Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia leo, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii mchana huu wa leo.

Mheshimiwa Spika, nimesoma vizuri sana kitabu hiki cha bajeti ya Wizara ya Ujenzi; mwaka jana 2021 barabara ya kwetu hii inayoanzia Karatu- Mbulu - Hydom - Sibiti ilishakuwepo kwenye mpango huu wa kujengwa. Nataka nirejee kumbukumbu hizi ili ukafahamu vizuri.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2000 kuja 2005 barabara hii ilikuwepo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi; lakini 2005 kuja tena 2010; mwaka 2010 kuja 2015; mwaka 2015 kuja 2025. Nataka kuwaonesha nini, nataka kuelezea tu Mheshimiwa Waziri ajue kwamba hii barabara ambayo imekuwa katika ilani kwa muda wa miongo hii minne mpaka leo haikujengwa kabisa kwa kiwango hicho cha lami. Lakini ukiangalia nimekuja na ilani hizi mbili kabisa hapa ili walau iwe ushahidi na ajue Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kweli sasa mimi nimetumwa huku kuiomba barabara hii na nimeombwa sana na wananchi wanapata shida kwa sababu tu barabara ile inakwenda kwenye Hospitali kubwa ya Rufaa ya Hydom.

Mheshimiwa Spika, hii hospitali inategemewa na majimbo saba, lakini pia hospitali hii pia pamoja na majimbo haya mvua ikinyesha barabara hii haipitiki kabisa, nimeona kwenye bajeti hii ipo imetengewa fedha. Ukiangalia sasa hivi mwaka jana kama itaruhusiwa hapa naweza kukumbusha kidogo kwenye kishkwambi changu ninayo sauti ya Mheshimiwa Waziri aliyetangulia, wakati anahitimisha bajeti yake hapa akatangaza kabisa hapa barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami kutoka Mbulu kuja Hydom na mwaka jana kwa bahati nzuri ulikuwa hapo na kama itaruhusiwa nifungue hapa ili aone kabisa;

Hapa Mheshimiwa Flatei G. Massay aliweka rekodi ya sauti ikisema:-

“...ambayo tumeanza kuitangaza wiki hii ni kama ifuatavyo barabara ya Mbulu - Hydom kilometa 25, barabara ya …” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka tu uone kwamba mambo yalivyo hapa, siyo hiyo tu katika majibu ya Wizara hii mimi nawapenda sana Mheshimiwa Mnyaa rafiki yangu kabisa, Mheshimiwa Godfrey rafiki zangu kabisa, lakini majibu wanayojipa kwa watu wangu kule ni hatari sikiliza na hii:

Hapa Mheshimiwa Flatei G. Massay aliweka rekodi ya sauti ikisema:- “...ya Mbulu na hasa Mbulu - Hydom yenye kilometa 50, kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ambayo pia Mheshimiwa aliombea kupiga sarakasi itatangazwa kabla ya mwisho wa mwaka huu ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sina shida leo nimekuja kwa amani kabisa ndugu zangu hawa nimekuja kwa amani kabisa leo na napenda niseme kwa amani ya Mungu na Mungu awatembelee na hawa. Sikiliza mwaka jana wamesema kwenye bajeti hapa kabisa kwamba kwa kweli watatangaza na nikaomba kushika shilingi hapa, wakaahidi vizuri kabisa na mimi nimechukua sauti hizi kwenye local yetu ya media hapo na ninayo kitu kinachoitwa maneno yote na hotuba yao na mwisho wa kumalizia.

Mheshimiwa Spika, niwaombe ndugu zangu hawa kwa sababu walisema watatangaza muda umepita mwaka mzima, sasa hawatangazi hii barabara na kama wametangaza wananchi wetu kule hawajui, kutangazwa huko kwa barabara ni mwaka mmoja tangu wakati wa mwaka jana ule.

Mheshimiwa Spika, sasa naona kabisa leo kwenye ukurasa huu wa bajeti wa kitabu chake Mheshimiwa Mnyaa ameandika hapa ukurasa wa tisa kifungu cha 17 anaonesha kabisa barabara itajengwa kwa kiwango cha lami kilometa 387.

Sasa mimi hoja yangu tu ya msingi nimeona hapa hoja ya Kamati, kamati wameandika kabisa kwamba kwa bajeti ya mwaka jana fedha wamepeleka kulipia madeni. Sasa niambie kama fedha zimepelekwa kulipa madeni na wao wameniahidi mwaka jana hapa barabara hii inajengwa, leo mwaka mzima umeshapita hilo tangazo linachukua muda gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi leo hapa siyo shilingi tu mimi shilingi hiyo wananchi wameniambia niichukue, nirudi nayo Mbulu Vijijini maana hapa hamna namna tena unajua kabisa hapa nikipiga sarakasi utanitoa nje na kama hunitoi nje nianze sasa hizi, halafu moja kwa moja najua kabisa huyu ndugu rafiki yangu hapa nafanyaje sasa, lakini wananchi wanataka barabara.

