Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika Wizara yetu hii Fungu 98.
Awali ya yote na mimi nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoendelea kufanya nchini, lakini pia nimshukuru sana nakumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima lakini pia na watendaji wakiongozwa na Balozi Mhandisi Aisha Amour; Mheshimiwa Aisha Amour Katibu Mkuu wa Wizara hii ya ujenzi hasa sekta ya ujenzi, kwa kweli ni mchapakazi mkubwa, mimi binafsi namtambua amekuwa RAS wangu nikuwa Mhasibu Mkuu wake Mkoa wa Kilimanjaro, kwa hiyo lazima niseme ukweli kwa jinsi ambavyo umeaminika ninajua sasa utakwenda kutusaidia katika Wizara hii kutuvusha kwa changamoto ambazo wengi wameendelea kusema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo na hasa nimempongeza Mheshimiwa Rais mahususi sana na lazima niseme kwa nini kwa sababu ya barabara yetu ya njia nane upanuzi wa barabara ya njia nane inayotoka Kimara mpaka Kibaha kilimeta 19.2 ambayo imeenda sambamba na madaraja ya Kibamba pale Kiluvya na daraja la Mpiji, tunamshukuru sana na Watanzania wengi, Wabunge wengi hiyo barabara ni ya kitaifa na wameiyona. Mheshimiwa Rais ana sababu za kushukuliwa katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam tumezungumza sana mambo ya Dar es Salaam, Waheshimiwa Wabunge wengi katika barabara hizi, wanatamani ziende kule zikaunganishe Wilaya, Mikoa na kadhalika zibebe mazao na mambo mengine ili yaende kwa wale walaji. Lakini leo nataka niwaambie kwa nini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Dar es Salaam? Kwa sababu sensa ya mwisho ya mwaka 2012 ilituambia tuna takribani ya watu milioni 4.2 lakini sasa hivi kuna maoteo ya makadirio ya watu au kadirio la watu la zaidi ya milioni sita kama Dar es Salaam na hii ni zaidi hata ya Afrika Mashariki katika majiji mengi pia zaidi sio tu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa nini Dar es Salaam? Ni kwa sababu ndio Jiji linalokuwa kwa kasi sana, miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi duniani, lakini kwa nini Dar es Salaam, Dar es Salaam ndio lango linaloongoza kwa kuingiza na kuondoa watalii yaani kazi kubwa aliyoifanya Mheshimiwa Rais juu ya jambo hili ambalo amelifanya Dar es Salaam ndio lango la hawa watalii sasa. Kuingia na kutoka, kwa hiyo wananchi hawa na Waheshimiwa Wabunge mjue Dar es Salaam katika umuhimu wake huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata kodi ni zaidi ya asilimia 85 kama kodi ndio inapatikana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, lakini zaidi contribution ya Dar es Salaam kwenye GDP tunaambiwa kwa research ya mwaka 2020 iliyofanyika zaidi ya shilingi trilioni 25.3 zinapatikana Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na hilo sasa niende kwenye hoja zangu mahususi, utanielewa sasa kwa nini nalilia Dar es Salaam. Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/2022 Dar es Salaam ukiondoa barabara kubwa hiyo ambayo nimeitamka ya kitaifa ziko barabara za kimikoa na sio nyingi, nikizitamka katika bajeti ya 2021/2022 ilitamka barabara ya Kibamba - Kisopwa - Kwembe - Makondeko kilometa 14 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kilichofanyika hivyo barabara kilometa 14 tu ndani ya Kibamba, lakini kuna barabara ya njia panda Matosa - Goba kwenda Matosa mpaka njia ya highway barabara kubwa kilometa sita. Katika kipindi cha miaka mitano mpaka leo tunamtafuta mkandarasi amepewa kilometa moja; miaka mitano na barabara hii ni muhimu kwa wananchi wa pale na wengi hapa wanapita na Wabunge wengi wanaishi pale kwenye ile barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Goba - Njia Nne kuelekea Matosa mpaka inatoka kwenye barabara ya njia nane hakuna kinachofanyika miaka mitano. Tuombe sana jicho la huruma liendelee kwenda pale kilometa tano; wenzetu wanaongea kilometa 100, 78, 304 ni kilometa sita hakuna kinachofanyika Dar es Salaam kweli ndani ya umuhimu wote nilioueleza huu mambo yote haya ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa kweli tunawaombeni sana mtuangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hapa la utekelezaji wa ahadi za Rais na viongozi wakuu, walisema mwaka jana kwenye bajeti ya mwaka jana Waheshimiwa Wabunge walisema kama nchi lazima tuone tunapoalika viongozi wetu wakubwa wanakuja kwenye mikoa yetu, kwenye majimbo yetu tunatamani kuwaomba vitu, na tukiwaomba wananchi wanajua leo amekuja mfalme na yapo maneno mengi ya kiswahili ambayo yanatumika juu kuenzi na kuheshimu wa ujio wa viongozi wa kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiongozi wa kitaifa anafika anaahidi hakuna kinachotekelezwa, lakini hata taarifa ya Waziri haituambii utekelezaji wa maelekezo na maagizo ya viongozi wa nchi imetekelezeka kwa asilimia ngapi. Kwa upande wa TAMISEMI, TARURA na sasa hivi ninatoka kwenye Kamati ndani, wameeleza hata utekelezaji wao umefikia asilimia 85 ya maelekezo au maagizo ya viongozi wa kitaifa, huku ni ngapi, hamjasema, tunataka kujua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua ninayoisema ya pale ndogo tu ya tarehe 25 Februari, 2019 nimepata bahati ya kusema na watu wanajua niliomba barabara ya kwanza, junction ya Makabe kwenda Msakuzi kutokea Mpiji Magohe kilometa tisa tu, lakini barabara ikaunganishwa na barabara inaitwa Kwa Yusufu kwenda Mpiji Magohe hadi Mabwepande.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na barabara ya tatu inatoka Njia Nane kwenda Njia Panda ya Shule kuelekea Kibwegere mpaka Mpiji Magohe, jumla ni kilometa 37. Wakati fulani niliuliza swali la msingi hapa nikaambiwa sasa ipo na imewekea hela na inaendelea kutengenezwa. Leo bajeti ya 2022/2023 lugha inayozungumzwa hapa upembuzi yakinifu, upembuzi wa kina sijui na mambo haya ya kitaalam taalam, mimi mhasibu hata sijui hayo maneno yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunaenda mbele tunarudi nyuma hoja ambayo itatoka leo hapa kwamba wananchi wataniuliza tuliambiwa na Hayati barabara hizi angetamani hela zitolewe kwingine zijengwe kwa haraka na azione zikiisha, ndani ya siku saba akafariki. Leo ujanja ujanja mtupu kama vile aliyetoa ahadi ni Rais sio taasisi. Ahadi ilitolewa na taasisi ya Uraisi tunaombeni sana msisababishe viongozi wakashindwa kuja tena, tunaombeni mtusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili niliona niliseme vizuri Mheshimiwa Waziri ukija kuhitimisha utuambie ndani ya Jimbo la Kibamba barabara chache hizi za kilometa 37 unaziachia kilometa ngapi na sio maneno ya kiahandisi ambayo unaendelea kutujazia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli mimi leo nilisema sitaki kusema maneno mengi dakika tano zinanitosha, ziada niombe tena naomba kwa heshima Wizara hii ituonee huruma sio leo kila siku niseme maji niseme watu wa Kibamba, nizingumze ardhi kesho kutwa nitasema Kibamba ya shida, nizungumze uchumi wa watu wa shida Kibamba tunaombeni msaada ili tuheshimishe, tuhemishe Chama chetu cha Mapinduzi chenye nia njema na Watanzania na Watanzania wanavyokipenda na kukipa kura nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kusema haya yaliyo machache, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)