Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pamoja na uchache wa muda, naomba nizungumze mambo machache yafuatayo; kwanza naomba kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu, lakini naomba nimshukuru pia kwa kututeulia kiongozi mzuri wa Wizara hii ambaye sisi kama Kamati ya Ulinzi tunafanya naye kazi kwa karibu na kwa kweli, amekuwa mtendaji wa karibu sana kwetu sisi kama Wanakamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba nilishukuru jeshi letu likiongozwa na afande CDF, lakini pia likisaidiwa na wenzetu wa Jeshi la Kujenga Taifa, niwashukuru sana. Naomba nitoe shukrani kwa sababu kwanza nchi yetu imetulia, nchi yetu inafanya kazi kwa amani, imejenga mahusiano mazuri pamoja na majirani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu ya muda naomba kuzungumza mambo matatu yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza; wenzangu wamezungumza maneno mengi sana ambayo ni muhimu na kwa kweli inasaidia kulijenga jeshi letu hili, lakini na kuweka usalama wa nchi yetu pamoja na mipaka yake. Ningeomba la kwanza, tusaidie kwanza kuipitisha bajeti hii, lakini kama itawezekana tuone namna ambavyo tunaweza kuiongezea bajeti kwa sababu jeshi ni utafiti, jeshi ni vifaa na jeshi ni nyenzo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuwa na jeshi ambalo tunaliminya minya tunataka lifanye kazi yetu ya kutulinda halafu bajeti yake tumeifinya. Tunamshukuru mama yetu kwa kuongeza bajeti, lakini bado jeshi letu linahitajika liwe na bajeti ya kutosha ili liweze kufanya kazi zetu kwa sababu jeshi kazi yake ni moja tu, ni kulinda mipaka ya Taifa letu kuhakikisha kwamba, sisi tunaishi vizuri, lakini tunalinda Taifa letu bila migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili; wakati wa amani jeshi letu linatumika kuzalisha mali. Nawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge, Jeshi hili limeonesha uimara na weledi mkubwa katika kutekeleza mambo yake. Amesema dada yangu pale, tumekwenda kutembelea Makao Makuu ya Ulinzi, chombo hiki kimetengeneza au kinajenga Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa letu ambayo kwa kweli haijapata kutokea, lakini inatengeneza kwa gharama ndogo kabisa. (Makofi)

Kwa hiyo, maana yake jeshi letu kwa kutumia wenzetu pia wa Jeshi la Kujenga Taifa wanatumia gharama ndogo. Nawaombeni sana tutawawezeshe na iwe ndio priority yetu sisi kama Bunge kuhakikisha kwamba tunatumia gharama ndogo lakini kwa utaalamu wetu wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano hapa, juzi Mheshimiwa Waziri Mkuu alitangaza kuondoa wenzetu wanaoishi kwenye mbuga zetu kule. Mimi nilitegemea kwamba priority tungewapa wenzetu wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa sababu gharama ni ndogo, lakini utaalamu ni mkubwa. Sina hakika, lakini nina wasiwasi tumewatumia wenzetu wale wa JKT kama ndio ni substitution, hatukuwapa priority. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana tuwaamini wenzetu wa Jeshi la Kujenga Taifa, lakini tuamine kwamba, uwezo wao ni mkubwa. Tusiwafanye kwamba hawa ni second class wajenzi, hapana, tuwatumie, tuwape kipaumbele. Ninaamini watafanya kazi kubwa, ninaamini watafanya kazi kwa kuzingatia uzalendo wa hali ya juu kwa hiyo, ningeomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho kuliko yote nilizungumza juzi hapa kwamba, namna tunavyowaajiri vijana wetu kwenye jeshi vigezo vinatumika vingi. (Makofi)

Naomba nirudie tena leo kwamba kigezo pamoja na elimu, kigezo cha kwamba, vijana wetu wanaopitia Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Kujenga Uchumi kwamba ndio kigezo kikubwa naomba sana hii iwe ni addition kwa sababu sisi kama jeshi hatuna uwezo wa kuwachukua vijana wote waliomaliza kidato cha pili, cha nne na cha sita kuingia ili wakapate mafunzo haya ya msingi. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba sana tusiwanyime vijana wetu wengine ambao wanao uwezo wa kuingia katika vyombo vyetu hivi, simply kwa sababu, hawakupata nafasi ya kupita kwenye majeshi haya, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)