Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, kwa kazi nzuri anayoifanya na tunaona Wizara hii kupitia yeye imeendelea kufanya kazi nzuri sana. Kama ambavyo tumekuwa tukisema kwamba lazima Watanzania wapate taarifa mbalimbali, lakini kupitia Wizara hii Waziri ameweka utaratibu mzuri na tumpongeze sana kwamba tuliwahi kumwona siku moja kwenye Aridhio akiendesha kipindi cha karibu nusu saa. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri ndugu yangu Engineer Andrea Mathew Kundo kwa namna ambavyo anamsaidia Mheshimiwa Waziri; lakini na timu nzima Katibu Mkuu, pamoja na wasaidizi wao wote katika Wizara na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu ya muda nitakwenda kwenye mambo mawili tu. Nitaanza na jambo la kuhusiana na kuboresha mawasiliano nchini. Tunajua kabisa kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kubwa, Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kupeleka minara. Ukiangalia mwaka wa fedha uliopita minara mingi imewashwa na mingine inaendelea kufanya kazi. Nikiwa Mjumbe wa Kamati tumekuwa tukiona kazi kubwa inayofanywa na Wizara yetu. Naomba tupongeze sana kwa sababu ni jambo kubwa, kupitia UCSAF hawa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote umefanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo hayana mvuto wa kibiashara, makampuni mbalimbali yalikuwa hayaendi, lakini kupitia mfumo huu wa Serikali yetu na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa fedha za kwenda kusaidia ruzuku ya kuhakikisha inajenga minara katika maeneo mbalimbali ya nchini kwetu. Kwa sababu, mawasiliano ni haki ya kila mtu, leo hii kila mtu kule kijijini bibi, babu naye unakuta ana simu yake anataka awasiliane na mjukuu wake popote alipo. Hili jambo kubwa limefanyika, lazima tuipongeze Serikali kwa kazi kubwa, hata mwaka huu wa fedha tumeona kuna fedha imetengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru sana sisi watu wa Singida Mashariki tulikuwa na changamoto kubwa katika Bonde la Misughaa, tumepata mnara ambao ulishakuwa tayari. Sasa hivi tunamsubiri Mheshimiwa Waziri aje azindue rasmi ili wananchi waanze kupata mawasiliano. Kwenye hili wananchi wanaomba, Waziri aruhusu na kampuni nyingine za simu ziweze kuweka mawasiliano yao kwenye ule mnara ili waweze kupata na mawasiliano mengine; kwa sababu pale ni mnara wa TTCL na wanaomba na mawasiliano ya simu zingine ili waweze kuwa na mawasiliano mbalimbali, wengine wanataka Airtel, Vodacom na Tigo. Naamini kabisa Waziri akifanya hivyo itakuwa na maana kubwa ya uwekezaji wa Serikali pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili, pia niombe sana tuongezewe tena mnara, katika Kata ya Libwa mawasiliano ni mabaya sana, lakini pale Mang’onyi tunataka tupate mawasiliano kwa ajili ya Mgodi wa Shanta ambao unakwenda kuzinduliwa hivi karibuni, kutakuwa na mwingiliano wa watu wengi sana. Kwa hiyo, niombe sana watuangalie, tuweze kupata minara angalau mingine miwili katika Jimbo la Singida Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili naomba suala la data, tuongeze uwezo wa data kwa wananchi, inawezekana kukawa na mawasiliano ya simu, lakini data zipo chini, kwa hiyo wamezoea 2G lakini tukiende 3G, 4G, kama Mheshimiwa Waziri alivyokuwa anasema hapa, wananchi watakuwa na mawasiliano, kwa sababu leo, mawasiliano ni biashara, kila mtu anaweza kuwa anafanya biashara kupitia simu yake hata akiwa kijijini kule. Pia na hilo Mheshimiwa Waziri akilifanya itatusaidia sana kuongeza uwezo katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo ni jambo la mwisho, nataka niongelee kuhusu TBC. TBC ndiyo Shirika la Umma; Habari ya TBC kokote ikitoka ni ya uhakika kwa sababu imekuwa edited na Serikali. Baadhi ya vyombo vinafanya biashara, vinaangalia walaji wanataka nini, lakini TBC inajenga umoja wa Kitaifa, ulinzi wa usalama wa nchi, historia ya nchi yetu na mambo mbalimbali. Kwa hiyo, TBC ikiwa na uwezo mkubwa itakuwa inajenga umoja wa kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba TBC imefanya kazi kubwa toka uhuru, lakini leo hii tunaona namna ambavyo tunauhisha; vipindi mbalimbali vinawekwa, bidhaa mbalimbali zinawekwa kupitia TBC, lakini Mkurugenzi Ayubu anafanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo niombe sana wapewe fedha ya kutosha, uwekezaji wa kutosha, huko kwenye maeneo ya huko nje kwa maana ya kwenye mipaka ya nchi yetu, kuna baadhi ya watu ambao toka wamezaliwa hawajawahi kusikia TBC kwa maana ya Kiswahili, wanaongea lugha za nje, wengine wanasema hao ni Wanyarwanda mpaka kwenye uraia tunapata shida, kwa sababu toka wamezaliwa wanasikia Kinyarwanda tu. Leo hii ukiwawekea TBC kwa uhakika, maana yake watu wetu utawasaidia kujua Radio yao ya Taif ana Televisheni ya Taifa. Kwa hiyo, niombe TBC wapate fedha ya kutosha ili iweze kufanya kazi nzuri ambayo inaendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)