ziwa Victoria kuanzia Mara mpaka Kagera; eneo la Lake Tanganyika; na eneo la Lake Rukwa, tunakwenda kufanya design mwaka huu na tunalifanyia design lote, tutaanza kujenga kuanzia mwaka ujao wa fedha. Tumeamua kujenga mabwawa na nataka kusema ndani ya Bunge hili na iingie on record, nadhani katika Mawaziri ambao, wamekwenda kukaa na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha mara nyingi, mimi ni mmojawao na namshukuru sana yuko hapa, anaelewa, ana-sympathize na anaunga mkono juhudi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunaweka effort kwenye irrigation? Nimewaambia watu wa Tume ya Umwagiliaji, ni hivi, haiwezekani tunajenga mradi tuna shilingi bilioni 2.0 unampelekea Hussein shilingi milioni 100, John shilingi milioni 2.0 nani shilingi milioni 3.0, mwisho wa siku mmegawana umasikini na hakuna kilichokamilika. Tukijenga scheme ya umwagiliaji tunajenga total package kuanzia water catchment na mifereji, ni heri tujenge scheme mbili kuliko kukaa tunagawana umaskini mdogo mdogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, priority yetu ya kwanza tunafanya feasibility study na kufanya design ya maeneo yote ambayo ni potential katika nchi, ili tunaposema kwamba mwaka kesho tunajenga nini tunajua tunakwenda kujenga sehemu ambayo hata nchi isipopata mvua mwaka mzima tunayo food basket ambayo inaweza kutulisha na kutuweka salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi tunazopeleka asilimia 90 zinakwenda kwenye development za irrigation, hakuna fedha inayokwenda kwenye matumizi ya kawaida. Mbali na hapo scheme nyingi zinajengwa katika nchi yetu, baada ya miaka miwili zimekufa. Nataka niwape mfano, Sheria ya Umwagiliaji inatutaka tukusanye Irrigation Development Fund, five percent katika kila scheme ambayo Serikali imewekeza. Niwape mfano Serikali imewekeza 21 billion shillings kwenye scheme ya Dakawa yenye hekta 2,000, turn over ambayo tunatakiwa tukusanye iingie kwenye Irrigation Development Fund ni 600,000,000 million shillings. Tumeamua ku-unlock hili tatizo kwa kufanya nini? Tunafungua Ofisi za Umwagiliaji kila Wilaya na kila scheme itakuwa na Meneja wa Skimu, ili tuweze kuzisimamia na wakulima wasimamiwe, wazalishe mara mbili kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapeleka manpower, tunapeleka vitendea kazi, tunanunua magari kwa ajili ya Irrigation Development iweze kufanyika katika nchi hii. Tunakwenda kufanya Luiche imekuwepo kwa muda mrefu lazima tufanye hivi vitu. Nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge, always na naomba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, Bunge hili lii-guide Serikali kwenye kilimo kwa kuhakikisha tunawekeza kwenye mambo ya msingi. Moja ni seed multiplication, kama hatuna mbegu zetu, kama hatuna umwagiliaji, kama hatua uwezo wa kum-subsidizing mkulima kwenye input, hatuko salama. Huu ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee issue ya mbolea, nitumie Bunge lako hili Tukufu, it is very danger kwenye capacity zetu tunaposimama mbele ya Bunge Tukufu na sisi ndiyo tunaowakilisha wananchi, tunapata air time and then we send a negative message and misleading information. Trend ya bei ya fertilizer duniani na mimi nimeamua niongee hapa. Kuna hoja inasemwa kwa nini Rwanda, kwa nini Malawi, kwa nini Zambia bei ya mbolea iko chini? Nataka niwapeni statistics za bajeti ya Rwanda mwaka huu. Rwanda for the last ten years amekuwa aki-subsidize input yake, hasa mbolea kwa support ya World Bank, WFP, FAO na wengine. Mwaka huu wa fedha Rwanda inatumia Dola Milioni 15 kutoa ruzuku ya mbolea. Ni sawasawa na asilimia 11.7 ya bajeti nzima ya kilimo ya Rwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Malawi anatumia Dola Milioni 131 ku-subsidize mbolea. Ni sawasawa na asilimia 44 ya bajeti nzima ya Malawi. Zambia ana-subsidize mbolea by 30 percent. Tena Zambia package yake ya subsidy ni mbolea na mbegu. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Tanzania?

