Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Kwa muda toka asubuhi tumekaa hapa tukiwasikiliza ushauri wenu, maoni yetu na maelekezo yenu. Niwahakikishie mimi na timu yangu tutayazingatia na kuyatekeleza ipasavyo. Maelekezo mengi na ushauri mwingi uliotolewa hapa mwingi umejikita kwenye maeneo makubwa mawili, yapo maeneo yanayogusa Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu mbalimbali tunazotumia katika kuendesha maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili limegusa utendaji wa Serikali, Wizara na Taasisi tunazoziongoza. Kwa sababu ya muda, siwezi kugusa zote lakini niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Wizara imeandaa Semina kabla ya Bunge hili kuisha kwa maana ya kipindi hiki. Tumeandaa Semina na baada ya kusikiliza michango yote hii Semina tutakayoiandaa itagusa maeneo yote waliyoyazungumza Wabunge ili tukazungumze kwa uwazi, kwa upana, tuone namna ambavyo tutachukua mawazo ya Wabunge. Tutaona hali ya Serikali, halafu tufanye maamuzi yenye tija. Kwa hiyo niwahakikishie, hakuna mchango ambao umepotea, yote tutahakikisha tumeichukua, tumeizingatia na tutaifanyia kazi. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge Semina hiyo itakapotangazwa tushiriki, tuje na maoni hayo, Wizara na Taasisi zetu na wadau wote tutakuwepo kwa ajili ya kuyaweka mambo haya sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hoja juu ya namna ya kwenda kwenye uchumi wa kidigitali. Tumeeleza hapa jumla ya bajeti yetu inataka kutupeleka kwenye uchumi wa kidigitali wa nchi yetu, sasa tumeanza safari, lakini hii safari wenzetu wameanza siku nyingi sisi tupo kwenye safari hii, tumepanga katika mwaka huu wa fedha kukamilisha framework itakayoeleza namna gani uchumi wa kidigitali unajengwa. Katika framework hii tutazungumza ushiriki wa kila mmoja, lakini tutapitia Sheria, Sera, Kanuni na Taratibu tutazibadilisha na zipo nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapa mfano mzuri, kaka yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, amezungumza namna ambavyo Mtanzania leo anatembea na vitambulisho vingi sana. Kuvijumlisha hivi vitambulisho kuna hitaji mabadiliko ya sera, ya sheria ya kanuni na taratibu na sisi tunaona, dunia tunakoenda huitaji kutembea la rundo la vitambulisho, lakini ili ufike huko, lazima utengeneze mabadiliko ya baadhi ya hizi sheria ambazo sasa kwenye blue print na hapa nimeeleza tumepata zaidi ya dola milioni mia moja hamsini kwa ajili ya kuchora hii ramani ya huko ambako tunataka kuipeleka Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo nadhani muhimu niiguse, nia ya Rais Samia na Serikali ya Awamu ya Sita ni kuongeza na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza katika nchi yetu. Ameingia madarakani yale mambo ambayo hayakuhitaji mabadiliko ya sheria na wote nyie ni mashahidi tumechukua hatua kubwa na wanahabari wanajua. Tumefungulia vyombo Habari yakiwemo magazeti, na mitandao. Baadhi ya sheria ambazo zipo tumeamua kutozisukuma na kuzitekeleza ili mambo yaende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni nia njema na thabiti kwamba jambo hili tunataka tulifikishe. Nataka niahidi nimesikia mchango wa dada yangu Mheshimiwa Ester Bulaya, niwaahidi wanahabari mwaka huu wa fedha tunaouombea fedha sasa tutakamilisha mabadiliko ya Sheria ya Huduma ya Habari kama ambavyo inatakiwa na tumeanza mchakato, tumekutana nao mara. Niwaambie nia ya dhati ipo, tutafanya mabadiliko na tutasonga mbele kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwathibitishie kwamba, zipo sheria Wabunge wamezitaja hapa kwa mfano Sheria ya Data Protection Sheria ya TEHAMA na sheria mbalimbali. Maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita, Mama hodari kabisa, amesema tupitie sera, sheria na kanuni tuone namna ambavyo zile ambazo zimepitwa na wakati tuzitengeneze tuzirekebishe. Niwaahidi Wizara yangu sheria zote, sera zote, kanuni zinazohusika na Wizara hii tutawashirikisha vya kutosha wadau ili tutunge sheria zinazotokana na mawazo ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani pia nigusie, nashukuru kwa pongezi walizotupa katika usimamizi wa zoezi la anuani ya watu na makazi. Jambo hili tumelisimamia wote Jambo hili ni la Watanzania pale tulipofikia kuna mapungufu ya hapa na pale, tumeomba fedha na tunaendelea kurekebisha na tutashirikiana pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru