Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mungu na nichukue fursa hii pia kuwapongeza sana Mawaziri wanaofanya kazi kwenye Wizara hii ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha Taifa letu linakua kwenye uchumi wa kidijitali, na pia kuhakikisha Taifa letu linakwenda kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia hapa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri mikakati mbalimbali ambayo wanayo kuhakikisha wanakwenda kuifanya kazi yao kikamilifu. Naomba nichangie kwenye suala zima la usalama mitandaoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri mikakati yake hapa, lakini kitu ambacho sijakisikia ni intrusion detection system. Mara nyingi matukio yanatokea halafu ndiyo watu wanaanza kuhangaika wakati tunaweza kutengeneza tools ambazo zitagundua mapema kabla mtu hajaweza kuiba. Wakati anataka kuingia kufanya uhalifu wake, tools zile zinaweza ku-detect.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Wizara hii ikafanye kazi zaidi. Naamini weledi mkubwa wa wataalam waliopo kwenye Wizara hii. Tumempata Dkt. Mwesiga, ni mwalimu wangu, naamini uwezo wake katika mambo haya, pia tuna Dkt. Pido, watu wote hawa ni wataalam wazuri, waje na mifumo ambayo itagundua mapema wizi unaotaka kufanyika kabla tukio halijafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshangaa kuona baadhi ya Ofisi za Serikali watu wanaiba mitandaoni wakati tunaweza kutengeneza intrusion detection system zikagundua mapema mambo haya. Kwa hiyo, naomba sana katika mikakati yenu, mbebe na hili tuone tunakuja na mifumo ya kugundua mapema kabla jambo halijatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba kusema kwamba, mwaka 2021 mwishoni tumeona kule Iringa, mfanyakazi wa Selcom ameweza kuhamisha Shilingi bilioni mbili na zaidi. Maana yake ni nini? Ni kwamba bado kuna shida ile ile katika wizi wa mitandaoni. Wakati kama Taifa tunakwenda kusema tunataka uchumi wa kidijitali, kuna mwananchi mmoja mmoja anazoroteshwa uchumi wake kidijitali. Suala la wizi wa mitandaoni ni tishio kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewaaminisha wananchi kwamba tunaweza tukahifadhi fedha zetu mitandaoni, lakini bado kuna hali ngumu kwa sababu wizi huo ni mkubwa mno. Kwa hiyo, naomba niishauri sana Serikali ihakikishe haraka inakuja na ile sera. Sera hii imechelewa sana. Katika nchi 54 za Afrika, ni nchi 28 tu ambazo zimekuwa na sera hii na tunataka Tanzania tuwe miongoni mwao, tusisubiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona nchi za Ulaya wana ile General Data Protection Regulation, tunataka na sisi kama Taifa twende kwa mwendo huo. Tunahitaji huduma hizi kwa haraka. Wala tusiridhike na yaliyoletwa na ITU (International Telecommunication Union) kusema kwamba sisi tumekuwa wa pili kwa usalama mitandaoni. Jinsi ambavyo wamechukua survey ya data zile, is wrong. Huwezi kuchukua kwa kutumia mfumo wa questionnaire. Walitakiwa kutafuta uhakika zaidi. Tatizo hili la usalama mitandaoni ni kubwa. Naomba sana kama Taifa tulibebe kwa uzito wake na juhudi hizo ziongezwe kupata mifumo ambayo itagundua tatizo hilo mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba, sisi kule kwetu Kilindi tuna shida kubwa mno ya kukosa mawasilioano. Kwanza naipongeza Vodacom kwa initiative yake ya mfumo ule wa mama; ile program ya mama, ya kuhakikisha inatatua tatizo la dharura mama anapokuwa mjamzito. Ndiyo maana halisi ya Wizara hii, kurahisisha huduma fulani za kijamii. Nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii i-support initiative ile ya Vodacom kuhakikisha inapeleka minara katika maeneo yale. Kwekivu, Kimbe, kule Kilindi hakuna kabisa mawasiliano. Yule mama mjamzito hata akipiga simu kwa yule dereva, dereva usiku hapatikani saa 8.00 ya usiku, tunatatua vipi tatizo lile? Inakuwaje katika kutatua tatizo la dharura? Tunaomba tupeleke minara ili wale akina mama waweze kutatua tatizo la kukimbia kwenye vituo vya afya kwa haraka zaidi na mapema zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mweshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)