WAZIRI WA KILIMO: Tumeanza kuchukua hatua. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutatumia Bilioni 150 kuanzia Tarehe Mosi.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bashe kidogo subiri. Waheshimiwa Wabunge hapa tunazungumza vitu very serious na kurukiarukia maneno ni nje ya utaratibu wa Kibunge. (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme haya mambo kwa uwazi na with respect nijibu hoja categorically ya Mheshimiwa Mpina. He has been a Minister katika Serikali, it is very danger kwenye capacity ya mtu ambaye ni Mbunge wa muda mrefu, amekuwa Naibu Waziri, amekuwa Waziri, kusimama Bungeni ku-present issue ambayo totally he is misleading the public. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya mbolea duniani siyo jambo la kuficha ni jambo liko kwenye public domain, it is a commodity like any other commodity. Hata uki-google unazipata taarifa za bei ya mbolea duniani. Nimechukua source yangu hiyo ni taarifa ya World Bank, a reputable organization. Bei ya mbolea Machi, 2018 DAP ilikuwa Dola 549, FOB rate an average price, today ni Dola 948. Urea Dola 134 leo ni Dola 723.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo jambo la siri, liko wazi halifichwi. Nipitie mbele ya Bunge lako nimuombe Mheshimiwa Mpina kama anayo source yoyote ya kunipatia mbolea ya bei rahisi aje nampa mkataba wa tani Laki Nne zote aniletee. Duniani kote wana-subsidize na mimi nataka niwaambie tusipotoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa nchi hii tutakuwa tunawaonea, tunawaumiza na hatuwatendei haki na hatulitakii Taifa letu uhai. Tusifanye siasa kwenye mambo hatari. Hii siasa ndiyo imeua kitalu cha mbegu ya pamba katika Jimbo lake. Ninawaomba, mimi ni very open na I am ready to bear any cost, this is what I believe, lazima tutoe ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaishia hapo kwenye ku-design ruzuku, tumeamua kufufua Kampuni yetu ya TFC. No where in the world, hii dhana ya kwamba, Serikali can not trade ni dhana iliyopitwa na wakati. Serikali ita-trade kwa sababu mbili, moja ku-make profit when it is necessary, lakini mbili ku-subsidize na ku-stabilize ndiyo maana tunanunua na kuuza. Sasa tumeamua kuifufua TFC tumeipa mtaji wa Bilioni Sita na tutaipa guarantee iende ikanunue mbolea kwenye soko la dunia ije hapa iweze kushindana na private companies. Kama tuta-subsidize lazima tuwe na mkono wetu ndiyo maana kwenye hotuba nimesema subsidy mechanism ya Wizara ya Kilimo safari hii tutawapa priority wazalishaji wa ndani and we will do this. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna siku zote hofu watu wataiba, halafu kuna dhana moja hatari sana, kuwaita wafanyabiashara wezi. Kwani hakuna Civil Servants wezi nchi hii? Big scandals zilizofanywa humu ndani hazijahusisha Civil Servants? Why we call our private sector everyday wezi kwenye nchi hii? Mtu wa sekta binafsi haibi peke yake lazima awe na mtu wa Serikali waibe nae. Kwa hiyo, mimi nataka niiambie private sector iliyoko kwenye kilimo, I will protect you kama ninavyom-protect mkulima wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna majadiliano hapa yamesemwa kuhusu ushirika, nataka niwaambie na nimwambie Ndugu yangu Mheshimiwa Sanga, mazao yote yanayopitia mfumo wa ushirika hayana lumbesa. Ili kumlinda mkulima, wakulima hawa wadogowadogo ni lazima tuujenge ushirika. Wanaushirika wapo wanaoiba lakini hatutaufuta ushirika kwa sababu kuna wezi, tutashughulika na wezi wakati tunaendelea kuujenga ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo success stories za ushirika, zipo. Ushirika ulikufa because the country decided kwenda kwenye role approach ya privatization, ndiyo ukweli huo na mimi hiyo ndiyo naamini. Leo tumefufua ginneries, tunafanya Chato, they are making profit, tunayo Mbogwe ya Mheshimiwa Maganga mwaka huu imepata profit na tumeifufua mwaka jana. Nikuhakikishie tunawapa 13 Bilioni ya kwenda kununua pamba. Tumefufua CACU, tunaenda kufufua SHIRECU Sola, tunaenda kufufua Nyanza, tunaenda kufufua Manawa, tunaenda kufufua Sola, tunaenda kufufua Lugulu, tunaenda kufufua ginnery ya Sengerema kwa Mheshimiwa Tabasamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme hivi, tutazifufua. Tuliziua kwa sababu tuliogopa kukabiliana na changamoto, tutakabiliana nazo, tutazifufua without any problem na huo ndiyo mwelekeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya Tanzania Agricultural Development Bank. Kisera TADB is a development bank siyo commercial bank. Kazi ya TADB ni ku-de-risk sekta ya kilimo na ku-invest kwenye miradi ya muda mrefu, ndiyo kazi yao. Bahati mbaya kwa sababu ya sera zetu na mifumo yetu ya ukopeshaji ambayo tunayo katika uchumi wetu, ambayo tume-copy na ku-paste huko kwingine tumeileta hapa ambayo hai-acknowledge rural economies ndiyo maana tunampeleka TADB kwenda kumkopesha mkulima ili akapande nyanya auze kesho, badala ya kumpeleka kwenye development projects. TADB anafanya hiyo kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekusikia