Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kupata nafasi ya kuweza kuchangia. Nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wataalam wote wa Wizara hii. Kutokana na ufinyu wa muda nijielekeze moja kwa moja upande wa mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa ya Waziri ambayo ameitoa hapa ameeleza kwamba kwenye huu mwaka wa fedha ambao tunaendelea nao kuna takribani Kata 85 ambazo zilikuwa zimepangwa kuweza kujengwa kwenye huu mwaka wa fedha. Kata hizi ni chache sana kulingana na ukubwa wa jiografia ya nchi hii na tukienda kwa mtindo huo maana yake, hatutoweza kuyafikia maeneo yote kwa kuweza kujengwa minara ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, minara hii inajengwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano wa UCSAF minara ambayo inajengwa kwa UCSAF minara mingi wamepewa TTCL na TTCL hawa wanakwenda kwa hali ya kusuasua, tukienda nao hivi tutafikia hatua ambayo hatutaweza kufikia lengo la kujenga hii minara na kuifikisha kwa wananchi kwa wakati. Kutokana na minara hii na TTCL kwenda katika maeneo ambayo kibiashara siyo rafiki sana ambayo Maopareta wengine wanaiogopa hii, sasa tunavyokwenda na TTCL maana yake hata ule ushindani na kukua kwao kuweza kupata faida inakwenda kuwa ni ngumu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na TTCL kwenda maeneo ambayo kibiashara hayana faida kwao ni kama wanatoa huduma matokeo yake TTCL wanakuwa hawafanyi vizuri sana sokoni. Nikiangalia kwenye takwimu ambazo tunazo, kwa watoa huduma saba ambao tuko nao, Telephone Operators TTCL ni wa pili kutoka mwisho. Kwenye market share wa kwanza anaongoza Vodacom ana asilimia 30.5, Airtel ana asilimia 27, tiGo 25.4, Halotel 13.3, Zantel asilimia Mbili na TTCL ana asilimia 1.7. Kwa hiyo, kuweza kushindana kwenye soko imekuwa ni gumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kushindana huku kunakuwa kugumu tuone namna ambavyo tunaweza kubadilisha Sheria kwa TTCL ambayo itaweza kuwabeba ili na wao waweze kufanya kazi yao vizuri. Ninashauri Serikali ili kuweza kuwasaidia TTCL tuweze kubadilisha Sheria zetu, TTCL wabakie kuwa ni wajenzi wa miundombinu peke yake, wasiingie kama Telephone Operators kuweza kushindana na haya makampuni mengine kwa sababu, kwenye ushindani tayari wameshaonesha kwamba hawawezi wameshindwa. Tukiweza kubadilisha sheria wao wakawa wanamiliki miundombinu minara hii wanapewa na minara mingine waendelee kuijenga, baada ya hapo hawa Telephone Operators wengine wawe wanapanga kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnara mmoja utaweza kupangwa na makampuni matatu mpaka manne, kwanza itasaidia minara kuwa michache, lakini mnara huo mmoja na makampuni mengine yakipanga hapo na huduma zote maana yake hazitaweza kupatikana vizuri na kwa wakati. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam, Mbunge wa Sengerema, taarifa.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa tu mchangiaji kwamba TTCL hata hiyo minara wameshauza.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, unaipokea taarifa?

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo. Tuseme tu TTCL wakiweza kumiliki hii minara lakini hata pia kwa usalama wa nchi itaweza kutusaidia sana, maana yake tutakuwa tuna uhakika na usalama na udhibiti mzuri ambao tuko nao. Tukienda hivi tuliona hapa miaka kama miwili iliyopita, wenzetu baadhi ya kampuni fulani tulishindwa kupata mawasiliano hapa, lakini tukiwa na uhakika wa TTCL kuweza kumiliki hii hapa hakuna mtu ambaye ataweza kufanya chochote kwenye minara ambayo tunayo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa hoja yako ambayo nafikiri pia yamepokelewa na Wizara.

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.