Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa sababu ya muda, nilikuwa na mambo mengi, lakini na-summaries. Nina suala la uduni wa mawasiliano Malinyi, kuna suala la cybercrime kwa maana ya uhalifu wa mitandao, lakini kuna suala la uhifadhi kwa maana ya suala la mawasiliano katika maeneo ya utalii na uhifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu Malinyi, nazungumza hili kwa kurudia kwani mwaka 2021 nililisema, tuna shida kubwa. Mpaka hivi ninavyozungumza mawasiliano hakuna kwenye Ofisi ya Halmashauri. Utendaji kazi kwa watumishi ni changamoto na wananchi wa eneo lile pia wanapata ugumu sana katika kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kata kama ya Sofi, Kata ya Kilosa kwa Mpepo ambayo iko mpakani inashikana na Namtumbo - Ruvuma, hakuna mawasiliano. Kwa kifupi hakuna hata kata moja ya Jimbo la Malinyi ambapo kuna uhakika unaweza kuwasiliana kwa asilimia 100 au hata 90. Kwa hiyo, naomba Wizara ilichukue hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 tulipata mnara kutoka UCSAF, namshukuru Mkurugenzi Mashiba, na tuliambiwa tu mchakato unaanza kwa ajili ya ujenzi, walipewa kazi TTCL, lakini mpaka leo bado. Namshukuru Mheshimiwa Waziri Nape ameniahidi, sasa ameingia analivalia njuga, kwa hiyo, ninaamini atafanya kitu kwa ajili ya watu wa Malinyi. Kwa hiyo, tunawaamini, naomba mtusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, suala la TCRA. Nadhani uwezo wetu wa mitambo ya kisasa kuweza kudhibiti suala la uhalifu mitandaoni bado ni mdogo. Kwa hiyo, kama shida ni bajeti, basi naomba Mheshimiwa Waziri bajeti ijayo ulete tuwe na mitambo ya kisasa kama ya wenzetu huko nje, tuweze kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi mpaka sasa hivi nilipoteza simu, tablets na vitu vingine, lakini wanaendelea kufuatilia, wanasema tunashughulikia. Mpaka simu iwe hewani ndiyo wanaweza wakaipata, lakini nilidhani ingefaa kabisa tuweze kupata hizi gadgets hata kama simu imezimwa, basi ionekane iko sehemu fulani, ila inaonekena kama bado tunabahatisha. Kwa hiyo, naomba tu tujitahidi mwakani kwenye bajeti mlete tuwe na uwezo mkubwa kama wenzetu wa nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hata kwenye mitandao ya face book. Watu wame-forge account fake, wametengeneza kama ya kwangu tangu 2018, nimelalamika, nimepewa RB iko Iringa, nimeandika barua Serikalini, mpaka leo watu wanaendelea kutapeli watu kwenye mitandao, accounts za face book zinafanya kazi ambazo ni fake. Namba za simu ambazo matapeli wanapokea fedha bado zipo hewani. Sasa unashangaa, inatakiwa tufanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama shida ni teknolojia, basi mwakani kwenye bajeti muilete, lakini kwa sasa Mheshimiwa Waziri mtusaidie hili jambo liweze kukoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni suala la mawasiliano kwenye maeneo ya utalii na uhifadhi. Maeneo mengi ya misitu (TFS), maeneo yetu ya game reserves, maeneo ya National Parks, kule kwenye vivutio mawasiliano hakuna. Wageni wanatalii; kwa mfano, Mlima Kilimanjaro pale ni maeneo mazuri ya watu kuona. Mtu anapiga picha na video anataka ku-share wakati huo huo dunia ione, iweze kutamani na yenyewe kupanga safari za kuja, lakini hawawezi, mawasiliano hakuna kabisa. Kwa hiyo, mtu akienda kutalii anakuwa kama ameenda sijui maeneo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi kuna haja kubwa sana ya mawasiliano yapatikane kwenye vivutio vyote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Nape ushirikiane na watu wa Maliasili, kwenye vivutio vyetu vyote mawasiliano ya simu yapatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa ni suala la vita dhidi ya ujangili pamoja na mawasiliano. Leo tunafanya doria kama za kienyeji niseme kwa Jeshi la Uhifadhi lote, tunabahatisha kutegemea tu nguvu za miguu na wapiganaji wa kawaida, lakini teknolojia ingeweza kurahisisha ujangili kwa maana ya kupiga vita ujangili. Kupitia mawasiliano ya simu ambayo unayafanya ingekuwa rahisi sana kuwa-track majangili, lakini leo kwenye vivutio vya utalii hakuna mawasiliano. Kwa hiyo, zoezi la doria linakuwa gumu, tunafanya kienyeji. Teknolojia ingeweza kutatua tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba niishie hapa kwa leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)