Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Ali Juma Mohamed

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shaurimoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuweza kunijalia kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwa dhati kabisa nilikuwa napenda sana nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuweza kuwasilisha vizuri hotuba yake ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana kwa Taifa letu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile napenda nimpongeze Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Mabeyo, kwa kazi nzuri anayoifanya kupitia Jeshi letu hili, Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania. Vilevile napenda nimpongeze kwa dhati Mnadhimu Mkuu wa Jeshi naye kwa kuendelea kufanya kazi nzuri kwa ajili ya Taifa letu na jeshi letu hili la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda vilevile kumpongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kaka yangu Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, amekuwa ni kiongiozi mwadilifu na anayetoa miongozo mizuri katika Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kwa ajili ya kulipongeza zaidi jeshi letu, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Katika kipindi kirefu katika nchi yetu wananchi wengi walikuwa wanachukua dhana ya kuwa jeshi letu kazi yake ni kulinda nchi pamoja na mipaka yake, lakini hivi sasa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limejikita zaidi katika kuinua na kuimarisha uchumi wa Taifa letu na katika haya tumeona, Kamati tumetembelea mambo mengi na kiukweli tumeridhika na namna Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wanavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jeshi letu sasa limekuwa lina taswira nzuri katika jamii yetu hasa katika mambo yale ya ujenzi majengo tofauti tofauti katika nchi yetu. Tumejionea majengo makubwa likiwemo la Ikulu ya Chamwino, Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa na Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji; haya ni majengo makubwa yamejengwa na wanajeshi wetu wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi sasa katika nchi yetu ukitaka kuona majengo makubwa na mazuri, basi uangalie majengo ambayo yamejengwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitaka kupata huduma nzuri za afya, basi angalia Jeshi la Wananchi wa Tanzania; ukitaka kuona mashamba mazuri ya kilimo pamoja na ufugaji wa samaki na mifugo mingine, basi liangalie Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania; ukitaka kuona elimu, shule ambazo zinasomesha vizuri, basi ni shule ambazo zinamilikiwa na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania; ukitaka kuona wanamichezo wazuri, basi vilevile uangalie Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania; na hata ukitaka kuona burudani na mambo mengine mazuri, basi pia uangalie Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile jeshi letu limeikuza nchi yetu…

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Ali kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Msambatavangu.

T A A R I F A

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ukitaka pia kuona afya nzuri ya akili liangalie jeshi letu, ahsante. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Taarifa hiyo.

MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, nimeipokea Taarifa ya dada yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jeshi letu vilevile limeipaisha vizuri nchi yetu ya Tanzania kwenye kada ya diplomasia ya nje. Jeshi letu mara kwa mara limekuwa likishiriki katika mission mbalimbali za kimataifa na hii imeipa taswira nzuri nchi yetu ya Tanzania ya kuonekana ni nchi ambayo inajitolea kwa ajili ya mataifa mengine duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya yote ambayo nimeyazungumza yamekuja kutokana na usimamizi mkuu wa Amiri Jeshi Mkuu kwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, mama yetu Samia Suluhu Hassan. Yeye ndiye ambaye anatoa miongozo mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kumalizia katika nchi yetu kuna scheme nyingi za umwagiliaji ambazo zimetelekezwa. Kwa vile jeshi letu linafanya kazi vizuri, hasa kupitia SUMA-JKT, nilikuwa naomba hizi scheme zote za umwagiliaji ambazo zimetelekezwa basi wapatiwe JKT ili waweze kuziendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, naunga mkono hoja. (Makofi)