Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti iliyokuwa mbele yetu.

Awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama mbele ya Bunge lako tukufu, lakini naomba uniruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliwahi kuuliza swali hapa Bungeni kuhusiana na mgogoro uliopo Kijiji cha Tondoroni, Kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani na majibu ya Mheshimiwa Waziri yalikuwa kama ifuatavyo kwamba; “tayari imeshaundwa task force kwa ajili ya kupitia migogoro yote iliyopo baina ya wananchi pamoja na Jeshi letu la Wananchi.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hivyo ndivyo nitapenda kujua sasa status ikoje ya mgogoro unaoendelea wa Kijiji cha Tondoroni, Kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani na Jeshi letu task force inasemaje? Nini hatma ya wananchi wa eneo hilo la Tondoroni? Mara ya mwisho katika eneo lile Serikali ililipa fidia lakini kile kilicholipwa kilikuwa kiduchu (kidogo), wananchi wakagoma kuondoka kwa ajili ya kupata nyongeza ama mapunjo ya madai yao. Lakini kilichofuata ni kwamba nyongeza hawakupewa na wananchi hawakuruhusiwa kuyaendeleza yale maeneo. Walipolima, walipojenga Jeshi lilikuwa linaingia usiku linabomoa na asubuhi linazua taharuki kubwa kuharibu mali za watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitapenda sana kupata majibu Mheshimiwa Waziri ukija ku-wind up ni nini majibu ya hiyo task force kuhusiana na wananchi wale?

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili na wa mwisho ni kuhusiana na suala hilo hilo la migogoro kati ya wananchi pamoja na Jeshi letu la Wananchi. Kwa sasa tunaangazia eneo la Kata ya Kazimzumbwi, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wetu wa Pwani. Kuna mgogoro mkubwa unaoendelea kati ya wananchi wa Kata ya Kazimzumbwi pamoja na Jeshi Kikosi Na. 191KJ Kisarawe. Hali sio shwari kiasi kwamba kuna malalamiko na masikitiko ambayo tayari yameshawasilishwa katika Ofisi ya CCM Wilaya, juu ya wananchi kupigwa, kuvunjiwa mali zao, nyumba zao pamoja na mashamba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa katika eneo lile la Kazimzumbwi Jeshi lilikuja likaomba nafasi ama likaomba eneo tukaweza kuwapatia eneo, lakini baadaye walirudi wakaomba waongezewe eneo la ukubwa wa mita 200. Serikali ya Kijiji iliwajibu kwamba hakuna hilo eneo, lakini Jeshi lilikaa kimya kwa muda na baadaye likafika likaanza kupiga watu, likaanza kudhuru watu na hatimaye wakatwaa hilo eneo la mita 200 na wakaongeza mita nyingine 300 kufika mita 500. Ni kwa nini Jeshi linatumia nguvu kubwa hivi, hivi imekosekana njia ya namna ya kutumika ili kama hilo eneo linahitajika kwa sababu za kiusalama na bado wananchi wakaendelea kupata haki zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hii migogoro ni ya tangu na tangu tangu enzi ya Mkuu wa Mkoa akiwa Mwantumu Mahiza mpaka sasa RC wetu ni RC Kunenge bado majibu hayajapatikana. Watu hawa wanapata shida sana.

Mheshimiwa Spika, nimeonelea nizungumzie hoja hizi mbili za maeneo haya mawili kwa sababu haya ni maeneo yao kutoka kwa mababu zao. Kama Serikali mnataka lipeni fidi kwa wananchi, mnawaweka wananchi wetu katika hali tatatishi.

Kwa hiyo, nitakuomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujibu nipate majibu ya kina ya hoja na haja wana Kisarawe wanataka kusikia juu ya hatma yao na haki yao ya ardhi yao ya maeneo mawili niliyoyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)