Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, niseme wazi mimi ni Mwandishi wa Habari na nitawasemea wanahabari, changamoto zao nazijua na nimeziishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na kwa kurudi kwako kaka yangu kuna nafuu, watu wamepata hope waandishi wenzangu. Na kwa kauli ya Mheshimiwa Rais imetoa hope kwa ile kuonesha dhamira. Tunahitaji dhamira Mheshimiwa Waziri yako na Mheshimiwa dhamira ya Rais sasa ije kwenye vitendo kwa kuleta mabadiliko ya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wewe unajua mbali ya kwamba kuna unafuu lakini bado kwenye maeneo mengine waandishi wanatishwa. Bado waandishi hawafanyi kazi kwa uhuru. Mheshimiwa Waziri unajua, leo hakuna investigation story si kwenye print media wala kwenye electronic media. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hizi Makala ambazo zinaandikwa ni za kawaida. Sheria hii ililetwa kutakuwa na mijadala ya kujenga, ya kukosoa Taifa letu lakini ya kujenga. Tunataka turudi enzi hizo, tunataka tuone Makala za uchunguzi, tunataka tuone vipindi mbalimbali kwenye Redio na Televisheni ambavyo wachambuzi watakuwa huru kwa maslahi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hayo yote Mheshimiwa Waziri hayawezi kutokea kama hakutakuwa na Sheria bora ya kuwafanya waandishi wa habari kwenye print media kwenye electronic media wanafanya kazi kwa uhuru. Na kufanya kazi kwa uhuru kukiwa na uwazi ndiyo Taifa letu linasonga. Lakini kwa dhamira tu, leo anaweza akamaliza Mama Samia muda wake ana dhamira njema, wewe una dhamira yako ukatoka lakini akaja wengine ambao hawana dhamira njema bado tukarudi kule kule kwa waandishi kuteswa, kwa waandishi kupigwa, kwa waandishi kunyanyaswa, kwa waandishi kunyimwa habari kwa maslahi ya watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Mheshimiwa Waziri, najua umeanza kukutana na wadau wa habari ni jambo jema. Lakini nilikuwa naomba zile Sheria zenye ukakasi Serikali ndiyo mzichukue, mzibadilishe kwa sababu ndiyo zinawanyima fursa waandishi wa habari. Kwa mfano Mheshimiwa Waziri wewe unajua, natolea tuu mfano kwenye Sheria ya Huduma ya Habari Kifungu cha 19(20)(21) ambacho chenyewe kinazungumzia kinawatambua watu gani ni waandishi wa habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tasnia yetu pia tunawahitaji Wanasheria, kuna watu wataandika habari zinazohusu Sheria. Tunawahitaji Madaktari ambao wataandika habari za afya. Tunawahitaji Wachumi ambao watafanya analysis ya masuala ya kiuchumi. Lakini kwa sheria hii inataka mtu mwenye degree ya Sheria ya udaktari akija aanze tena degree ya habari, hapana. Sisi kwetu tuna taratibu zetu, kwa mfano mimi wakati nipo uhuru pale tulikuwa tunasoma media law and ethics kwa sababu gani? Tunajua lazima waandishi wa habari wapate training mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hawa wakiwepo Wanasheria wamekuja kutaka kufanya kazi ya habari watapewa mafunzo ya miiko, maadili namna gani ya kuandika habari lakini bado wana taaluma zao. Sasa hayo Mheshimiwa Waziri ni mambo ya muhimu sana na leo kwa mfano kuna kina Jenerali Ulimwengu ni Mwanasheria lakini ni Mwandishi nguli. Tuna Kibanda ni Mwalimu by profession lakini ni waandishi wazuri. Kwa hiyo, na sisi tunawahitaji watu wa namna hiyo kuja kufanya uchambuzi wa kina kwenye tasnia yetu. Lakini watapewa miongozo inayohusu habari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano pia, Mheshimiwa Waziri wewe unajua kuna Kifungu cha 5(e)(8)(9) kinazungumzia masuala ya leseni. Hiki kifungu kinatoa mwanya kwa Mawaziri wenye nia mbaya kufungia vyombo vya habari. Hiki kifungu ni kifungu kibaya kuliko vifungu vyote, tunaomba vifanyiwe kazi. Gazeti linatakiwa lisajiliwe tu, sasa kila mwaka leseni, kila mwaka leseni mtu ana kampuni hiki kifungu kibaya kinatengeneza mazingira ya kufungia vyombo vya habari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mzigo mzito kapewa Mnyamwezi wakati hii Sheria mbovu inatungwa ulikuwepo wewe na umeiona na imetestiwa imekuwa mbaya. Mzigo huu unao wewe mwenyewe wahakikishie kipindi kile kilikuwa kingine, hiki kingine, rekebisha hii Sheria sisi waandishi wa habari tunataka tuwe huru, tulikosoe Taifa letu kwa maslahi ya kujenga ili nchi yetu iende kama nchi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)