Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Zuena Athumani Bushiri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Mawasiliano, Teknolojia na Habari. Tunatambua kwamba, Habari na mawasililiano ni kila kitu. Bila mawasiliano hakuna biashara, bila mawasiliano hakuna kazi, bila mawasiliano hakuna kitu chochote kinachoweza kuendelea katika Mataifa yaliyoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama hapa kwa masikitiko makubwa sana kwamba katika Mkoa wa Kilimanjaro kuna baadhi ya Kata ambazo ziko kwenye mipaka ya mikoa ambazo hazina mawasiliano kabisa. Kenya Safaricom imekuwa ikitawala maeneo ya mipakani kwa sababu wananchi wa maeneo hayo hawapati mawasiliano ya nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 nilisimama katika Bunge hili nikaongelea maeneo ambayo yameathirika sana ikiwepo Wilaya ya Rombo, maeneo yote ya mpakani; Wilaya ya Mwanga, Kata za Kivisini, Jipe, Kigonigoni, Kwakoa na Toloha. Nasikitika kwamba maeneo haya kwanza yana hatari ya wanyama wakali, lakini pamoja na hatari hiyo hawana mawasiliano kabisa, hawawezi hata kujikwamua katika shida wanazozipata kuwasiliana ili wapate misaada. Naiomba Serikali iangalie maeneo yale ambayo ni hatari kwa wananchi ipeleke minara ile ili wananchi wakapate huduma stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisimama tena hapa mwaka 2021 nikiongea Habari ya minara katika Hifadhi ya Mkomazi. Hifadhi ile inapita barabara ambayo inaenda katika Makao Makuu ya Wilaya ya Same ambayo inategemea Vijiji vya Ndungu, Maore, Kihurio, Kisiwani, Kadando, Mpirani na vingine vingi vya maeneo ya milimani; wanategemea kupita barabara ile kwenda Makao Makuu ya Wilaya. Pamoja na hayo, wafanyabiashara wengi wa maeneo hayo wanaenda kufungasha mali zao Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pametokea na changamoto ya vijana kuvamia maeneo hayo na kuvamia baadhi ya Land Rover zinayopita pale kuiba na kupora mali za wananchi. Naiomba Serikali yangu Sikivu iangalie wananchi wake taabu wanazopata ili ione umuhimu wa kupeleka minara eneo lile ili wananchi wa maeneo yale wapate huduma stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ikumbukwe kwamba hifadhi ile sasa hivi imekuwa na wanyama wengi sana. Tembo kama tunavyosikia na tunavyoendelea kusema kwamba, tembo wamekuwa ni changamoto kubwa sana. Eneo lile zamani nikiwa mtoto, kwa kuwa ndiko nilikozaliwa, lilikuwa linaitwa kambi ya simba. Kwa hiyo, lina wanyama hatarishi. Inawezekana wananchi wakapata matatizo katika eneo la hifadhi, lakini wanashindwa kujikwamua pa kupata msaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, wakati mtakapokuja kuhitimisha hapa leo, mimi sitashika Shilingi, lakini mtuambie ni lini mtapeleka minara katika maeneo ya mipakani ili wananchi wale nao wakapate huduma stahiki? La kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini pia mtapeleka minara katika maeneo ya hifadhi ya Mkomazi Game Reserve ili wananchi nao wakaweze kupata huduma stahiki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)