Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari - Ndugu Nape Nnauye na Naibu wake Engineer Kundo Mathew na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu la Moshi Vijijini kuna maeneo ambayo yana changamoto kubwa ya mawasiliano kutokana na kutokuwa na mvuto wa kibiashara na mashirika ya kibiashara (Tigo, Vodacom, Ttcl, Halotel, Airtel) hayajawekeza kwenye maeneo haya. Maeneo haya yanahusisha vijiji vilivyopakana na Mlima Kilimanjaro katika kata za Kibosho Magharibi, Kibosho Okaoni, Uru Kaskazini na Oldmoshi Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishauri Serikali kupitia kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iwekeze na kujenga minara ya mawasiliano katika maeneo haya. Kata hizi ni za kimkakati kwani baadhi zina njia za kitalii za kupeleka watalii katika Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa UVIKO-19, mikutano ya ana kwa ana ilisitishwa kwa kuwa nchi nyingi zilijifungia ili kulinda raia wao na maambukizi ya UVIKO-19. Majukwaa maarufu ya Zoom, Skype, GoToMeetings, Microsoft Teams, na Google Hangouts yalitumika kwenye mikutano kwa njia ya mtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukwaa haya yamesaidia sana nchi yetu kwa kiasi kikubwa, hata hivyo, haikua rahisi kuandaa na kushiriki matukio mbalimbali kwa njia hii. Moja ya changamoto kubwa zaidi ni gharama kubwa za mtandao wa internet na uwezo hafifu wa mitandao. Pia ni kawaida kwenye maeneo yetu kuona upatikanaji wa huduma ya internet ikibadilika mara kwa mara kutegemeana na mahali mtumiaji alipo. Kwa mfano, wakati mtu akiwa kwenye mawasiliano, mitandao hukatika mara kwa mara wakati shughuli zikiendelea na kuwaaacha washiriki njia panda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hizi, ninaishauri Serikali iboreshe miundombinu ya mawasiliano katika maeneo yote muhimu hapa Tanzania. Maboresho haya yatasaidia kuifungua nchi hasa kwa kuzingatia kuwa tunategemea kupata watalii wengi baada ya kampeni ya Rais ya Royal Tour.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili unahusiana na huduma za habari na mawasiliano kwa watu wenye ulemavu wa usikivu (viziwi) nchini Tanzania. Kwenye hili bado kuna changamoto licha ya juhudi za Serikali za kulisaidia kundi hilo lipatiwe huduma. Viziwi ni moja kati ya makundi ya watu wenye ulemavu wanaohitaji huduma maalumu kupata habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo waliyonayo viziwi huwakwaza katika mawasiliano katika mazingira wanayoishi na hivyo kuwaathiri kwa njia nyingine mbalimbali katika nyanja za elimu, mahusiano na maendeleo ya kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya viziwi ni ya kimawasiliano na kwa hiyo hayaonekani kwa macho, viziwi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la kusahaulika katika utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali iwekeze kikamilifu na kuweka miundombinu na rasilimali watu ya kutosha ili kundi hili lipate haki yao ya msingi ya kupata habari na kuwasiliana na jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezuka tabia mbaya ya kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya YouTube na matapeli wa mitandao ya simu kwa kutumia majina ya watu maarufu. Baadhi ya taarifa zimesababisha kero, usumbufu na kuvunja heshima na haki za kibinadamu kwa wahusika kwa kuwasingizia mambo yasiyo na ukweli. Suala hili linasababisha taharuki na kuvuruga haki za kibinadamu kwa walengwa. Video hizi za YouTube husababisha hasara kwa watumiaji kwani watu hugharamia kununua bundle na kuishia kupata habari potofu. Matapeli wa simu wanaotumia majina ya watu maarufu hutapeli watu na kuomba fedha haramu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali ichukue hatua za haraka kukabiliana na tatizo la taarifa za uongo za waandishi wa YouTube na matapeli wa simu kwa mtazamo wa kulinda haki za binadamu kwa waathirika ikizingatia misingi ya kisheria na kisera inayosimamia tasnia ya habari Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na TCRA iweke utaratibu wa kuwabaini na kuwachukulia hatua waandishi wanaokiuka maadili kwenye mtandao wa YouTube na matapeli wa simu. Adhabu kali zikitolewa, mambo haya yatapotea kwenye jamii yetu ya Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.