Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi nami nitumie nafasi hii kumpongeza Kaka yangu Mheshimiwa Waziri Nape kwa weledi mkubwa anaoufanya katika sekta ya habari. Kwa kweli uongozi wake wa kusaidia Vyombo vya Habari na sekta nzima ya habari tumeuona na mimi nimtie shime aendelee na mwendo huo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina hoja mbili, kwanza ni kuhusiana na utaratibu wa kuambiwa tuombe loss reports pale ambapo unapoteza laini za simu. Kwa hapa tulipo kwa sasa hivi, mtu anavyosajili line ya simu anasajili kwa kitambulicho cha NIDA na anaweka finger prints kwa hiyo, utaratibu wa kuambiwa kutafuta loss reports wakati umepoteza laini ya simu naona ni utaratibu unaoleta urasimu ambao hauna maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani utaratibu huu labda walivyokuwa wanaweka waliwawekea watu wa Mjini, kwa sababu kwa huko Vijijini tunakotoka mtu tu afike kwenye Kituo cha Polisi kwenda kuomba loss report ameshatumia zaidi ya Shilingi 10,000 ama Shilingi 5,000 ama Shilingi 15,000 nauli. Anakwenda kutafuta loss report ya Shilingi 500 au siku hizi tunaambiwa kwamba unaweza kuomba kwenye simu, haya ni mambo ya watu wa Mjini Vijijini kule internet inasumbua. Mimi sina mashaka na Mheshimiwa Waziri Kaka yangu Nape haya masuala madogo madogo, yanaleta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi simu ndiyo maisha yetu, haiwezekani mtu akatafute loss report zaidi ya siku moja, siku mbili awe nje ya mtandao. Namuomba Mheshimiwa Waziri waweze kuangalia utaratibu huu uweze kuondoka, tayari tunatumia kitambulisho cha NIDA kwenye kusajili laini zetu. Kwa hiyo, tunaomba utaratibu wa kuambiwa tutafute loss report wakati tumepoteza laini ya simu uweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye suala langu la pili kuhusiana na ulinzi wa taarifa binafsi. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 16 inasema: “kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake, unyumba wake, lakini pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake binafsi”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia habari ya usiri na ulinzi wa taarifa binafsi za mtu. Kwa nyakati hizi ambazo tunazo, simu zetu zinabeba taarifa zetu nyeti na nzito, ambazo hata watu wetu wa karibu hawazifahamu. Simu zetu zinabeba siri zetu, zinabeba ulinzi wa fedha zetu na maisha yetu kwa ujumla ya kila siku, kwa hiyo, tusipokuwa na ulinzi wa taarifa zetu binafsi ni jambo ambalo kidogo linahatarisha. Naomba nieleze kwa lugha inayoeleweka, kwenye ukusanyaji wa taarifa kuna kitu kinaitwa data collection na kuna kitu kinaitwa data processing. Data collection ama ukusanyaji wa taarifa kwa mfano kampuni ya simu inavyosajili laini yangu inachukua jina langu, inachukua makazi yangu ninapokaa na umri wangu na taarifa za msingi siyo mbaya kwa sababu ni kwa ajili ya kutupatia huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa inapoanza kuchakata taarifa hapo ndiyo ugumu unapokuja. Kwa sababu, inachakata taarifa ina maana inazi-process halafu inawapa watumiaji wengine/makampuni mengine kwa kuyauza. Kwa mfano, unashangaa tu unatumiwa message za betting kwenye simu, ina maana wamechakata wamewapa wale makampuni ndiyo maana tunatumiwa taarifa. Namuomba Mheshimiwa Waziri, Sheria ile ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi lazima ije hapa Data Protection and Privacy ili tuweze kulinda taarifa za watu binafsi, lakini taarifa zetu zinazoenda pia nje ya nchi, kwa sababu taarifa zinatumika bila idhini yetu. Vilevile taarifa zinatumika kwa kuwanufaisha wengine bila sisi kutunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kabisa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga…

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja namalizia. Kampuni za simu zinatupa terms of conditions wakati unasajili laini, zile terms of conditions zimeandikwa kwa lugha za kisheria na ngumu mno na tunaambiwa tutazikuta kwenye website. Kwa hiyo, tunaomba wakati tunasajili laini tupewe ule mkataba wa namna ya matumizi ili tuweze kuelewa kwamba tunaposajili laini tunajiingiza kwenye vitu gani ambavyo vya msingi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)