Dada yangu Mheshimiwa Jacqueline, nimewasikia Wabunge wote wanaotaka wamuone TADB karibu, tutakaa na commercial banks zote ambazo zimesaini makubaliano na Tanzania Agricultural Development Bank ziwe na madirisha ya TADB kwa ajili ya kutoa guarantees kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, benki zote ambazo zina asili ya Kitanzania zimeanza kuelewa sekta ya kilimo, zipo benki NMB, CRDB na mimi wala sioni aibu kuzitaja, TADB, Equity, benki hizi zimeanza kutoa fedha kwa ajili ya kilimo, zimeanza, Wizara tutazisaidia na kuzi-support. Benki yoyote, nilisema mbele ya Rais, nasema mbele ya Bunge, benki yoyote ambayo haitakwenda kutoa mikopo ya kilimo kwa single digit kama tulivyokubaliana haitafanya biashara na Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, misimu inakuja, unakuja msimu wa korosho wa turn over ya zaidi ya Bilioni 500, wanunuzi wote tutawapeleka kwenye benki zinazofanya biashara na sekta ya kilimo. Unakuja msimu wa pamba, unakuja msimu wa kahawa, unakuja msimu wa chai, unakuja msimu wa kakao, nataka niziambie commercial banks, they must play our music. Kwa muda mrefu turn over zao zinabebwa na kilimo, lakini kinachoenda kwenye kilimo hakionekani, tutafanya nao biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu kuwaambia commercial banks pelekeni fedha kwenye ushirika wa korosho. Wakopesheni AMCOS, tumeshakubaliana mimi na ninyi na mmetaka barua kwangu nimewaandikia, sasa ambae hatopeleka tutakaa naye mezani. Ninasema categorically tunaenda kwenye msimu atakaye-enjoy fedha ya msimu wa korosho ni yule aliyeenda kwenye korosho kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo hoja hapa kwamba, kwanini tunaanzisha Benki ya Ushirika, nashauri tuende tukasome mifumo ya ukopeshaji na ya uendeshaji wa Cooperative Society na Cooperative Society Financing Modals. Vyama vya Ushirika haviwezi kukopesheka katika mifumo hii ya commercial approach tuliyonayo kwenye mabenki, ndiyo maana duniani kote watu walioendelea wanazo benki za cooperatives. Niwahakikishie benki ya ushirika haitaenda kuchukua hela ya umma. Tumefanya modal Benki ya Kilimanjaro. Tumeingia benki wameweka mkono wao, wameweka management, tumeanza kupata faida. Tunai-reform Benki ya Tandahimba, tunazi-merge benki hizi mbili tuna-form Cooperative Bank. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuwe na negotiating tool. Lazima taasisi za fedha zijue kwamba wakulima wa nchi hii wana benki yao wasiposikilizwa there is somewhere they can go. TADB ni mali ya Serikali, tuiache TADB ifanye kazi yake ya msingi ya ku-invest kwenye long term project, tuziache commercial banks na cooperative bank zitaenda kwenye short term, hii cooperative bank tunashirikiana na commercial bank kuianzisha. Kama zilikufa benki nyingine, zilikufa because tuliamua kuziua kwa kufanya political decisions kwenye mifumo ya ukopeshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda kuanzisha insurance ya wakulima, inakuwa total package. Tumeanza kazi na TIRA na inakuwaje, kwenye production, kwenye storage na kwenye market, mkulima anapata risk kote, tumeamua. Kwa nini tunaenda kwenye eneo hili? Tunaenda ili kumlinda mkulima na siku ya mwisho aweze kukopesheka kirahisi. Tunashirikiana na Wizara ya Fedha, tunashirikiana na TIRA na tutaanzisha na ku-launch scheme ya insurance ya wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mafuta ya kula. Siku zote toka nimeingia Bungeni tumekuwa tukijisifia mchikichi ulianzia Tanzania, nataka niseme hivi kama tutaendelea na modal tunayoendelea nayo sasa hivi ya mchikichi tusahau kuwa na utoshelevu wa mafuta, tusahau! Hauwezi kuzalisha miche, unai-breed halafu unampelekea Hussein anaenda kupanda kwenye robo eka. Ninamuomba Mbunge wa Kalenga usiwagawie wakulima eka moja-moja kilimo siyo kugawana umasikini, that is wrong approach. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachukua hatua gani kwenye mchikichi? Hatua ya kwanza tunayoichukua kama Serikali, tumejiwekea lengo la kuzalisha metric tons Laki Tano ya mafuta ya mchikichi. The first approach tunayotaka tunahitaji hekta 154,000. Nimemuandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Pwani, nimemuandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Tabora, nimemuandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, nimemuandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Katavi, tunaenda kuchukua maeneo makubwa kama yatahitaji fidia Serikali italipa fidia. Tunaenda ku-clean, kuyasafisha, tunagawa blocks kubwa kubwa na kuwagawia wakulima tumewakabidhi eneo, kama ni eka 20 unampa eka 20, umempandia, mnasimama. Then automatically kitakachotokea processors ndiyo watakuja pale wataanza ku-process. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii wanayofanya Kaka yangu Mheshimiwa Kirumbe kule Kigoma ni kutengeneza michikichi nusu eka, wanaichemsha kwenye pipa na mti, haiwezi kutuondoa, ndiyo ukweli. Tumeamua kuchukua modal ya ku-subsidize kwenye alizeti na ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tunaenda kuanzisha Tanzania Agricultural Growth Corridors, lazima tufanye hivi. Wazee wetu hawa akina Mheshimiwa Mkuchika na wenzake hawakuwa wajinga kutoa muongozo wa TANU wa maeneo ya kilimo. Leo unalima korosho kutoka kule kwa kina Mheshimiwa Katani unaipeleka mpaka Ngara. Economically does not pay, logically it has no sound. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie inawezekana ikawa unpopular decision, lakini lazima tuwe na growth corridors za kilimo katika nchi hii, lazima na ndiyo mwelekeo tunaoenda nao kama Wizara. Ninaliomba hili Bunge yeyote atakayekuja Wizara ya Kilimo mumhoji juu ya Agricultural Growth Corridor, lazima! tusipofanya hivi hatuitendei haki hii nchi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunagawa mbegu za alizeti, tuna-subsidize, it is a painful decision na Serikali itaweka Bilioni 11. Nitumie Bunge hili kuwambia Mkurugenzi wa ASA, Dada yangu Sofia mmoja wa Civil Servant wanaofanya kazi nzuri sana katika nchi hii, tulivyoamua kugawa tani 2,000 hakulala yule Dada. Ninawaomba Wakurugenzi wa Halmashauri, targets za kukusanya mapato mtazipata kwenye kilimo, m-support kilimo, tutazalisha, tutagawa tani 5,000 msimu unaokuja kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na tutagawa certified seeds, msimu uliopita tuligawa standard seeds, safari hii tunaenda kugawa certified seeds kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusipogawa mbegu na kuwapa ruzuku wakulima wa nchi hii, Marekani anatoa ruzuku, European Union wanatoa ruzuku, sisi ni akina nani kudhani kwamba eti mkulima atajinunulia kila kitu? We should not be misled. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliongea sana kuhusu suala la mbegu na ninataka niseme kwamba mwelekeo wa Serikali ni kufanya research and development, kuzalisha mbegu bora za kisasa, tuwe na mbegu zetu ambazo tunazalisha wenyewe. Tukijizalishia wenyewe hizi mbegu bora whether ni hybrid au ni OPV na kwa kuwa tunataka growth rate ya 10 percent by 2030 haya tunayoyaanza leo matokeo yake siyo ya kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo watu waliwekeza huko nyuma, leo tuna-enjoy sisi. Let us sacrifice now. Tujitoe, tuwekeze kwenye uzalishaji wa mbegu, tujitosheleze. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mazao 13 ambayo ni mahindi, mpunga, mtama, alizeti, soya, ufuta na maharage; mazao haya tukiwekeza kwa muda mrefu kwa kipindi cha miaka mitatu tu kwenye eneo la mbegu nchi hii itajitosheleza. Tutakuwa na mbegu zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena kuiambia sekta binafsi ya Tanzania, iache tabia ya kuwa traders, wawe investors. Njooni tutawapa maeneo, tutawapa mikataba ya muda mrefu mzalishe mbegu, tutazinunua sisi, tutawapa wakulima wa nchi hii kwa ruzuku. This is the best model, kote duniani wamefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ameniambia ndugu yangu Mheshimiwa Katani kwamba nawapendelea watu wa tumbaku kwa sababu natoka Tabora kwenye tumbaku. Kwanza sikani, natoka Tabora. Pili,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja. Ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niseme hivi, wakulima wanasajiliwa wote wala msiwe na hofu. Kupitia Bunge lako nimwambie Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, usipoanza kusajili wakulima, kuanzia mwaka huu tunaanza kugawa pembejeo, mimi na wewe hatutaelewana. Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba ni lazima usajili wakulima. Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa ni lazima usajili wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Katani anasema tumewapendelea watu wa tumbaku; niseme, kwa mwaka huu mmoja…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bashe toa hoja. Ahsante kwa michango mizuri na majibu mazuri.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie. Karatasi ya hela imepotea nini? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.