Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kushukuru Serikali kipekee kiongozi Mkuu wa Serikali ambaye ni Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Ninamshukuru kwa sababu mbili; sababu ya kwanza ni kwa sababu ya wataalam ambao amewapa kazi ambao ni Waziri wetu wa Ujenzi, Naibu Mawaziri, pamoja na watendaji wake.

Mheshimiwa Spika, lakini namshukuru kwa sababu ni kiongozi ambaye anaamini kwenye maono pamoja na matokeo. Nimetumwa na watu wa Mufindi Kusini leo kama barabara za Nyololo - Mtwango na Mafinga - Mgololo hazipo kwenye bajeti nigomee kupitisha bajeti hii leo. Kwa sababu wameahidiwa kwenye Ilani ya CCM, msururu wa viongozi wamefika huko, lakini pia unyeti wa maeneo hayo, lakini nafikiri msimamo wangu nilioingia nao utakuwa mlegevu kidogo. Kwa mara ya kwanza watu wa Mufindi Kusini tumeona kwenye bajeti ukurasa 173 ujenzi wa barabara ya kutoka Mafinga - Mgololo kilometa 78, na ujenzi wa barabara Nyololo - Mtwango kilometa 40.

Mheshimiwa Spika, ukiacha kwamba kwenye Ilani ya CCM yamesemwa nikikueleza orodha ya viongozi waliotembelea Mufindi Kusini, nikikueleza unyeti wa maeneo hayo, kwa maana ya viwanda unaweza ukasikitika sana. Wote tunafahamu kwamba Mufindi Kusini makampuni makubwa ya chai yote nchini Tanzania yako Mkoa wa Iringa, yako Mufindi, yako Mufindi Kusini. Kiwanda kikubwa cha karatasi Barani Afrika na ukanda wa Afrika Mashariki cha Mgololo kiko Tanzania, kipo Mkoani Iringa, kipo Mufindi Kusini.

Mheshimiwa Spika, viwanda vya nguzo kwa wingi katika nchi yetu viko Iringa, viko Mufindi Kusini. Siyo hilo tu hata shamba kubwa la miti katika nchi yetu la Sao Hill liko Mufindi Kusini pamoja na Mafinga. Lakini pia hata viwanda vya fiberboard viko pale Mufindi Kusini nikianza kuvitaja kwa uchache hapa pamoja na faida zake nitataja kimoja tu cha Mgololo.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Mgololo kimeanza miaka ya 1980, kina supply karatasi ukanda wote huu, chenyewe peke yake kina magari zaidi ya 70 ma-heavy trucks, lakini yako magari mengine yanayoingiza mizigo pale ndani zaidi ya 90, yako yanayokuja kwa ajili ya kufanya boiler (kuchemsha maji) kwenye kiwanda yako 90, viko viwanda vya Wachina pembezoni. Kwa hiyo kiwanda hiki kinaajira zaidi ya 7,000, magari zaidi ya 200 na kodi yake peke yake ni zaidi ya bilioni pengine 25 mpaka 30. Ukivichanganya viwanda hivi vinaiingizia Serikalini kodi ya zaidi ya bilioni 50 kwa mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukichukua kwa miaka 10 ni bilioni 500; barabara tunazozitaji kuzijenga hazihitaji hata bilioni 120 watu wa Mufindi wanauliza wamemkosea Mungu nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikikupa orodha ya ziara ya viongozi kuanzia mwaka 1980 nimechukua sample tu; tarehe 10 Oktoba Mwalimu Nyerere alifika pale Mufindi Kusini; tarehe 10 Aprili, 1987 aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Salim Ahmed Salim alifika Mufindi Kusini akaahidi; tarehe 30 Aprili Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi alifika kwenye kiwanda hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kanali Kinana - Waziri wa Ulinzi alifika pia tarehe 12 Juni; lakini Mwalimu Nyerere tena tarehe 4 Agosti, 1988 asubuhi saa tatu alifika tena akitoa ahadi hizo hizo. Wana Mufindi wakiahidiwa hayo hayo. Haikuishia hapo Makamu wa Rais Dkt. Omar Ali Juma yeye alichelewa kidogo alifika saa tano alifika tarehe 9 Machi, 2002. Aidha, Rais wetu wa sasa akiwa Makamu wa Rais alifika Mufindi Kusini katika Kiwanda cha Mgololo tarehe 11 Februari, 2018 akaahidi, haikuishia hapo tarehe 1 Oktoba, 2021 Mheshimiwa Mizengo Pinda alifika; orodha ni ndefu Kasekenya ametumwa na Waziri Mbarawa amefika, Mheshimiwa Waziri Mkuu bahati mbaya hayupo hapa leo alifika Iringa alizungumzia. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tarehe 29 Septemba, 2020 akiomba kura alifika Mufindi Kusini; Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Rais mwaka 2005 alifika pale na akazungumza. Wote hawa walikuja na wakaahidi ujenzi wa barabara hizo.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye mpango wa tatu na mpango wa pili wa miaka mitano theme yake kuu ilisema naturing industrialization for economic transformation and human development. Ukiangalia anazungumzia viwanda, anazungumzia kuongeza manpower ya watu.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Ilani ya CCM, ilani yetu ya CCM ambayo sehemu kubwa tuko hapa ukiangalia kifungu cha pili anasema moja ya majukumu yetu itakuwa ni kukuza uchumi wa kisasa fungamanishi, jumuishi na shindanishi unaojengwa kwenye misingi ya viwanda huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.

Kwa nini tunapiga kelele kuhusu kujenga barabara ya Mufindi Kusini? Sitaki kusema nchi hii maeneo mengine siyo muhimu sana, lakini tutakuwa ni watu wa ajabu sana dunia itatushangaa unakimbilia kujenga maeneo ambayo hata production iko chini unaacha sehemu ambapo ukiongeza barabara, ukijenga barabara, utasafirisha bidhaa, utaongeza uzalishaji hata dunia itakushangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu moja nimepongeza viongozi kwa hatua kubwa ya kuingiza kwenye mpango leo na watu wa Mufindi Kusini leo wanashangilia. Lakini tunaomba barabara hizi zianze kujengwa sasa nimezungumza na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, tumekutana zaidi ya mara 11, zaidi ya mara tisa tumekutana na Naibu Waziri, lakini tumezungumza na Waziri wa Fedha nimefurahi kuona leo wamekubali kwamba barabara ya Mafinga - Mgololo itaanza kujengwa katika utaratibu wa kawaida. Lakini Nyololo - Mtwango itajengwa kwa mfumo wa EPC + unfinanced kwa maana engineering, procurement, construction na finance na amenihakikishia Waziri mwaka huu wa 2022 inaanza kujengwa.

Mheshimiwa Spika, nikuombe wewe kwa nafasi yako pia pamoja na Serikali kwa ujumla ahadi hii ya Serikali na ili tuendelee kuonekana watu serious mbele ya Watanzania ujenzi huu uanze mara moja. Tumepiga danadana kwa miaka 60 sasa hatimaye tukatekeleze na wananchi wetu waone umuhimu wa wao kuelekeza eneo lao kwa ajili ya uchumi wa viwanda na tuzidi kuongeza ajira zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)