Leo hii angalia tunakwenda bajeti ya mwaka 2022/2023 barabara wananiambia itatangazwa tu kilometa 25; sasa hivi nimekwenda nimeongea naye vizuri kabisa nina marafiki kweli kweli wako kwenye Serikali hii, mimi naona wananitengenezea ajali, ajali yenyewe ni ipi wameahidi tumeahidi kama chama chetu hapa. Chama changu kwa nini kitengenezewe ajali? Sasa kuliko kitengenezewe ajali chama changu si bora uniruhusu niruke manyati hapa ili wastuke! (Makofi)

Sasa nafanyaje! Hebu angalia nikwambie tumepeleka kwenye ilani hii iko kwenye ilani, ilani zote zipo nimeeleza sauti zao unazisikia ninazo hapa, Hansard kule maneno yao yako, ninayo hapa ukitaka nakuletea Hansard wamezungumza hawa wakubwa zangu maswali nimeuliza kwa mwaka jana mara saba mwaka huu mara nne. Nafanyaje hapa nisaidie nifanyaje? (Makofi)

Mimi nakuomba wewe wao nimezungumza nao sana inatosha na kwa sababu inatosha mimi sitakuruka hapa mimi ni mtiifu sana mtiifu kwa baba Mungu wangu, na mtiifu kwa Bunge hili na watiifu kwa watu wangu.

Mheshimiwa Spika, sasa mipango yote nimefuata, utaratibu wote nimeufuata, inatia uchungu utaratibu wa Kibunge nimeufuata, utaratibu wa Serikali nimeufuata waulize Makatibu Wakuu nawashukuru sana hata yule mama mgeni nimekwenda ofisini kwake nimeenda; tumekwenda Wabunge saba Mheshimiwa Hhayuma, Mheshimiwa Zacharia, hata Mwigulu pia tumeenda naye, tukaomba bwana wekeni basi mambo yaende hayaendi sasa!

Mheshimiwa Spika, kwangu mimi sasa hivi wanasema wameweka fedha kwenye madeni, wamelipa madeni. Sasa kwa nini hiyo fedha ambayo wamelipa madeni msiingie hiyo fedha kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali tukawa na madeni yote kama Serikali nzima hii ya Mbulu tu kuja Hydom kwa nini mnaweka kwenye madeni?

Mheshimiwa Spika, nifanyaje sasa ndugu yangu? Baada ya hapa yaani baada ya kuzungumza, kuleta hoja wananchi barabara hawaoni, mimi kila siku naambiwa upembuzi yakinifu, details design, sasa tunajenga, tumetangaza tender, tender yenyewe haionekani, saa hizi tena naambiwa wametangaza tender kilometa 25.

Mimi ni mtaaalmu wa sarakasi hakika nasema maana yake sasa nilichofanya kwa elimu yangu nimepita vyuo vyote nimekuja hapa nimezungumza zaidi ya hapa unafanya nini mwanaume wa watu? Nimetumwa na wananchi hapa wanasema wanaleta barabara hawaioni. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, umefika Jimbo la Mbulu Vijijini hakuna barabara mwanafunzi wa shule hawezi kujua barabara kwa sababu lazima nimsafirishe nimpeleke Babati, wanakuja hapa ndiyo wanakuja kuona hata namna ya barabara hawajui kilometa moja nzima hamna. Karatu wakati wa masika wananchi wanaomba Mungu mimi nikwame ili gari langu likikwama labda nitaelewa. Siku moja nimekwama wakasema safi sana labda hasemagi sasa baada ya haya Flatei Massay nafanya nini?

WABUNGE FULANI: Ruka sarakasi.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, niruhusu leo niwaoneshe mambo yaani leo ngoja nipige. (Makofi)

(Hapa Mhe. Flatei G. Massay alibinuka sarakasi)

SPIKA: Mheshimiwa Flatei, Mheshimiwa Flatei. (Kicheko)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, niongeze? Haiwezekani hapa mimi naelewa nimechukua. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mnyaa elewa nimechukua mzee, leo ama zangu ama zako. Mheshimiwa nimechukua leo nataka uniambie barabara hii usipoileta siku ya mwisho hapo mzee mimi naanza mambo maana haiwezekani Mheshimiwa.

SPIKA: Mheshimiwa...

MHE. FLATEI G. MASSAY: Sasa wananchi hawaelewi kabisa kwa sababu wewe umepeleka hii barabara pabaya, mimi kulia siwezi mwanaume haliagi, mwanaume anasema na kusema kwangu ndiyo huku angalia hapa saa hizi wameweka vizuri kabisa hapa wameandika tena wameongeza kilometa 25 tena wameongeza sasa wanasemaje; kutoka Labai hadi Hydom. Mwaka jana wanasema kutoka Mbulu mpaka Garbab; mwaka huu wanasema kutoka Labai mpaka Hydom. Sasa hii nini?

SPIKA: Mheshimiwa Flatei, sasa muda wako umekwisha.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakuheshimu sana unielewe naheshimu hata hili Bunge, naheshimu chama changu, naheshimu kila kitu.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, naomba mwishoni kwa kweli nikamate hii shilingi aniambie

SPIKA: Umeshaeleweka hoja yako. Muda wako umekwisha, ahsante sana.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mungu akubariki. (Makofi)