Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuweza kuchangia katika Wizara yetu hii muhimu ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwa kuanza na mimi ningependa vilevile kumshukuru sana Mwenyeezi Mungu Sub-hanallah Wataallah kwa kutujaalia uhai uzima na salama lakini halikadhalika kumshukuru Jemedari Mkuu au Amiri Jeshi Mkuu wetu, Mama Samia kwa jitihadi ambazo amekuwa akizichukua katika kuliendeleza Taifa hili. Mheshimiwa Rais ametuletea jembe Waziri wetu ambaye kwa kweli anatusaidia sana katika kuiendeleza Wizara hii na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri muda mfupi lakini ameweza kufanya makubwa katika Wizara hii pamoja na timu yake, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja katika mchango wangu mimi nikiwa kama Balozi wa Mazingira na nimpongeze sana Mheshimiwa Jafo kwa kunipa nafasi hii, ili niende kuitendea haki ningekwenda moja kwa moja kwenye mchango wangu katika page 13 ambayo inaelezea utunzaji wa mazingira katika speech yake Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri umepanda miti 147,000 katika makambi yetu kwa kweli hiki kiwango kidogo tukizingatia mahitaji ya nishati ya kupikia, miti ya kujengea katika makambi yetu. Kwa hiyo, ningeomba tu kwamba katika bajeti hii inayokuja tukaongeza kidogo kiwango cha upandaji miti katika makambi yetu kwa sababu miti 100,000 ni kidogo Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili Mheshimiwa Waziri kule Zanzibar kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika makambi yetu na zaidi kuna Kambi ya Ali Khamis Camp ambayo ilipanda miti mingi kipindi cha nyuma, lakini pia kuna kambi ya Mwanyanya ambayo ilipanda miti mingi kipindi cha nyuma lakini hivi sasa miti ile inavunwa lakini bila ya kurejeshewa miti mingine. (Makofi)

Kwa hiyo, ningeomba tu katika kipindi kinachokuja tukajikita zaidi katika upandaji miti katika makambi yale haya ile miti ambayo tunavuna basi tuirudishe tena. Lakini kuna Kambi ya Makuwe na Bububu kuna uharibifu mkubwa wa mazingira Mheshimiwa Waziri, ningeliomba pia ukaweka jicho lako kule kwa sababu Idara ya Misitu na Maliasili kwa miti isiyorudishwa wamekuwa wakigombana mara kwa mara na kambi hizi kwa ukataji miji hovyo. Kwa hiyo, ningelipenda tu pia tukawaelimisha kambi zetu kwamba wakachukua jitihada za kutunza mazingira kama ulivyoahidi katika hotuba yako hapa kwamba miti hii ya asili inalindwa na kutunzwa. Kwa hiyo, nafikiri kambi hizi kwa sababu vilevile kuna miti ya asili basi tungeitunza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika Mheshimiwa Waziri katika suala la uwekezaji katika kambi zetu hizi za Zanzibar kumekuwa na uwekezaji ambao siyo sahihi, kwa sababu mfano kama kuna msitu mdogo katika Kambi ya Bavuai, ulikuwepo msitu ambao ni mzuri na umetunzwa kipindi kirefu, lakini hivi karibuni tumeanza kuumega, tumejenga vituo vya mafuta (shell) pale na tukitoka Kiembesamaki, Uwanja wa Ndege mpaka Mwanakwerekwe kuna karibu vituo vya mafuta (shell) saba. Sasa sijui kama kulikuwa na umuhimu wa kuwa vituo vya mafuta (shell) nyingine pale.

Kwa hiyo, mimi ushauri wangu tu Mheshimiwa Waziri tunapowekeza katika Kambi zetu hizi tuangalie uhalisia na tuangalie vilevile ramani za Manispaa na Miji yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini halikadhalika, tukiangalia katika Kambi ya Mtoni kuna vi-garage pale vya ajabu ajabu, sasa sijui kama kulikuwa na umuhimu wa zile garage pale kwa sababu zinaharibu haiba ya Mji; tunataka vikosi vyetu viwekeze kiuchumi, lakini vilevile tufanye tathmini ya kuangalia huu uwekezaji kama una tija. Lakini halikadhalika kuwema mazingira ya mji kwa sababu katika Mji wa Zanzibar kuna Kambi karibu tano na Kambi zote hizi zipo ndani ya mji. Sasa kama tutakuwa tunawekeza katika lengo siyo zuri tunaweza tukaaribu mazingira. Lakini pia kuna Kambi ya Welezo, ndani kule wamechimbisha mchanga ni mashimo matupu. Kwa hiyo, pia ningelikuomba Mheshimiwa Waziri ikiwekana ungefanya ziara ukaenda Zanzibar...

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Soud kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Asya.

T A A R I F A

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, naomba ni mpe taarifa mchangiaji siyo tu kwamba kuna uharibifu wa kimazingira kwenye kambi, lakini kuna wananchi wanaishi pembezoni mwa kambi, yaani Kambi ya Jeshi kwa mfano kambi anayozungumza Mheshimiwa Soud ya Mtoni watu wanaishi hapa ndani ya Kambi. Kwa hiyo, ni hatari zaidi hata mabomu muda mwingine yanaporipuka madhara huwa yanatokea kwa wananchi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Soud unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, naipokea hiyo taarifa. Naomba niendelee haraka haraka muda wangu nafikiri utakuwa umenichungia kidogo.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kuna Kambi ya Welezo kuna Mheshimiwa mmoja pale alijenga jengo na akaambiwa kwamba lile jengo litakuwa sio salama na ikabidi afidiwe aondoke. Sasa utashangaa sasa hivi yeye ameondoka, lakini sasa hivi pana maduka ya miti, pana maduka ya garage, yameanzishwa pale sasa utashangaa kama je, ilikuwa ni usalama ndio tukamuondosha yule. Sasa je, huu uwekezaji tunaouweka sasa hivi nao ni sahihi? (Makofi)

Kwa hiyo, ningemuomba tu Mheshimiwa Waziri ukafanya ziara ukaenda Zanzibar na ikiwezekana ikikupendeza, ukafuatana na Mkurugenzi wa Mazingira, Mkurugenzi wa AZEMA…

SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa, muda umekwisha.

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, na Mkurugenzi wa Misitu ili waweze kushauri. Ahsante sana. (Makofi)