Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tarehe 13 Mei, 2022 niliuliza swali hapa Bungeni juu ya Makampuni ya simu kukata muda wa maongezi wa watanzania ambao haujatumika kwa maana kwamba bundle lime-expire. Na Waziri wakati ananijibu alisema kwamba wameelekeza Makampuni ya simu mtu kama bundle lake lime-expire basi akinunua bundle lingine ule muda uliyopita arudishiwe. Hiyo ninahesabu kama ni dhulma kwa watanzania kama ndivyo wanavyofanya basi Mheshimiwa Waziri haujatenda haki kwa watanzania.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jackson Kiswaga, taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka niweke sawa jambo hili kwamba ukizungumzia bundle linakuwa limited kama ni siku 30 kama ni siku 15. Lakini nafurahia Waziri alisema kwamba kama ukiongeza linavyokaribia kwisha unaongezea muda wa mazungumzo. Kwa hiyo ndiyo business model yaani ndiyo biashara iko namna hiyo. Ahsante sana.

MWENYEKITI: Kwa hiyo ndiyo taarifa. Mheshimiwa Salome unapokea taarifa?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei na namshauri Mheshimiwa Mbunge atulie, asubiri nifafanue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kasema clear hapa kwamba watanzania asilimia 95 wana-access ya mtandao kwa maana ya kwamba wana-access ya minara ya simu. Kwa hiyo, wanaweza kutumia simu, kwa maana hiyo wanaweza kujiunga kwenye vifurushi vya kupiga simu. Na amesema asilimia 68 ya watanzania wanauwezo wa kujiunga kwenye vifurishi vya internet yaani wanaweza kupata access ya internet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, ukijiunga kwenye kifurushi cha internet au bundle lile bundle unatakiwa ulitumie ndani ya siku moja. Ikitokea kwa namna yoyote ambazo mara nyingi mtu anashindwa kutumia bundle lile kwa sababu ya kukosa mtandao kwa sababu maeneo mengi bado hayana access ya mtandao au anashindwa kutumia bundle lile kwa sababu ya changamoto za kampuni za simu. Kwa sababu hizo sasa yule mtu ambaye bundle lake lime-expire hawezi kurudishiwa hiyo pesa ambayo ime-expire. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa mantiki hiyo, kama mtu yule analazimishwa ili arudishiwe ile pesa yake ambayo ime-expire ni lazima ajiunge dakika chache kabla yaku-expire kwa bundle lile au muda wake wa maongezi kama analazimishwa kufanya hivyo ni kumlazimisha mtu kufanya matumizi ambayo hakuyapanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni ya simu yakifanikiwa kukata shilingi 200 tu kwa watanzania Milioni 50 ambao Mheshimiwa Waziri amesema, wakifanikiwa kukata shilingi 200 tu kwa siku kwa maana ya kwamba bando lime-expire au kifurushi cha muda wa maongezi kime-expire kwa siku moja wanauwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 10. Kwa mwezi wanakusanya zaidi ya bilioni 300. Mheshimiwa Waziri hapa ameomba hapa hela anayoomba kwa ajili ya Wizara yake, ameomba shilingi bilioni 282. Kwa hiyo, pesa hiyo wanaweza kukusanyia ndani ya mwezi mmoja tu wakakupatia na ukafanya kazi za Wizara yako zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe makini sana. Bilioni 300 za watanzania zinaweza kupotea ndani ya mwezi mmoja kwa sababu ya bundle lime-expire au muda wa maongezi umeisha muda wake na wakati siyo kosa la watanzania kushindwa kutumia muda wa maongezi. Kusema kwamba hiyo ni biashara, biashara ni nguvu ya negotiation na kazi kubwa ya Wizara ni kuwalinda watanzania wasiibiwe na makampuni ya simu. Na Mheshimiwa Mbunge ananipa taarifa, kwa taarifa yake na mimi nimpe taarifa, hiyo biashara ya bundle ku-expire huko duniani ilishapitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea hakuna biashara ya bundle ku-expire. Nchi zinazoendelea hakuna biashara ya bundle ku-expire. Kwa nini Tanzania tunaruhusu makampuni ya simu yaibe pesa za watanzania kwa sababu bundle lime-expire? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Bashe kwenye Wizara ya Kilimo wakati anaomba hela, ameomba bilioni 750. Hiyo pesa makampuni ya simu yanakusanya ndani ya miezi mitatu tu. Miezi mitatu tu wanakusanya, sisi tunatafuta mwaka mzima wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Wizara tunayo sheria ya kulinda mlaji (Consumer Protection Act) na kazi ya Sheria ile ni kumlinda mtanzania asiibiwe ambaye anatumia bidhaa hii ya simu na mtandao. Mheshimiwa Waziri anatakiwa kuacha legacy kwenye hili na ataacha legacy kama atahakikisha kwamba anawalinda watanzania waweze kutumia pesa yao ambayo wamenunua bundle au wamenunua muda wa maongezi bila bundle lile kuharibika. Na ukisema bundle lime-expire umeshusha thamani ya pesa ya Tanzania. Kwa sababu kama pesa yangu mimi shilingi 2,000…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: ...iko mfukoni haijaexpire, ina-expire vipi pesa ambayo iko kwenye simu? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)