Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii nami nichangie katika mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema, lakini vile vile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii ya Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile nishukuru Bunge lako Tukufu kwa kuendelea kutupatia mchango mawazo maoni ili kuhakikisha kwamba tunaendelea kuboresha katika utekelezaji wa majukumu yetu. Lakini sambamba na hilo nawapongeza sana na kuwashukuru watendaji wote wa Wizara vile vile wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Nape Mose Nnauye lakini vile vile namshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mpango pamoja na Waziri Mkuu pamoja na Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu lakini pia natambua mchango mzuri sana ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kabisa kwamba muda hautoshi lakini natambua michango ya Waheshimiwa Wabunge inalenga kwenda kutatua changamoto za wananchi walioko katika Majimbo yao. Lakini tunasema kwamba ili nchi yoyote iweze kuendelea ni lazima kwanza tuwe na huduma bora na za uhakika, lakini kabla ya kuwa na huduma bora za uhakika ni lazima tuwe na miundombinu ambayo inaweza kutoa huduma hizo lakini pia tuwe na sera safi tuwe na utulivu wa kisiasa na sheria nzuri lakini haya yote yanawezekana kutokana na kiongozi mahiri mwenye maono na anayetaka matokeo chanya kwa watanzania ambaye sasa tunaye Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kweli mambo mengi yanafanyika kwa kasi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu zifuatazo; mwaka huu pekee minara 488 inaenda kufanyiwa upgrading ambayo ni takriban bilioni 9.76 ambayo imeandaliwa. Lakini vilevile tuna dola milioni 150 ambayo inaenda kutekeleza mradi wa Tanzania ki-digital ambapo ukiangalia ni minara 763 inaenda kujenga. Lakini vilevile kuna minara ambayo tayari imeshajenga takriban 161, kuna minara ambayo haijawashwa imeshakamilika 181. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yakishakamilika changamoto zote za Wabunge ambazo leo wameziongea hapa zitakuwa zimeisha kama siyo kupungua kwa kiasi kikubwa sana umeshuhudia Waheshimiwa Wabunge wamesimama hapa wameongelea namna ambavyo tumefika kwenye majimbo yao lakini vile vile maeneo ambayo tumefika katika majimbo yao wamejionea katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri maeneo yao yamejumuishwa katika bajeti yetu. Kwa hiyo, tuwaombe Waheshimiwa Wabunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha kwamba tunaendelea kujenga Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ambacho naweza kuongea hapa ni uelekeo wa Tanzania tunayoenda nayo sasa ni Tanzania ya kidigitali na Tanzania hii inaendana sambamba na ujenzi wa miundombinu ambayo inaenda kutoa huduma hizi. Miundombinu hii ni pamoja na Mkongo wa Taifa, ni ujenzi wa minara kama ambavyo nimetaja, katika zoezi la anuani za makazi na postcode ambalo Mheshimiwa Waziri ameongoza timu yetu ya Wizara kuhakikisha tunafikia kiwango cha asilimia 106.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa majukumu yetu haya ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 98 Ibara 61(j)na(m) ni katika kuhakikisha tunaweka mawasiliano kwa Watanzania ili waweze kufanya biashara zao, waweze kuwasiliana kwa sababu tafsiri yetu ni kwamba mawasiliano ni uchumi, mawasiliano ni usalama na mawasiliano ni haki ya kila mtanzania kuipata. Na sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais tunaenda kwa kasi kweli kweli kama ambavyo yeye mwenyewe ametuelekeza tufanye kwa utashi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyagusia naomba niyajibu kwa haraka haraka. Suala la TTCL ambalo limegusiwa na Mheshimiwa Tabasamu TTCL hawajauza minara na kama ambavyo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba TTCL tunaenda kuiwezesha ili ikasimamie miundombinu yote ya kimkakati ikiwemo na ujenzi wa minara na usimamizi na Mkongo wa Taifa minara yote na miundombinu mingine yote ya kimkakati TTCL inaenda kusimamia. Kwa hiyo, niliomba niweke ufafanuzi kwa namna hiyo katika upande huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile naomba nitolee ufafanuzi jambo moja ambalo liliongelewa na Mheshimiwa Zuena Mheshimiwa Bushiri. Kwenye suala la Mkomazi tayari tumeshaliingiza katika utekelezaji kwa bahati mbaya katika bajeti iliyopita tuliliingiza kwa bahati mbaya watoa huduma hawakuweza kulichagua lakini tumeliingiza kwenye mpango mahsusi wa National Parks ambapo sasa tunaenda kuhakikisha kwamba tunaweza utaratibu maalum ili mtoa huduma lazima apatikane kwa ajili ya kufikisha mawasiliano katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile suala jingine ambalao nimeona Mheshimiwa Condester Sichalwe ameliongelea kwa sababu ameongelea masuala ya teknolojia na sisi tunahakikisha kwanza tunaweka Sera safi ambayo ni wezeshi wawekezaji waweze kuja lakini vile vile katika force industrial Revolution imaging technology hatuwezi kuzikwepa kwa sasa. Imaging technology ni kama vile Artificial Intelligence, Block Chain Technology, Internet of Things haya yote tunaenda kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira rafiki ili yote yaweze kufanyika kwa sababu…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: …na sisi ndiyo uelekeo wetu wa Tanzania kwenda katika Tanzania ya kidigitali…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, majibu mazuri!

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.