Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Kwanza naomba kuwaasa tu Waheshimiwa Mawaziri wanaposhauriwa au tunapokosoa udhaifu wao wasipende kuunganisha hoja zetu na kusema kama tunampinga Mheshimiwa Rais au tunakipinga Chama au tunaipinga Serikali, wajibu wetu sisi Wabunge ni kuishauri Serikali na kuisimamia vilevile. Kwa hiyo tu na kila sababu tunapokuja kuchangia hapa basi tukijenga hoja isije ikaunganishwa moja kwa moja kwamba Wabunge tunaipinga Serikali yetu, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja kama tatu hivi, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alipoteuliwa mara ya kwanza kabisa aliahidi kujenga uwanja wa ndege wa Sumbawanga Mjini, ilipita kwenye bajeti hapa nasi tukapitisha. Wananchi wa Sumbawanga walifurahia sana kwa kuwa mwaka huu tulisema tunajenga uwanja wa ndege, akatoka Mheshimiwa Waziri Mbarawa akaja Waziri mwingine tukapitisha bajeti hiyo hiyo ya kujenga uwanja wa ndege Sumbawanga katoka Waziri kaja Waziri mwingine karudi tena Waziri Mbarawa Waziri wa Nne huyo hatujajenga uwanja wa ndege Sumbawanga na bajeti tunaipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niulize hoja yangu ya msingi kwamba tuko hapa Bungeni tunapitisha bajeti ili ikafanyiwe kazi au tuna- buy time au tunataniana, maana yake mwisho wa siku tunapitisha bajeti lakini mpaka leo mwaka wa tano uwanja wa ndege Sumbawanga hata nusu kilometa haujawahi kujengwa. Sasa ninamuomba Mheshimiwa Waziri kwamba ni miongoni mwa Wabunge ambao na mimi nitashika Shilingi kwamba nisipopata majibu ya msingi lini uwanja wa ndege unaanza kujengwa na kama haupo tuuondoe kwenye bajeti tusisema kitu ambacho hakipo, mwisho wa siku wananchi kule wanatuona sisi hatufai kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ukija uje na majibu lini sasa Uwanja wa ndege utaanza kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili ni kwamba tumekuwa tukilia sana kuhusiana na usafiri wa maji ndani ya Lake Tanganyika, huu ni mwaka wa Tatu au wa Nne hakuna usafiri wa meli ndani ya Lake Tanganyika, usafiri wao ni maboti, wananchi wanakufa siku hadi siku lakini kila tukija hapa wanasema fedha tumetenga za kujenga meli, sasa tunasema hiyo meli mpya hatuiihitaji sasa hivi warekebishe meli zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza jana nimeona wanakarabati meli ya MV Sangara - meli ya mafuta, wanashindwa kukarabati meli ya kubeba abiria wanakarabati Meli ya kubeba mafuta, ndani ya Lake Tanganyika hakuna hata meli moja inayotembea mpaka sasa hivi, watu wanakufa hakuna anayewajali lakini mwisho wa siku meli ya MV Liemba ambayo ni meli ya kihistoria mpaka leo imesimama, tumelia hapa Mkandarasi amepatikana mwisho wa siku Mkandarasi hayupo amepotea. Sasa hivi tunatafuta Mkandarasi mwingine naye hajulikani lini atakuja, sasa mimi nafikiri labda tuna bahati mbaya Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila jambo tunalolipigia kelele hapa tunaambiwa litafanyika, litafanyika mwisho wa siku tukija hapa tukitaka kupinga tunaonekana sisi tunapinga na Serikali yetu, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri umekuwa ukituahidi sana, sasa ifike mwisho mtuambie Meli itajengwa au haitojengwa, meli itakarabatiwa au haitokarabatiwa sisi wananchi tujichange fedha kidogo kidogo kule tununue meli yetu. Au tutumie hata ungo sasa kusafirisha abiria wetu ambao wanahangaika na wanakufa siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inasema inakuja kujenga meli ya tani 2,000 ya mizigo na meli ya tani 800 ya abiria, nilishauri hapa kwamba ukijenga meli ya tani 2,000 utabeba mzigo wa nani ndani ya ziwa Tanganyika? Tukashauri kwamba hii meli kwa nini tusijenge ya tani Elfu Moja Moja ili zikafanya kazi kwa wakati, zikawa zinapishana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mfano mzuri kabisa, kuna meli ya Amani ya Congo haitembei kwa sababu mizigo hakuna tani 2,000 nani atapakia? Nafikiri hapa kuna mawazo ambayo siyo sawa wanafikiria Kalemi ile ni kubwa kama Dar es Salaam, Kalemi ni dogo kuliko Kigoma, kwa hiyo ukitengeneza meli ya tani 2,000 hautapata mzigo wa kubeba kwa wakati mwisho wa siku meli itakaa bandarini kama meli ya utalii, watu watakuwa wanakwenda wanaishangaa wanaondoka lakini mizigo hamtopata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ushauri wangu Mheshimiwa Waziri badala ya kujenga meli ya tani 2,000 tujenge meli mbili za tani elfu moja moja ambazo zitakuwa zinapishana kwa wakati na zinafanya kazi kwa wakati, ninakuomba sana jambo hili mlizingatie kwa sababu mimi nipo huko Lake Tanganyika na ninajua biashara za kule zinavyofanyika, kwa hiyo tukijenga meli ya tani elfu moja zikawa mbili zitakwenda kwa wakati na tutapata faida na wananchi watanufaika pia biashara itakwenda kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kumekuwa na vi-meseji meseji vinapita huko kuhusiana na ujengaji wa reli, kwanza naomba nikanushe maana Wabunge wengi wanasema hizi meseji ni Aeshi anaandika, hapana mimi siyo kigogo wala simjui na wala sijawahi kukutana naye, lakini taarifa hii inamhusisha na Waziri wa Fedha sasa nataka nitofautishe kidogo. Jambo hili lipo Wizara ya Uchukuzi halipo Wizara ya Fedha, hoja yangu ilikuwa ya msingi tu mimi sipingani na single source mliyotaka kuifanya, nashindana na utaratibu uliotumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili Bunge jamani naomba mnielewe kidogo, unajua mwisho wa siku tukisema jambo kuna watu wanafikiria labda kuna jambo limepita, kuna rushwa imefanyika, au Mbunge amepewa fedha naomba nilikanushe hili. Mimi nipo kwenye Kamati ya Miundombinu ninajua kila kitu kinachoendelea ndani ya Kamati, kwa hiyo taarifa ninayoitoa ninaitoa ambayo nimeipata ndani ya Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi mliyempa yule ambaye anajenga kutoka Isaka kwenda Mwanza haja-perform vizuri na hadi leo amejenga kwa asilimia Nne japokuwa kwenye taarifa tumeambiwa amejenga kwa asilimia Nane siyo kweli! Sasa huyohuyo Mkandarasi, hoja yangu ya msingi ni kwamba kwanini mmempa kazi nyingine ya ziada kwa single source kwa muda mfupi ambapo kazi ya kwanza hajafanya vizuri ndiyo hoja yangu ya msingi hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba ukirudi utufafanulie kidogo inawezekana Wabunge hawa mkiwapa semina hivi wanajua mambo ni nini? mambo ni shwani, naomba niseme ukweli hili jambo la LOT Namba Sita ambayo mmeenda kuwapa wale wakandarasi …

