Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kupewa fursa ya kuchangia bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze viongozi wa Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi; Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri mnafanya kazi kubwa na kusema kweli mnapeleka kicheko kwenye mikoa na wilaya zetu na Majimbo yetu. Niwapongeze watendaji wakuu na taasisi zote zilizoko chini ya Wizara hii, kusema kweli bila wao hata Waziri hii kazi ambayo inaonekana haiwezi kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nazipongeza Wizara zote ambazo ziko chini ya Serikali ya Mama yetu Samia Suluhu Hassan, zinafanya kazi nzuri. Katika Jimbo langu na Wilaya yangu ya Muleba Wizara zote zinafanya kazi nzuri isipokuwa Wizara moja tu ambayo badala ya kutuletea kicheko wanatuletea kilio na hiyo si wengine ni watu wa NARCO, hawa wanatuletea kilio kwenye Jimbo langu la Muleba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa barabara; Mheshimiwa Waziri tumeongea sana hii barabara ya Muleba – Muhutwe – Nshamba - Muleba ni barabara yenye kilometa 54 tangu awamu ya nne tumekuwa tukijenga hii barabara kipande kwa kipande. Mheshimiwa Waziri uliniahidi kwamba mwaka huu, mwaka jana nilikuona lakini mwaka huu ukasema barabara hii tutaipatia kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma bajeti yako Mheshimiwa Waziri nimekuta umetupatia kilometa sita tu, Mheshimiwa Waziri kwa kilometa sita tutaimaliza barabara labda tutachukua miaka 50. Chonde chonde Mheshimiwa Waziri hebu angalia kwenye bajeti yako Mheshimiwa, hii barabara imejengwa kwa muda mrefu, tunaomba katika awamu hii tumalize hii barabara huu wimbo tufunge ukurasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii nimesoma mmetutengea pesa kwa ajili ya madaraja mawili Kyabakoba na Kamashango na haya ni madaraja makubwa ambayo katika Bonde la Mto Ngono. Lakini kilichowekwa pale tumeweka feasibility study, upembuzi yakinifu sijui na usanifu nini. Lakini na hii mwaka jana ilikuwa imetengewa pesa kwa ajili ya usanifu na upembuzi yakinifu, lakini hakuna kilichofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaimani kubwa na Waziri ninaimani kubwa watendaji wa Wizara hii, ni watu makini, Mtendaji wa TANROADS Engineer Aisha Amour ninamuamini na utendaji wa kazi unaonekana, Ndugu yangu Migire nawaamini sana. Nawaomba barabara hii na madaraja haya mawili tukayamalize mwaka huu. (Makofi)
Lakini kuna daraja lingine mmelisahau Mheshimiwa Waziri kuna daraja la Marahara na lenyewe linahitaji kufanyiwa kazi kwa sababu ni sehemu ya hiyo barabara. Ninatumaini kwa kazi na mwendo wenu hii kazi mtaifanya na itakamilika kwa wakati.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Mtendaji wa TANROADS Engineer Mativila na Katibu Mkuu ndiyo Engineer Aisha, ahsante sana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Ishengoma.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunikumbusha na naipokea taarifa yake kumbukumbu zikae salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera na hususan Wilaya ya Muleba tuna visiwa 39 na katikati ya Ziwa Victoria tuna kata tano ambazo zinaundwa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na hizo kata mpaka tunaongea hazina usafiri wa uhakika. Lakini niishukuru Wizara inayo mpango wa kutuletea meli ya Clarias kuanzia Mwanza kwenda kutembelea visiwa vya Ziwa Victoria, niwashukuru. Lakini huo mpango wa kutuletea hiyo meli ulianza kuasisiwa tangu mwaka jana, lakini mpaka sasa tunavyoongea tunasubiria hiyo meli ianze kufanya kazi. Na taarifa nilizonazo ni kwamba tunaisubiri TASAC itoe okay ili meli hiyo ianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze Mheshimiwa Waziri kuwa wananchi wanaisubiria hiyo meli kwa hamu kubwa, tunaomba hao TASAC ambao wako chini ya Wizara yako kawahimizehimize najua watachangamka na najua ni vijana wazuri sana, wakatoe kibali hiyo meli ianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika kupanga utaratibu wa hiyo meli, awali ilikuwa itoke Mwanza iende Godziba, iende Kerebe, iende Bumbile iishie Kyamkwiki. Lakini tuna bandari yetu ndogo ya Katembe Magarini ambako tumepata kibali cha kuanzisha soko la kimataifa la kuuza dagaa. Kwa kuwa pale kuna mzigo mkubwa na