Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa dakika tano za kuchangia Wizara ya Ujenzi. Nami kwa kifupi nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS. Kama utakumbuka vizuri nilikuwa na mgogoro mkubwa wa barabara yangu ya Ifakara Kidatu kiasi cha Kwenda, siyo kuruka sarakasi lakini kwenda kukaa kwenye matope. Hivi ninavyozungumza na wewe lile eneo tulilokaa kwenye matope lina kilometa 20 za lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napenda kuwapa taarifa wananchi wangu kwamba, katika kilomita 66.9 zile ambazo tulikuwa na mgogoro mkubwa…
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa mnaotoka, Waheshimiwa sitaki kutaja majina ila mtoke kwa nidhamu na staha ya kibunge.
Mheshimiwa Asenga endelea.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunilindia dakika zangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli bila unafiki na kwa dhati ya moyo, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Makame Mbarawa kwa kuja Jimboni kwangu mara mbili kufuatilia barabara hii ya Ifakara - Kidatu ambayo ni barabara muhimu sana kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Waziri alivyofika Ifakara na Kilombero, ukweli ni kwamba changamoto kubwa ya barabara hii na nimemwomba Katibu Mkuu Engineer Aisha Amour na Engineer Mativila watusaidie kero kubwa ya fidia. Fidia ya barabara hii kwa wananchi wa Mbasa, Katindiuka, Mlabani mpaka kutokea Lipangalala imekuwa ni kero kubwa. Hivi ninavyozungumza wananchi walikuwa wanataka kuja Dodoma kufuatilia fidia yao, kwa sababu takriban miaka minne sasa wamewekewa alama na bila kulipwa fidia yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naona anashika kalamu pale anaandika, namwomba sana atusaidie kero hii kubwa na nimewasiliana na Meneja Razak wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, amenijibu majibu mazuri kwamba wanafanya upembuzi upya ili kupata thamani ya sasa ya fidia kwa wananchi hao. Meneja wa TANROADS Mkoa ni bwana mdogo, anafanya kazi nzuri na tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tunapenda kushukuru pia Waziri alipokuja Kilombero ametupatia taa za barabarani katika Mji wa Ifakara. Ifakara Mjini sasa kuna barabara ya TANROADS inayopita pale, ina msongamano mkubwa ndiyo maana tunasisitiza kuhusu barabara ya mchepuko, lakini Mheshimiwa Waziri ametupatia taa za barabarani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu la pili, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, baada ya ombi la fidia kwa wananchi wetu wa Mbasa, Katindiuka na Mlabani ni ombi la kuchukua barabara ya roundabout ya Kibaoni kuelekea TAZARA kwa kuwa Wizara hii ni ya Uchukuzi pia, TAZARA yetu ya kibaoni ina hali mbaya. Naomba wachukue ile kilomita 2.5 ambayo nimemwomba pia Katibu Mkuu Balozi Engineer Aisha Amour kutoka roundabout ya Kibaoni kuelekea mpaka TAZARA kwa sababu TAZARA ni yao. Ile barabara inapita stendi yetu ya Kata ya Kibaoni, stendi yetu ambayo tunaitumia kama ya wilaya, tunaomba sana watusaidie kuchukua barabara hiyo ili tujenge hata kwa lami nyepesi ili iweze kupitika wakati wote na wananchi wanaokwenda kupanda treni kuelekea TAZARA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema Wabunge wengine wa Mkoa wa Morogoro, naomba kusisitiza, kama tunavyosema Mkoa wa Morogoro katika kilimo ni ghala la Taifa, ni wazi kuwa amesema Mheshimiwa Kunambi hapa pacha wangu wa Jimbo la Mlimba, kwamba sisi ni wakulima wazuri, tunalima mpunga wetu mzuri, ubwabwa wetu mzuri, mama Aleksia amesema hapa. Hata hivyo, bado mkoa wetu na hasa kiungio kama Jimbo la Ifakara, Jimbo la Kilombero, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, haujaunganishwa na mikoa mingine. Waziri akimsaidia barabara Mheshimiwa Kunambi akitokea Njombe lazima atapita Ifakara. Akimsaidia barabara Mheshimiwa Antipas wa Malinyi, lazima atapita Ifakara kwenda Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkimsaidia Mheshimiwa Salim wa Ulanga lazima apite Ifakara kwenda Lindi. Kwa hiyo tunasisitiza sana, tunajua kuna upungufu wa bajeti, lakini kwa kweli katika hali ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha kwamba tunaunganisha mikoa na mikoa mingine, tunaomba tuwe na mkakati mzuri wa kuhakikisha Mkoa wa Morogoro unaunganishwa na Lindi, Ruvuma na Njombe. Naomba kusisitiza sana hilo, sitaki kusema mambo mengi hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia hapa kwa kumshukuru Waziri kwamba katika kilomita 66 za Ifakara - Kidatu sasa tuna kilomita 21 zinaenda kuwekwa lami. Narudia kusisitiza Mheshimiwa Waziri Profesa Makame Mbarawa suala langu la fidia, ombi langu nasisitiza chonde chonde, fidia kwa wananchi wetu wa Kata za Mbasa, Mlabani, Lipangalala na Katindiuka wamesubiri sana, imeshapita miaka minne, naomba Waziri alichukue na hiyo barabara ya kilomita 2.5 kutoka roundabout ya Kibaoni kuelekea TAZARA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)