usimamizi wa Waziri Mkuu, lakini wa Rais, Rais aliamua kwa makusudi akatoa zaidi ya bilioni 28 kwenda kutekeleza jambo hili. Aliahidi, akatoa na hapa ni vizuri nikasema hoja ya kaka yangu Mheshimiwa Kapinga. Maelekezo hatukuelekeza kuhamisha fedha za miradi ya maendeleo mingine kupeleka kwenye zoezi la anuani na makazi, kama kuna mahali wamefanya hivyo, wamekosea fedha husika zirudishwe kwenye miradi husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulichoelekeza, kwanza kuna fedha zilikwenda na kwa Mbinga tumepeleka zaidi ya milioni mia moja na kitu kwa ajili ya zoezi hili. Sasa kama kuna mahali fedha zimetumika za miradi marufuku kutumia fedha za miradi mingine ya maendeleo kutekeleza zoezi la anuani za makazi. Tumesema fedha zitumike, kama kuna wadau, kama kuna taasisi za Serikali zitumie fedha za dharura na siyo kuhamisha fedha za miradi ya maendeleo, hilo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ilitolewa hapa, dada yangu Mheshimiwa Salome ameniambia bando ngoja niseme. Jambo hili tutalieleza vizuri wakati wa semina, lakini hapa niseme jambo, bando kama bando ni huduma ya ziada kwenye huduma ya data, ni huduma ya nyongeza, mtoa huduma anaamua kutengeneza bandos nyingi ili akupe wigo wa kufanya uchaguzi wa huduma unayoitumia. Hapa kwetu asilimia 98 ya watumiaji wa data wanatumia hii huduma ya ziada, majirani zetu asilimia kubwa wanatumia basic tariffs hawatumii hizi bado kwa sababu bado ni kidogo mno, ni sehemu ndogo na kama ninavyosema ni huduma ya ziada.

Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji hapa wa hizi data, data moja inazalishwa kutoka Sh.2.3 mpaka Sh.9.0. Hapa Tanzania tunauza kwa Sh.1.5 as we are talking tunauza chini ya gharama ya kuizalisha hiyo data. Sasa watoa huduma walichofanya wakaona katika msingi ukitaka kutumia basic tariffs huduma zitakuwa za ghali sana, ndio maana wakaamua kuweka bado nyingi. Sasa bando ni sawa sawa leo ukinunua tiketi yako, tiketi ya kuitumia kwa mwezi mmoja kwenye basi ukiitumia siku moja muda wa mwezi mmoja ukaisha huwezi kwenda kuidai hii tiketi kwa sababu hii umepewa ofa, kama hautaki kutumia ofa ya mwezi mmoja, tumia ya siku moja moja, ndio biashara ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kuna maneno yanasemwa kama vile kuna wizi, kuna wizi. Nasema tumefanya utafiti mwingi wa kutosha na tukatoa wito, kama kuna mtu anadhani ameibiwa, njooni tufanye uchambuzi. Hata hivyo, hebu tujiulize, kampuni zinazotoa na naogopa sana kuwahukumu haya makampuni kwamba wanatuibia, mimi kama Serikali bila kuwa na ushahidi hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu twendeni Kampuni ya VODACOM, ya Tigo, ya Airtel wapo listed kwenye soko la hisa, wanafanyiwa ukaguzi, niambieni ni nani anakaa kwenye kampuni hii kubwa ya simu anasema twendeni tukaibe data, halafu inapitishwa kwenye kikao, halafu anaambiwa yule mtaalam anaye-set kwa sababu wizi lazima u-set, ana-set wizi, hii fedha inayotokana na wizi nani anachukua, kwamba inaingia kwenye vitabu vya kampuni ambayo ipo listed kwenye makampuni, serious Hapana! Nataka kuwaomba Watanzania, twendeni taratibu, naamini uelewa TCRA wametoa press release nzuri sana, wakaeleza kwa kirefu na hili jambo likapungua kelele zake. Nataka kwenye Semina tutakayoifanya hapa niwaombe …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nape, dakika moja.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, …Waheshimiwa Wabunge waje na ushahidi halafu waje tufanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Wakuu wa Taasisi na wataalam ambao kwa kweli wamenisaidia katika kutekeleza majukumu yangu. Natambua mchango wenu na nawashukuru sana. Niwashukuru sana wanahabari wa Tanzania kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kutekeleza majukumu yetu, lakini niyashukuru makampuni ya kutoa huduma na hasa makampuni yanayotoa huduma za simu, hasa simu za mkononi kwa uwekezaji wao, kwa teknolojia wanayoitoa, ulipaji wa kodi na huduma mbalimbali, lakini ajira walizowapatia Watanzania. Kwa niaba ya Serikali naomba tuwapongeze sana na kuwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge, chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Kakoso na Makamu wake Mheshimiwa Mama Anne Kilango kwa usimamizi wao mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi na naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.