Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi, lakini namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ambayo ametupa nafasi ya kuweza kujadili Wizara hii ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nijielekeze kuipongeza Serikali kwa mpango mkubwa wa reli ya SGR ambao unatoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza, nimeona kuna lot kama tano ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi. Kila lot iko kwenye hatua fulani hatua za mwisho, ziko kwenye manunuzi, lakini naomba tu niseme wazi kwamba pamoja na lot hizi inatakiwa tunapotengeneza SGR hii tuone namna Wizara zingine zinavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Wizara yetu ya Kilimo imeongezwa fedha, kwa hiyo, tunaamini kabisa kwamba kuna mazao mengi yanakwenda kuzalishwa kwenye umwagiliaji yatahitaji kupata hii miundombinu ya reli ili yaweze kufanya biashara. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hili kwa sababu ninaamini kabisa uzalishaji huu utahitaji kuitumia reli hiyo. Lakini nipongeze tena meli ambazo nimeona meli moja inasemwa iko asilimia 60 ya Ziwa Victoria, MV Mwanza ambayo mkataba ulikuwa unaonesha kwamba ingekamilika mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu Mheshimiwa Waziri utakaposimama pamoja na nia njema ya kutengeneza meli hii utuoneshe kwa sababu mwaka huu hatuna uhakika kama asilimia 60 itaweza kumalizika kwa mwaka huu wa fedha. Niombe sana uweze kuonesha hilo ili tuweze kujua kwamba watu wetu wataanza kuhudumiwa na meli hii ya MV Mwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa ujenzi wa Daraja la Busisi Kigongo daraja hili limeendelea kujengwa, lakini naiona kama kasi yake ni ndogo, sasa ni ombi langu na niombe kuishauri Serikali iweke usimamizi wa kutosha kuhakikisha kwamba daraja hili linakamilika kwa muda wake ili wananchi wa Kanda ya Ziwa waweze kupata nafasi ya kuvuka sehemu ile ya maji kwenda Geita, kwenda Bukoba na maeneo mengine ambayo yanaweza kuwa na nchi za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze Mheshimiwa Rais japokuwa kwenye hatua za kwanza mradi wetu wa Rais wa barabara ya kutoka Katoro kuelekea Ushirombo tunategemea unaanza sasa kwamba Bilateral Agreement imeshafanyika na sasa tunatarajia tu kwamba ile technical aspect ya wataalam wetu kutoka kwenye Wizara wataendelea kushughulikia kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa kwa wakati na wananchi wanapata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze sana Mhandisi Nnko ambaye amekuwa pamoja nasi Mkoani Geita barabara nyingi ambazo anasimamia sasa zinapitika. Niombe tu fedha hizi ambazo zinaonekana zinapitishwa kwenye bajeti hii ziendelee kwenda kule kwa ajili ya kuhakiksiha kwamba wananchi wetu barabara hizi za TANROADS zinaendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko moja ambalo sio la barabara, niwapongeze sana ATCL kwamba tulikuwa na shida kama Wabunge unaweza ukaitwa kwenye Kikao cha Halmashauri hapa kutoka Bungeni ikawa changamoto lakini wameanzisha route nzuri ya kutoka hapa kwenda Kanda ya Ziwa ya ndege ambayo inatuchukua hapa kutoka Dodoma kwenda Mwanza na baadaye unaweza kwenda kwenye vikao na baadaye ukaweza kurudi niwapongeze sana kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na pongezi zote nilizozitoa sisi kwa maana ya Jimbo la Busanda tumekuwa na changamoto ya barabara ambayo kama wenzangu wanavyosema imeingia kwenye Ilani kila mwaka, kila miaka mitano inakuja lakini haitengenezwi; barabara hii tumekuwa tunaiuliza hapa kila siku barabara hii inatoka Geita - Nyankumbu kwa Mheshimiwa Kanyasu inatakiwa ipite Nyarugusu, ipite Bukoli iende Bulyanhulu pale Kakola halafu iende Kahama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inashughuli nyingi sana za uchumi kwa watu wa Geita watu zaidi ya milioni mbili wanatakiwa kupita kwenye barabara hiyo, lakini barabara hiyo inapita kwenye migodi midogo midogo mingi maana yake tukiijenga barabara hii watu wetu watapata urahisi wa kufanya shughuli za kiuchumi. Lakini itakuwa ni barabara inayoturahisishia sisi kwenda Dar es Salaam na nchi za jirani kwa maana ya Burundi na Rwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana mwaka jana niliona ilikuwa imetengewa bilioni karibu tatu, mwaka huu sasa bahati mbaya imetengewa bilioni mbili, maana yake yenyewe kila mwaka pesa yake inazidi kupungua. Kwa hiyo, nikiambiwa ni-predict mwakani itatengewa bilioni moja na mwaka kesho kutwa itakuwa imetengewa sifuri. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri badala ya pesa hii kuonekana inapungua iende inaongezeka na kila tunapoweza kufanya tuisaidie barabara hiyo iweze kujengwa kwa lami kwa ajili ya uzalishaji wa watu wa barabara ile. Ni barabara inayokuja Dar es Salaam na watu wa Geita ni barabara inapitisha makinikia, ni barabara inapitisha mazao mengi ya kutoka Geita kwenda maeneo mengine. Niombe sana Mheshimiwa Waziri utusaidie barabara hii iweze kujengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho kabisa ni barabara hii ya kutoka Mwanza kwenda Bukoba kwenda Chato. Ilipokuwa inajengwa inapita kwenye eneo langu la Katoro, maana yake Jimboni Busanda walisahau kuweka taa, nafikiri wakati huo lot zilikuwa hazitembei na taa kwa hiyo, ukifika eneo lile kuna giza. Niombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii, japokuwa sikuona mahali popote, eneo hilo liwekewe taa ili barabara ile kwenye eneo hilo ambalo ninalisema la kuanzia Kibingo kwenda mpaka Buseresere liwekewe taa ili wananchi waweze kuona, waweze kufanya shughuli zao sio ikifika saa 12:00 jioni biashara imekwisha, iendelee kwa muda kwa sababu kuna taa za barabarani zinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mengi ya kuzungumza, lakini Mheshimiwa Waziri naomba haya machache kwa leo yatoshe kufanya bajeti hii niiunge hoja. Ahsante sana. (Makofi)