Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa kwa kuchangia kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwa moyo wangu wa dhati kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya hasa katika kuwezesha uhuru wa vyombo vya habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii Mheshimiwa Nape na Naibu wake Mheshimiwa Kundo kwa jitahada kubwa zinazofanywa na katika Wizara hii na Serikali ya kuboresha sekta ya habari na mawasiliano nchini bado mkoani Rukwa hususani Jimbo langu la Kwela kuna changamoto bado zinatukabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumfahamisha Mheshimiwa Waziri kuwa Mkoa wa Rukwa ni takribani miaka mitatu sasa hatuna reporter wa television ya Taifa (TBC) toka aliyekuwa reporter Mzee Nswima Ernest kustaafu. Mheshimiwa Waziri ifahamike kuwa TBC ni kituo kikubwa cha habari katika Taifa letu, hivyo kutosikika kwa takribani miaka mkoani kwetu tunapoteza fursa nyingi zikiwemo za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kuwa katika Jimbo langu kuna maeneo ambayo mawimbi ya TBC FM hayakamati kabisa katika Kata za Milepa, Lusaka na kadhalika, wanapata habari za TBC kupitia runinga kwa wale wenye ving'amuzi ambao ni kundi dogo sana hasa wale waliokaribu na miji changamfu. Mkoa wa Rukwa una vivutio vingi vya kiutalii kama Kalambo falls, fukwe za Ziwa Tanganyika, game reserve na Ziwa Rukwa, lipo Ziwa Kwela na vivutio vingi vya asili vitokanavyo na desturi na tamaduni za Wanarukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa TBC FM kwa baadhi ya maeneo, tumepunguza wigo wa kutangaza utajiri wa mkoa wetu kwa ukosefu wa TBC reporter na kutokuwepo kwa mawimbi ya TBC FM katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni baadhi ya vyombo vya habari vilivyo nje ya Mkoa wa Rukwa kutoa habari zisizo na uhalisia, zenye maudhui ya kutisha wageni na hata wawekezaji juu ya Mkoa wa Rukwa na kusababishia mkoa hasara za kiuchumi. Kwa mfano vyombo vingi vya habari vimekuwa vikitoa maudhui mbalimbali kwa kutumia jina la Sumbawanga vikihusisha matendo ya kishirikina na uchawi jambo ambalo si sahihi na halipaswi kufumbiwa macho na taasisi kama TCRA na nyingine zenye mamlaka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumuomba Mheshimiwa Waziri apokee changamoto na tatizo kubwa la huduma za mitandao yaani kukosekana kwa minara ya simu inayofanya kazi kwa saa 24 kwa baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kwela lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa. Kwa mfano kuna tatizo sugu hasa Kata ya Milepa kwa Vijiji vya Milepa, Kinambo, Msia, Kisa na Talanda. Mnara uliopo Kijiji cha Milepa ambacho ndipo yalipo Makao Makuu ya Kata haufanyi kazi saa zote kwani unafanya kazi kwa saa tano tu yaani unawaka kuanzia saa 3:30 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri unakuwa umezima na siku kukiwa na mvua au mawingu basi mnara huo hauwezi kuwaka kwa siku nzima tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji hiki kinazo taasisi zinazohudumia wananchi kikiwemo Kituo cha Afya Milepa, Kituo cha Polisi, kituo cha kukusanyia mapato ya Halmashauri kilicho na Pashine ya kukusanyia mapato (POS machine), sekondari ya kata, shule za msingi zipatazo sita na ofisi za utawala ngazi ya kata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma hizi zote zimefungiwa mifumo ya malipo na ya mawasiliano kupitia mitandao, hivyo kuanzia saa 9:00 alasiri hadi kesho yake saa 3:00 asubuhi hakuna huduma inayofanya kazi kupitia mtandao na hivyo husababishwa huduma zote za umma kuzuiwa kufanya kazi kupitia mitandao ikiwa ni pamoja na kutoa risiti zote kupitia mifumo kuanzia huduma za malipo ya ushuru. Usajili wa wagonjwa kimfumo, kutoa risiti kwa wagonjwa wanapokuwa wanataka kulipia gharama za matibabu, kutoa taarifa mbalimbali za kiuhalifu polisi, kutoa taarifa zozote kwenye Idara za Elimu na Utawala yaani huduma hizi zote husitishwa kutokana na mnara kuzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi zimetokea kesi mbalimbali na kupelekea vifo hasa kwa akina mama wajawazito baada ya kukosekana mawasiliano pindi wanapohitaji huduma ya gari la wagonjwa lililopo Kituo cha Afya Milepa ili likawachukue wajawazito walioshindwa kujifungua kwenye zahanati zilizopo nje ya kituo hicho, lakini huduma hiyo hukosekana kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano kunakotokana na kuzima kwa mnara wa Vodacom ambao ndiyo mnara pekee uliopo kijiji hiki cha Milepa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki cha afya kinahudumia kata zipatazo saba zenye zaidi ya wakazi 108,700 lakini eneo wanalolitegemea kupata huduma muhimu ndilo hili ambalo tatizo la mtandao ni shida kubwa sana. Kutoka Kata ya Milepa kilipo Kituo cha Afya hadi kata ya mwisho ambayo ni Kilangawana ni zaidi ya umbali wa kilometa 125 hivyo utaona ni namna gani mgonjwa hasa mama mjamzito endapo mawasiliano yatakuwa hayapo atakavyoshindwa kuokolewa mapema pindi uhitaji wa gari utakapokuwa unahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo madaktari wanapofanya huduma kubwa hasa za upasuaji huhitaji wakati mwingine kuwasiliana na madaktari bingwa hasa linapotokea tatizo kubwa lakini hushindwa kufanya hivyo kutokana na aidha muda huo kunakuwa hakuna mawasiliano. Pamoja na tatizo hili kuwepo, umeme wa REA upo na umepita umbali wa mita 400 kutoka mnara ulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine yenye changamoto za kukosekana kwa mawasiliano kwa njia ya simu ni pamoja na vijiji vya Kizumbi, Kamnyaza na Mpembano Kata ya Lusaka, vijiji vya Katoto na Kazi Kata ya Lyangalile; vijiji vya Zimba, Misheni Kata ya Zimba; vijiji vya Mtetezi na Kapewa Kata ya Mpui na vijiji vya Msila na Kasekela Kata ya Mfinga vyote vipo ndani ya Jimbo la Kwela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba msaada wa haraka ili kuwasaidia wananchi hawa katika sekta ya mawasiliano kimtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naomba kuunga mkono hoja.