hiyo bandari ndogo iko chini ya TPA na hapa tunavyoongea nawashukuru TPA wanaendelea kuijenga na kuikarabati hiyo bandari yao kwa sababu gati ilikuwa imezama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tutatengeneza pesa kwa sababu kuna mzigo mkubwa wa dagaa lakini itatusaidia ku-promote hata bandari yetu na soko letu la kimataifa ambalo limeanza kufanya kazi kwa sasa. Kwa hiyo naomba katika mpango wa awali tukaingize na hiyo kituo cha Katembe Magharini ili hiyo meli yetu tutapoanza na kuchakata na kufanya kazi itoke Katembe Magarini na mzigo wa dagaa ikawalishe watu wa Mwanza. Tutakuwa tumefanya biashara, lakini tutakuwa tumeongeza kwa ajili ya Wilaya yangu ya Muleba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Katemba Magarini watu wa TEMESA tangia mwaka jana wamekuwa wanasema wanajenga gati kwa ajili ya kuegesha vivuko kwa ajili ya Katembe Magarini hadi Ikuza. Lakini na huu umekuwa wimbo wa Taifa Mheshimiwa Waziri na hakika kwenye bajeti hii na hapo kwenye bajeti yako umeitaja na umeitengea pesa. Naomba sasa hii kazi ifanyike na ikamilike kwa wakati ili wananchi wetu waendelee kufaidi matunda ya uhuru wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho. Ndugu yangu Kyombo ameongelea uwanja wa ndege wa Omukajunguti. Nimeona kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri ametenga pesa kwa ajili ya kujenga jengo la VIP uwanja wa ndege wa Bukoba, kukarabati mita 200 kuongezea njia ya kuruka na kutua ndege na kuongeza kujenga taa za kuongozea ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kutupatia hivyo vyote, lakini kwa wakati tulionao ukichukua mazingira ya Mkoa wa Kagera, mahitaji ya sasa ya Mkoa wa Kagera tunahitaji uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Omukajunguti, huu uwanja tuendelee kufanya haya tuliyoyafanya lakini kule kutokana na jiografia ya Mkoa wa Kagera, Kagera sasa baada ya DRC kuingia Afrika Mashariki tutakuja kuleta hoja hapa Kagera ndiyo ipo katikati ya Afrika Mashariki kwa sasa. (Makofi)
Kwa hiyo tutahitaji uwanjwa wetu wa Omukajunguti na tutaendelea kuisemea na tunaomba Mheshimiwa Waziri na leo wakati tuko mapumziko nimeongea na Mtendaji wako kijana machachari Wakili Mbura. Tukaliongelea hili akasema watakwenda kuliangalia, nakuomba Mheshimiwa Waziri mliangalie uwanja wa ndege wa Omukajunguti ni wa siku nyingi na wakazi wa Mkoa wa Kagera tunahitaji uwanja huo. Naendelea kuwashukuru kwa utendaji mzuri wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni la utawala bora; Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina taasisi zake ambazo zinafanya kazi vizuri, lakini na taasisi nyingine ndogo ambazo ziko chini ya Wizara ya Uchukuzi; moja iko chini ya LATRA na nyingine iko chini ya TCAA. Tuna mabaraza ya ushauri wa watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na mamlaka hizo. Lakini kwa bahati mbaya nilikuwa naangalia bajeti na huu umekuwa uzoefu wa muda mrefu sana hayo mabaraza hayatengewi bajeti, yanabaki kwa utashi wa Wakurugenzi ambao wanaongoza hizi mamlaka, na matokeo yake imekuwa kwamba Mkurugenzi akikuangalia vibaya asubuhi ataamua akutengee kiasi gani cha pesa.
Nashukuru Wizara ya Mawasiliano huwa wanawatengea pesa, Mheshimiwa Waziri unajua mchakato tuliyokuwa nao na ugumu tunaopitia na hizi taasisi ndogo ndogo naomba kuanzia labda bajeti ijayo nashauri tu haya mabaraza yatengewe bajeti na tuione kwenye bajeti ya Serikali inayoletwa hapa Bungeni kwa sababu na zenyewe ni taasisi za umma. Hatuwezi kuziacha mtu mmoja apange bajeti kwa ajili ya hizi taasisi ni makosa makubwa Mheshimiwa Waziri.
Kwa hiyo nashauri na kupendekeza haya mabaraza yanafanya kazi kubwa, yanafanya kazi nzuri ya kuelimisha umma na yenyewe tuone bajeti yake katika haya, kwa sababu na yenyewe yanakuwa audited na CAG, kwa hiyo, wana wajibu na wana haki ya bajeti yao kuonekana hapa. Yameanzishwa kwa sheria na yanafanya kazi yana bodi zake lakini nashangaa kwa nini yabaki huku yakilelewa na mtu mmoja ambaye wakati mwingine anaamua tu kuya-suffocate na kufanya anavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo kwa kazi nzuri wanayoifanya nawaunga mkono hoja na naomba Wabunge wenzangu tuunge mkono hii bajeti ipite waende wakafanye kazi, nashukuru sana. (Makofi)