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nami ni Mwanakamati wa Kamati ya Miundombinu, nataka nimpe taarifa mchangiaji anayezungumza sisi tumetembelea miradi na tumejiridhisha na kazi inayoendelea lakini jambo lingine ambalo nimpe taarifa ni kweli kumekuwepo na kampeni na mhusika ndiye amekuwa akipiga kampeni kupinga ile kampuni. Ninampa taarifa kwamba baada ya kuona hayo mambo yanaendelea sisi kama Kamati tumejiridhisha tumeita wahusika wametueleza kazi inavyoendelea na tenda hadi sasa hivi imeshatangazwa lakini mpaka sasa hivi hakuna Mkandarasi ambaye ameshapewa tenda. Kwa hiyo, ninampa taarifa mzungumzaji kampeni zake ambazo amekuwa akiendelea nazo siyo za kweli na Wabunge tumepewa semina na Waziri ametuhakikishia kuwa hakuna aliyepewa tenda hadi sasa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aeshi, taarifa hiyo.

MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo wale wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilihakikishie Bunge, kama upo tayari, uniruhusu nilete ushahidi kwa haya ninayoyasema mimi halafu na wao wajumbe hao wa Kamati wanaosema kwamba sisi tunafanya kampeni waje na ushahidi wao, halafu tuje tukae Bungeni tueleze. Kama nitakuwa nimesema uongo, hatua za Bunge zichukuliwe. Ila ninachojua mimi, tender ilitangazwa, mkandarasi akapatikana kwa single source na sasa hivi wapo kwenye evaluation. Sasa Mbunge, Mjumbe mwenzangu wa Kamati hujui kinachoendelea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Muda wako umekwisha, ni kengele ya pili Mheshimiwa Aeshi.

MHE. AESHI K. HILALY: …halafu unakuja kunipa mwongozo. Mwongozo wako siupokei, isipokuwa naishauri Serikali; namshauri Mheshimiwa Waziri mwangalie jambo hili lisije baadaye likatu…